*Kongani za Viwanda Ni Moyo wa Dira ya maendeleo ya 2050.
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema kuwa ujenzi wa uchumi jumuishi unaozalisha ajira ndiyo msingi mkuu wa Dira ya Taifa 2050, na njia bora ya kulifikia lengo hilo ni kupitia ujenzi wa mitaa ya viwanda (industrial parks) nchini.
Hayo ameyasema leo Desemba 10, 2025 wakati akizungumza katika ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya Kwala Industrial Park (KIP) mkoani Pwani, Prof. Mkumbo amebainisha kuwa serikali inatekeleza kwa kasi maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye uchumi wa viwanda.
Amesema hadi sasa, Tanzania ina jumla ya mitaa ya viwanda 34 iliyosajiliwa, ikihusisha ushirikiano wa Mamlaka ya uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Taasisi ya Uwekezaji Tanzania (TISEZA), halmashauri za mikoa, pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara, Kwala Industrial Park ikiwa mojawapo ya miradi mikubwa zaidi nchini, imeendelea kupanuka kwa kasi.
Waziri Mkumbo amesema kwamba wakati alipotembelea eneo hilo mwaka jana kulikuwa na viwanda vitatu pekee, lakini leo kongani hiyo ina viwanda 20 vinavyoanza uzalishaji, huku malengo yakiwa kujenga zaidi ya viwanda 200 katika eneo hilo. Hadi sasa, uwekezaji wa takribani shilingi bilioni 25 umeishafanyika na tayari maelfu ya Watanzania wamepata ajira, huku kongani hiyo ikitarajiwa kutoa ajira zaidi ya 100,000 pindi itakapokamilika.
Katika ziara hiyo iliyohusisha mawaziri kutoka sekta za maji, nishati, Viwanda na Biashara pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani na wataalamu mbalimbali, serikali imetatua changamoto nne kubwa zilizokuwa zikiwakabili wawekezaji ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme, maji, miundombinu ya SGR, na masuala ya vivutio vya kodi.
Amesema serikali imekubaliana na wawekezaji kuwa katika kipindi cha wiki mbili watapatiwa megawati 4 kutoka Mlandizi, huku suluhisho la kudumu likiwa ni mradi wa ubia kati ya sekta binafi na serikali (PPP) kwa kuleta umeme wa kilovoti 220 kutoka Chalinze.
Vilevile, Wizara ya Maji imetoa maelekezo ya utekelezaji wa mradi wa maji unaogharimu shilingi milioni 25, ambao pia utatekelezwa kwa mfumo wa ubia na wawekezaji.
Kuhusu miundombinu ya usafirishaji, Prof. Mkumbo ameeleza kuwa Rais Samia tayari ametoa maelekezo ya kuifanya Kwala kuwa Bandari Kavu (Dry Port) kamili ili kurahisisha uingizaji na uuzaji wa bidhaa, huku Mkoa wa Pwani ukitekeleza maelekezo hayo.
Katika taarifa za uwekezaji mpya, Waziri Mkumbo ametangaza uwepo wa kiwanda kikubwa cha kutengeneza vifaa vya kuzalisha umeme wa jua (solar power panels) kinachomilikiwa na kampuni ya Tanzone. Kiwanda hicho, ambacho ni cha kisasa zaidi na kikubwa barani Afrika, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa kwa ajili ya masoko ya India na Marekani.
Kiwanda hicho kitawekeza zaidi ya dola milioni 300 mwanzoni, na kuanzia mwakani kitaongeza uwekezaji hadi dola milioni 500, sawa na takriban shilingi trilioni mbili (2)
Prof. Mkumbo ameongeza kuwa thamani ya mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda Marekani kupitia kiwanda hicho pekee itafikia kati ya dola milioni 300 hadi 600 kwa mwaka, kiwango ambacho kinazidi jumla ya mauzo yote ya Tanzania kwenda Marekani mwaka 2020.
Serikali pia imethibitisha kuanzishwa kwa kiwanda cha kwanza cha kuchakata chuma (steel processing) nchini, ambacho kitapunguza utegemezi wa kuagiza bidhaa za chuma na kuongeza thamani ya mazao ya ndani ya chuma.
Waziri Mkumbo amesema serikali inaendelea kuunga mkono kwa nguvu zote wawekezaji wanaowekeza nchini kwani mafanikio yao yanaleta tija kubwa kwa taifa kupitia kodi, ajira, na ukuaji wa uchumi.
“Sera na maono ya Rais Dkt. Samia kuhusu Tanzania ya viwanda si hadithi ni uhalisia unaoonekana. Tunalishukuru sana eneo hili kwa uwekezaji mkubwa, na tutaendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha mafanikio ya kila mwekezaji yanawezekana,” amesema Prof. Mkumbo.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kongani ya Viwanda ya Kwala, Janson Huang amesema kuwa ziara ya leo ya mawaziri wanne imekuwa na mafanikio makubwa katika kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na kituo hicho cha viwanda Afrika Mashariki.
Amesema kuwa majadiliano yalilenga kuharakisha upatikanaji wa miundombinu muhimu ikiwemo umeme wa uhakika, maji, reli, kituo cha abiria, pamoja na huduma za gesi ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji na kuvutia wawekezaji zaidi.
Amesema mradi huo unaoendelea kwa kasi umeanza miaka mitatu iliyopita katika eneo lenye ukubwa wa ekari 2,500, na tayari awamu ya kwanza yenye ukubwa wa kilomita mbili za mraba imeshakamilika ikiwa na miundombinu yote muhimu.
"Hadi sasa, jumla ya viwanda 15 vimejengwa ndani ya eneo hilo, baadhi vikiwa tayari vimeanza uzalishaji huku vingine vikiwa katika hatua za mwisho kukamilika. Miongoni mwa viwanda hivyo ni vya uzalishaji wa waterproofing materials, mafuta ya injini, nguo, friji, chuma, vifaa vya umeme wa jua
Huang ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa, ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa huduma kama umeme, maji na miunganisho muhimu kupitia wakala wa serikali wa uwekezaji, TISESA, chini ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji.
“Mpaka sasa kila kitu kinaenda vizuri, na Serikali imetuonyesha dhamira ya dhati kutuunga mkono ili kuhakikisha kuwa kituo hiki kinakuwa kitovu cha viwanda na ajira kwa Watanzania,” amesema.
Matukio mbalimbali katika ziara kwenye Kongani ya Viwanda Kwala Mkoani Pwani.


No comments:
Post a Comment