Babati, Manyara Desemba 19, 2025: Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga, leo Desemba 19, 2025 amezindua rasmi na kuhamasisha utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (NHIF) katika Mkoa wa Manyara, akisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kuwa na bima ya afya ili kupata huduma za matibabu kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
Uzinduzi huo umefanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) mjini Babati, na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wataalamu wa afya, wawakilishi wa mpango wa kitaifa wa Bima ya Afya kwa Wote pamoja na wananchi mbalimbali.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Sendiga amesema mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutimiza ahadi ya siku 100 za kuanzisha mfumo utakaohakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya.
“Mfumo huu unalenga kumwondolea mwananchi mzigo wa gharama kubwa za matibabu na kuhakikisha kila mmoja, bila kujali kipato chake, anapata huduma bora za afya kwa wakati,” amesema Mhe. Sendiga.
Aidha, amewaelekeza Wasimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Manyara kuhakikisha mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unatekelezwa kwa kuzingatia miongozo, kanuni na taratibu zilizowekwa, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali.
Sambamba na hilo, Mhe. Sendiga amesisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi na watendaji wote kwenda kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujiunga na mpango huo, ili waweze kunufaika na huduma za afya kwa uhakika.
Kwa upande wake, Bi. Janeth Kibambo, Mwakilishi wa Timu ya Kitaifa ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, amesema lengo kuu la mfumo huo ni kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na uwezo wa kupata huduma za afya katika vituo vyote vya umma na binafsi vilivyosajiliwa, bila kikwazo cha kifedha.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Andrew Method, ameeleza kuwa mkoa umejipanga kikamilifu kutekeleza mpango huo, akibainisha kuwa changamoto ya wananchi kushindwa kugharamia matibabu imekuwa kubwa, hivyo kuanzishwa kwa Bima ya Afya kwa Wote ni mwarobaini muhimu katika kuboresha sekta ya afya.
Dkt. Method ameongeza kuwa Mkoa wa Manyara uko tayari kuupokea na kuutekeleza mpango huo kikamilifu, kwa kushirikiana na vituo vyote vya afya na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na endelevu.
Uzinduzi wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote mkoani Manyara unatarajiwa kuongeza wigo wa upatikanaji huduma za afya, kupunguza vifo vinavyotokana na ukosefu wa matibabu kwa wakati, na kuboresha ustawi wa jamii kwa ujumla.













No comments:
Post a Comment