Taasisi inayojihusisha na harakati za kijamii inayojulikana kama Hadithi Nzuri, kwa kushirikiana na kampuni ya WeMedia, imetekeleza tukio la WE GIVE BACK 2025, mpango wa ufikiaji wa jamii unaolenga kurejesha matumaini, hadhi, na fursa kwa watoto na vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi jijini Dar es Salaam.
Kadri ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na uhamiaji wa mijini unavyoendelea kuongezeka katika miji mikubwa ya Tanzania, WE GIVE BACK 2025 inaonesha dhahiri kwa kiasi kikubwa hali ya kutengwa inayowakumba vijana wanaoishi mitaani, pamoja na uwezo mkubwa walio nao endapo watapatiwa fursa na vikwazo vya kimfumo vitaondolewa.
Mpango huu uliwahusisha watoto na vijana 156 kutoka maeneo ya Kijitonyama - Sayansi, Ubungo, Coco Beach, Kinondoni - Morocco, na Kariakoo, ambapo wengi wao wameishi mitaani kwa kipindi kinachokadiriwa kati ya miezi mitatu hadi miaka 15. Utafiti wa Ripoti uliofanywa na mpango huu wa WE GIVE BACK kwa 2025 inaonesha kundi la vijana wenye umri mdogo, ujuzi, na ari ya kujenga upya maisha yao, lakini wanakwama kutokana na changamoto za kimfumo kama vile ukosefu wa vitambulisho vya Taifa au NIDA, makazi yasiyo na uhakika, upatikanaji mdogo wa mafunzo ya ujuzi, pamoja na kutofikiwa na mahitaji ya afya na msaada wa kisaikolojia.
“Kazi yetu kama Hadithi Nzuri huanza kwa kusikiliza,” alisema Bw. Baraka Peneza, Mwanzilishi wa Taasisi ya Hadithi Nzuri.
“Kwa kushiriki chakula pamoja, tunatengeneza maeneo salama ambapo watu huwa huru na kutuelezea wao ni nani, wanafahamu nini, na wana matumaini gani siku za usoni. Tunachoendelea kuona si kizazi kilichopotea, bali ni vijana wanaohitaji fursa, mwongozo, na mtu wa kuambatana nao katika safari ya maisha.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni washiriki wanne tu kati ya 156 waliokuwa na Vitambulisho vya Taifa (NIDA), wakati 86 wakihitaji kwa dharura kusajiliwa—hali inayokuwa kikwazo kikubwa katika ajira, mafunzo, na ujumuishwaji katika kijamii. Wakati huohuo, hamasa ya kushiriki mafunzo ya ufundi stadi kupitia VETA ilikuwa kubwa, hususan katika fani za udereva na masomo ya ufundi wa magari, TEHAMA, ukarimu na hoteli (hospitality), uchomeleaji (welding), na umeme.
Mbinu ya Hadithi Nzuri inaunganisha usimulizi wa hadithi na vitendo, ikitumia chakula kama daraja la kujenga imani na kubaini mahitaji kwa kina. Zaidi ya msaada wa haraka kama vile chakula, mavazi, viatu, blanketi, na mahitaji ya usafi, mpango huu unaweka kipaumbele katika ujumuishaji wa muda mrefu, ikiwemo msaada wa kupata nyaraka za utambulisho, njia za mafunzo ya ufundi, upatikanaji wa ajira, rufaa za afya, na mwongozo wa kihisia.
Ushirikiano na kampuni ya WeMedia uliimarisha uwezo wa mpango huu katika kurekodi manufaa na kutoa jukwaa kwa sauti ambazo mara nyingi hazisikiki na watu wengi.
“Hadithi Nzuri ipo kutukumbusha kuwa kila mtu anastahili kuonekana na kuungwa mkono,” aliongeza Bw. Peneza.
“Jamii zinapoungana, na hadithi zinaposimuliwa kwa uhalisia na heshima, mabadiliko ya kweli yanawezekana.”
WeMedia imeeleza kuwa ushirikiano huo unaenda sambamba na dhamira na maono inayoyasimamia. Kama kampuni inayosaidia chapa au makampuni mbalimbali kusimulia hadithi zenye kuleta tija, WeMedia iliiona mpango wa WE GIVE BACK 2025 kama fursa ya kurudisha kwa jamii kwa kusaidia kusimulia hadithi za watoto na vijana ambao sauti zao husikika mara chache—kuhakikisha wanaonekana, wanaeleweka, na wanapewa nafasi ya haki ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo kwenye jamii.
Washirika wa tukio hilo ambao ni Dough Works (KFC & Pizza Hut), Chemicotex (Tressa & Whitedent), GSM Beverages, Demichtoph, Tembomax, Ruby International, Keds Limited, Men-Men-Men the Podcast, na Code Studios, wanasema kuwa maarifa yaliyopatikana kupitia WE GIVE BACK 2025 yanaonesha hitaji la dharura la suluhu shirikishi zinazoongozwa na jamii husika, zaidi ya hisani zinazotolewa kwa muda mfupi ili kuwa na ujumuishi endelevu. Hadithi Nzuri inatoa wito kwa taasisi za serikali, vyuo vya mafunzo ya ufundi, waajiri, asasi za kiraia, na viongozi wa jamii kushirikiana kuondoa vikwazo vya kimfumo—hususan vinavyohusiana na upatikanaji wa vitambulisho, mafunzo ya ujuzi, na njia zenye hadhi za kuingia katika ajira na jamii.
Dira ya Hadithi Nzuri inabaki kuwa na Tanzania ambayo matumaini yanapatikana kwa kila mtu, na ambapo jamii zinaungana kusaidiana kabla ya kutafuta msaada nje.
MWISHO.
Kuhusu Hadithi Nzuri
Hadithi Nzuri ni taasisi ya harakati inayoongozwa na jamii za nchini Tanzania inayotumia usimulizi wa hadithi, kushiriki chakula, na kujenga imani ili kuwaunga mkono watoto na vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi. Kazi yake inalenga heshima, ujumuishaji wa kijamii, na suluhu zinazoongozwa na jamii husika, zinazokidhi mahitaji ya haraka na kuandaa njia za muda mrefu zitakazoleta fursa.












No comments:
Post a Comment