JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


KAMISHNA MKUU TRA AWAOMBA WAFANYABIASHARA NA WASHAURI WA KODI KUZINGATIA MAADILI NA WELEDI ILI KUIMARISHA UTII WA KODI

Share This

 

Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, akizungumza na  wafanyabiashara pamoja na washauri wa walipakodi  jijini Dar es Salaam.


KAMISHNA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, ametoa wito kwa wafanyabiashara pamoja na washauri wa walipakodi kuimarisha maadili, uaminifu na weledi katika utoaji wa huduma zao, ili kujenga mazingira salama, shindani na yenye utii wa kodi kwa manufaa ya uchumi wa taifa.

Hayo ameyasema leo Desemba 12, 2025 wakati akizungumza katika kikao maalum na wataalamu hao, Kamishna Mwenda aliwakumbusha kuwa nafasi yao katika mfumo wa kodi ni nyeti na ina athari kubwa kwa ustawi wa biashara nchini.

Amesema kuwa licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kurahisisha biashara na kuongeza utii wa hiari, bado kunahitajika kutumia utaalamu wao kwa njia inayolinda uadilifu kuliko kusaidia ukwepaji kodi au kutoa taarifa za kupotosha.

Amesisitiza kuwa vitendo hivyo vinaharibu sifa ya sekta, vinapunguza mapato ya serikali, na kuvuruga uwanja sawa wa ushindani kwa wafanyabiashara wanaofuata sheria.

Kamishna Mwenda amesema baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika ukusanyaji wa kodi zimekuwa zikichangiwa na washauri wachache wanaowasilisha taarifa zisizo sahihi kwa niaba ya wateja wao au wanaoshiriki moja kwa moja katika vitendo vya smuggling. Ameeleza kuwa tabia kama hizo haziwezi kufanyika bila ushirikiano kati ya baadhi ya maafisa wasio waadilifu na wataalamu wa kodi wenye maslahi binafsi, hali ambayo imekuwa ikihatarisha uaminifu katika mfumo wa kodi.

Aidha, ametoa rai kwa washauri wa kodi kujitambua kama watu wanaotekeleza wajibu wa umma (public officials) kwa kuwa wanahusika moja kwa moja katika kuhakikisha taarifa zote muhimu za walipakodi zinawasilishwa kwa ukweli na kwa wakati. Amesema hatua hiyo itasaidia si tu kuongeza mapato ya serikali, bali pia kuimarisha mazingira ya biashara na kuondoa malalamiko ya viwango vikubwa vya kodi vinavyotokana na utii mdogo wa baadhi ya walipakodi.

Kwa upande wa wafanyabiashara, Kamishna Mwenda amewasihi kuepuka kutafuta njia za mkato kupitia washauri wasiokuwa waaminifu, kwa kuwa kufanya hivyo kunawaweka katika hatari ya kisheria, kunaharibu taswira ya biashara zao na kunachangia ushindani usio sawa katika sekta.

Amesema biashara inayofuata sheria ina nafasi nzuri ya kukua, kupata huduma bora kutoka TRA na kuongeza uaminifu wa masoko ya ndani na nje.

Aidha, katika kuelekea msimu wa mwisho wa mwaka ambapo biashara na uingizaji mizigo huongezeka, Kamishna Mwenda amewataka washauri wa kodi na wafanyabiashara kuendelea kushirikiana kwa karibu na TRA kwa kuwasilisha taarifa sahihi za bidhaa, kuepuka hofu zisizo na msingi na kufanya maamuzi kwa uadilifu.

Amesema ushirikiano huu utasaidia kuondoa misuguano, kujenga uaminifu na kuhakikisha shughuli za Desemba hazitetereki.

Kamishna Mwenda amewahimiza wadau hao kutoa maoni ya kuboresha mahusiano kati yao na TRA, huku akiweka msisitizo kuwa maadili na weledi ndiyo msingi wa kuongeza wigo wa walipakodi bila kuongeza viwango vya kodi.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekutana na washauri wa kodi na wafanyabiashara kwa lengo la kuhamasisha utii wa kodi, kuboresha mawasiliano, na kujadili changamoto zinazowakabili walipakodi kuelekea mwisho wa mwaka wa fedha unaoishia Desemba 31, 2025. Kikao hicho, kilichoongozwa na Kamishna Mkuu wa TRA, kililenga kuhakikisha walipakodi wanawasilisha marejesho yao kwa usahihi na kwa wakati ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya nchi na uendelevu wa biashara.

Mfanyabiashara, Melkzedek Festo, amesema kikao hicho kimetoa mwelekeo mpana kuhusu wajibu wa walipakodi katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, hususan kwa biashara zinazotumia kalenda ya Januari hadi Desemba.

“Kamishna Mkuu amesisitiza umuhimu wa walipakodi kupitia faida halisi ya mwaka, kuhesabu kodi sahihi, na kuwasilisha returns pamoja na kulipa kabla ya tarehe 31 Desemba 2025,” amesema Festo.

Ameongeza kuwa walipakodi wanapaswa kurekodi kikamilifu mauzo yao kwa kutumia risiti za EFD, na kuhakikisha wanalipa kodi kwa wakati ili kuepuka riba na adhabu zinazoweza kujitokeza kutokana na ulipaji wa kuchelewa.

“Ukaribu kati ya walipakodi na TRA utasaidia kuongeza uelewa wa sheria za kodi na kuimarisha uwezo wa sekta kukusanya kodi kwa ufanisi,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Washauri wa Kodi Tanzania, CPA Victoria Alex, amesema mkutano huo ni hatua muhimu katika kuimarisha mahusiano kati ya washauri wa kodi na TRA, hususan katika kipindi hiki ambacho walipakodi wanajiandaa kukamilisha majukumu yao ya mwisho wa mwaka.

“Mawasiliano ni muhimu sana. Mkutano huu umetupa fursa ya kushirikiana kwa karibu na TRA ili kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari, ambayo ndiyo msingi wa kuimarisha uchumi,” amesema.

CPA Victoria amesema kupitia mkutano huo, washauri wa kodi wamepata ufafanuzi wa changamoto mbalimbali pamoja na nafasi ya kuwasilisha maoni yao moja kwa moja kwa Kamishna Mkuu.

“Jambo hili linasaidia serikali na TRA kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutatua changamoto za walipakodi. Lengo ni kuwa kwenye daraja moja katika kuwaelimisha na kuwahimiza walipakodi kutekeleza wajibu wao,” amesema.

Aidha, amesema washauri wa kodi wataendelea kushirikiana na TRA katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ili kuhakikisha walipakodi wanalipa kodi kwa wakati na kwa hiari, kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.

“Tumejipanga kutoa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha hakuna mlipaji anayekosa kutimiza wajibu wake kabla ya kuingia mwaka 2026,” amesema CPA Victoria




Baadhi ya Matukio mbalimbali wakati Kamishna Mkuu wa TRA akizungumza na wafanyabiashara pamoja na washauri wa walipakodi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad