Kampuni ya Puma Energy Tanzania imezindua PumaGas jijini Dodoma, hatua inayoonyesha dhamira yake katika kuhakikisha suluhisho la nishati nafuu na ya uhakika kwa matumizi ya nyumbani na kibiashara nchini Tanzania.
Hatua
hii inadhihirisha uungaji mkono wa kampuni wa Mkakati wa Taifa wa
Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 2034), uliozinduliwa Mei 2024
na Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu Nishati
Safi ya Kupikia jijini Paris ulioandaliwa na Shirika la Nishati Duniani
(IEA).
Waziri wa Madini na Mbunge wa Dodoma Mjini, Mhe. Anthony
Mavunde, amehudhuria uzinduzi huo na kuipongeza kampuni hiyo kwa kuwa
mdau mkubwa wa kuunga mkono jitihada za serikali za kukuza na kuwezesha
upatikanaji wa huduma ya nishati safi nchi nzima na kuhakikisha ifikapo
mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Napenda kuwapongeza wadau wetu wakubwa wa huduma na bidhaa za
nishati nchini, Puma Energy Tanzania, kwa kuendelea kushirikiana na
serikali kuhakikisha wananchi maeneo mbalimbali wanafikiwa na huduma za
uhakika. Ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi ni muhimu katika
kufanikisha malengo ya kitaifa ya kukuza matumizi na kuhakikisha
upatikanaji wa nishati safi, hususani kwa maeneo ya vijijini ambayo bado
upatikanaji wake unakumbana na changamoto mbalimbali,” amesema Mhe.
Mavunde.
“Kiwango cha matumizi ya nishati safi nchini bado
hakiridhishi kitu ambacho kinaathiri taifa kwa kiasi kikubwa hususani
kimazingira na kiafya. Bado Watanzania wanategemea kuni na mkaa kupikia
wakati rasilimali za nchi zinatosheleza kuwafanya waachane na mazoea
haya. Uwekezaji huu wa Puma Energy Tanzania kupitia bidhaa yenu ya
PumaGas utakuwa chachu ya kuwapatia wananchi chaguo rahisi na la uhakika
la nishati kwa matumizi ya nyumbani na kibiashara.
Ninawaomba
pia uzinduaji wa huduma hii uendane na shughuli za utoaji elimu na
uhamasishaji kwasababu bado watu wengi wanadhahania kuwa nishati safi ya
kupikia ni gharama na sio salama. Kama serikali tuko nanyi bega kwa
bega kuhakikisha mnalifanikisha hili na kuwafikia wananchi wengi zaidi
hususani maeneo ya vijijini,” alimalizia Waziri wa Madini.
Uzinduzi
wa nishati safi ya kupikia ya Puma Energy Tanzania ni sehemu ya kampuni
hiyo ya kupanua wigo wa huduma hii ambayo kwa sasa inapatikana katika
mikoa ya Dar es Salaam na Pwani pekee.
Akielezea kuhusu uzinduzi
huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Bi. Fatma Abdallah
amebainisha kuwa wamejizatiti katika uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya
uhifadhi, maeneo ya manunuzi, pamoja na mawakala wa usambazaji wa
mitungi ya gesi.
"Uzinduzi huu unathibitisha dhamira yetu ya
dhati katika kuunga mkono serikali kufikia lengo lake la mabadiliko ya
suluhisho la nishati endelevu ambayo inaboresha afya ya umma na ustawi
wa kiuchumi kwa kizazi cha sasa na kijacho. Mkakati wa Upikaji Safi wa
Tanzania unalenga kufikia asilimia 80 ya watu kuhamia kwenye upikaji
safi na kutoa wito kwa sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika gesi safi
asilia,” ameelezea na kuongezea Bi. Fatma Abdallah, Mkurugenzi Mtendaji
wa Puma Energy Tanzania, “Gesi safi asilia ni njia salama, rahisi na ya
gharama nafuu ya kuzipa jamii zetu nishati; kuwezesha upikaji safi na
kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya nishati asilia za kupikia.
Mbali na matumizi ya nyumbani, gesi safi ya kupikia pia ni chanzo
muhimu cha nishati kwa matumizi ya kibiashara na viwandani, ikitumika
katika hoteli, migahawa, hospitali, shule na maduka makubwa.”
“Watumiaji
wa PumaGas wanahakikishiwa nishati mbadala ya uhakika, salama na bora,
ambayo itapunguza utegemezi wa nishati asilia za kupikia kama vile mkaa
na kuni, ambazo huchangia uharibifu wa mazingira. Hivyo, napenda
kuualika umma na wadau wengine kuungana nasi katika mpango huu katika
kupanua wigo wa upatikanaji wa suluhisho la nishati safi nchini kote,”
alimalizia Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania.
Wateja
wataweza kununua mitungi ya gesi katika vituo vyote vya huduma za kujaza
mafuta Dodoma, pamoja na mawakala wa uuzaji wa rejareja. Kampuni pia
inatarajia kuzindua maduka mawili ya kisasa ya PumaGas ambayo yatatoa
huduma za kisasa, yakiwa na huduma mbalimbali ikiwemo kujaza na
kubadilisha mitungi ya gesi, kuhakikisha watu hawakwami katika shughuli
zao za kila siku.
Kama hiyo haitoshi, kwa kuanza rasmi
upatikanaji wa huduma hii mpya jijini Dodoma, wateja watapatiwa ofa
mbalimbali pindi wanunuapo mitungi ya gesi ya ujazo tofauti kama vile
6kg, 15kg, na 38kg. Kwa kuongezea, pia kampuni inategemea kuzindua
huduma ya uuzaji wa uuzaji wa nishati kwa wingi au ujazo mkubwa kuanzia
200kg mpaka 20,000kg.
Mbunge
wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (katikati) akikata
utepe kuzindua mpango wa Nishati safi ya kupikia Mkoani Dodoma
inayoendeshwa na Puma Energy Tanzania. Kushoto kwake ni Mkurugenzi
mtendaji wa Puma Energy Tanzania Bi Fatuma Abdallah. Kulia kwake ni Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Alhaji, Mhe Jabir Shekimweri na watumishi
wengine wa Puma Energy Tanzania. Tukio hili lilifanyika leo jijini
Dodoma.
No comments:
Post a Comment