JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


MEYA KIBAHA KUTOA ZAIDI YA MILION 18 KUCHIMBA VISIMA VINNE KUPUNGUZA KERO YA MAJI PANGANI

Share This

Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha Disemba 22, 2025

Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Kidimu, Kata ya Pangani, Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wanakabiliwa na uhaba wa maji safi na salama hali inayowalazimu kutumia maji ya mtoni, madimbwi na kununua maji kwa wananchi wenye visima kwa gharama kubwa. Wakazi wa eneo hilo akiwemo Hawa Mkongwa na Suzy Lukiwa, wakizungumza wakati wa ziara ya Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, walisema licha ya kuwepo kwa mradi wa maji unaotekelezwa na Serikali wenye thamani ya shilingi bilioni 8.9, bado haujakamilika jambo linalosababisha kero kubwa kwa wananchi.

“Tunakosa muda mwingi kutafuta maji na mara nyingi tunayapata lakini si salama, Tunamuomba Meya atusaidie kupata maji ya uhakika wakati tukisubiri kukamilika kwa mradi mkubwa,” 

Diwani wa kata ya Pangani, John Katele alieleza kwa sasa hakuna mbadala wa maji safi na salama hivyo wananchi wanalazimika kutumia maji yasiyo salama.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkombozi, Jackson Msaki maarufu kama Chuma, alieleza, Shule ya Msingi na Sekondari Mkombozi zina maji ya kisima, huku Kituo cha Afya Mkombozi kikiwa hakina maji na hulazimika kuchota maji katika shule ya sekondari. 

Chuma aliongeza kuwa visima hivyo vilichimbwa kwa ufadhili wa Mfadhili kutoka Uturuki, ambapo kila kisima kiligharimu shilingi milioni 4.5.

Akijibu kero hiyo, Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas, alieleza wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kukamilisha mradi mkubwa wa maji, Ofisi ya Meya itatoa fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima vinne katika mitaa ya Pangani, Kidimu, Mkombozi na Lumumba.

Alisema tatizo la maji limekuwa sugu kwa muda mrefu hivyo mpango huo wa muda mfupi utasaidia kupunguza adha wanayoipata wananchi.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka matokeo ya haraka,Sisi tuliopewa dhamana tunapaswa kushuka kwa wananchi, kuwasikiliza na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zao badala ya kuleta bla bla,” alifafanua Nicas. 

Naye fundi kutoka DAWASA, Joseph, alisema mradi mkubwa wa maji Pangani utakuwa suluhisho la kudumu la tatizo hilo.

Alibainisha mradi huo utasambaza maji katika mitaa sita pamoja na maeneo ya jirani na utahusisha ujenzi wa tanki kubwa la maji lenye ujazo wa lita milioni sita.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha ambaye pia ni Afisa Utumishi, Mrisho Mlela, alimshukuru Meya kwa maelekezo aliyotoa na kusema kuwa zoezi la uchimbaji wa visima litaanza rasmi Disemba 23, 2025.

Meya Dkt. Nicas ameanza ziara ya kutembelea kata zote 14 za Manispaa ya Kibaha, akianzia Kata ya Pangani, kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi uso kwa uso na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad