Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, ameushukuru uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kumhamasisha kuendelea kuchangia kupitia mpango wa hiari badala ya kutoa fedha zake, jambo ambalo amesema limekuwa na manufaa makubwa kwake binafsi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kugawa majiko ya gesi kwa baadhi ya mama lishe, baba lishe, wastaafu na wanachama wa NSSF mkoani Mbeya, Mhe. Itunda alisema awali alipata ushawishi wa kutoa fedha zake baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Songwe, lakini ushauri wa viongozi wa NSSF ulimsaidia kubadili uamuzi huo.
“Nilikuwa mwanachama wa NSSF, lakini baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Songwe, nilipata vishawishi vingi vya kutoa fedha zangu. Wapo walionishauri nifanye hivyo ili niwekeze kwenye biashara. Hata hivyo, NSSF walinishauri nisitoe michango yangu, bali niendelee kuchangia kwa hiari. Nilifuata ushauri wao na sasa mimi ni mchangiaji mzuri wa NSSF,” alisema Mhe. Itunda.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta ya hifadhi ya jamii, yaliyowezesha wananchi waliojiajiri kujiunga na kunufaika na mafao yote yanayotolewa na NSSF.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, aliwahimiza wananchi waliojiajiri kujiunga na kuchangia katika Mfuko huo ili kunufaika na mafao mbalimbali, ikiwemo mafao ya matibabu, uzee, na uzazi.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba kupitia NSSF kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye, akisisitiza kuwa hifadhi ya jamii ni msingi muhimu wa ustawi wa wananchi na maendeleo ya taifa.

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)



No comments:
Post a Comment