
MAMLAKA
ya Masoko ya Mitaji na Dhamana imetoa pongezi kwa Bodi, Menejimenti na
Wafanyakazi wa benki ya CRDB kwa kutupatia furaha kubwa katika sekta ya
masoko ya mitaji, kwa kuwa mauzo ya hatifungani ya Miundombinu ya Samia
yamepata mafanikio ya asilimia 215.4, ambapo kiasi cha Sh.bilioni 323.09
kimepatikana ikilinganishwa na Sh.bilioni 150 zilizopangwa kupatikana.
Aidha,
asilimia 63.64 ya mauzo ya hatifungani imetoka kwa wawekezaji mmoja
mmoja yaani na asilimia 36.36 imetoka kwa Kampuni na Taasisi.Kati ya
wawekezaji wote walioshiriki, asilimia 99.9 ni wawekezaji wa ndani yaani
na asilimia 0.1 ni wawekezaji wa kigeni..jpeg)
Hayo
yameelezwa leo Februari 18,2025 jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA)CPA. Nicodemus Mkama
wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya miundombinu ya Samia
katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.
Aidha amesema kuorodheshwa
kwa Hatifungani ya Miundombinu ya Samia, kunaongeza thamani ya
uwekezaji katika Hatifungani za Kampuni na Taasisi kwa asilimia 38.59na
kufikia Sh.trilioni 1.16, kutoka Sh.bilioni 837.31.
“Mafanikio
haya yana maana kubwa katika ustawi na maendeleo ya sekta ya fedha.
Kwanza, inaonesha imani waliyonayo wawekezaji kwa benki ya CRDB na
masoko ya mitaji. Pia masoko ya mitaji hapa nchini yamekuwa kivutio na
kutoa fursa za uwekezaji kwa wawekezaji mmoja mmoja; Taasisi; wawekezaji
wa ndani; na wawekezaji wa kimataifa.
“Tatu, kutokana na
mazingira wezeshi katika masoko ya mitaji, bidhaa mpya na bunifu
zinatolewa, hivyo kuwezesha Kampuni, Taasisi na benki kama CRDB kupata
fedha za kuendeleza na kukuza biashara; na kugharamia shughuli za
maendeleo, ikiwa ni pamoja na miundombinu ya barabara zilizo chini ya
TARURA zinazosimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
“Hivyo, tuna
kila sababu za kuipongeza Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wa benki ya
CRDB; TARURA; pamoja na taasisi na wataalamu katika masoko ya mitaji
waliowezesha kukidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Uuzaji wa
Hatifungani hii kwa umma.”
Ameongeza mafanikio hayo ni
uthibitisho wa mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kiutendaji
yanayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi madhubuti wa
Rais Dkt. Samia Saluhu Hassan huku akifafanua lengo kuu la Hatifungani
hiyo ni kuwawezesha wakandarasi wa ndani ambao wanafanya kazi na Wakala
wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) kuwa na uwezo wa
kifedha ili kutekeleza kwa ufanisi na kwa wakati miradi ya ujenzi wa
miundombinu ya barabara vijijini na mijini hapa nchini.
CPA Mkama
amesema utoaji wa hatifungani hiyo ni hatua muhimu katika utekelezaji
wa Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30 wenye
lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi.
Pia
amesema utoaji wa hatifungani hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya
Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwani fedha zilizopatikana
zitatumika kuwezesha kampuni za kandarasi zinazomilikiwa na watanzania
kutekeleza miradi ya miundombinu kwa wakati na kwa ufanisi; na wananchi
waliowekeza katika hatifungani hiyo watalipwa riba, hivyo kuinua vipato
vyao.
“Kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Miundombinu ya Samia kwenye soko la hisa la Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, kunawapatia fursa wawekezaji kuuza hatifungani zao pale watakapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi mengine.”
Aidha amesema uorodheshwaji wa hatifungani katika Soko la Hisa unawawezesha wawekezaji kujua thamani halisi ya hatifungani zao na kuwapatia fursa wawekezaji wapya kununua hatifungani hizo, ambapo wawekazaji hao watapata riba kama faida itokanayo na uwekezaji huo.
Ameongeza uorodheshwaji wa hatifungani katika soko la hisa unaongeza Utawala Bora na ufanisi katika uendeshaji wa Kampuni na kumwongezea mwekezaji wigo na fursa zaidi za uwekezaji.Hiyo inamsaidia mwekezaji kuwa na anuwai, jambo ambalo hupunguza athari za uwekezaji.
Pamoja na hayo CPA Mkama amesema CRDB ni miongoni mwa kampuni ambazo zinatumia vizuri fursa katika masoko ya mitaji na kuongeza benki hiyo imeuza hisa kwa umma na imeorodheshwa katika soko la hisa.
Pia benki hiyo imepata rasilimali fedha za zaidi ya Sh.bilioni 500 zilizotokana na mauzo ya bidhaa mbalimbali katika masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na Hatifungani ya Kijani na Hatifungani ya Miundombinu.CRDB ina leseni nne kutoka CMSA za kutoa huduma katika masoko ya mitaji.
Amesema kutokana na mafanikio hayo Benki ya CRDB inatekeleza mikakati ambayo inaleta mageuzi na mafanikio yenye tija katika utendaji wa benki, wanahisana masoko ya mitaji. Mathalani, Bei ya hisa za Benki ya CRDB imeongezeka kwa asilimia 366.7 kutoka Sh. 150 kwa hisa wakati wa mauzo ya hisa katika soko la awali, hadi Sh.700 kwa hisa, kwa Februari 17, 2025.
Amefafanua kama Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ilitoa idhini kwa benki ya CRDB kufanya mauzo ya Hatifungani ya Miundombinu ya Samia yenye thamani ya Sh.bilioni 150, kuanzia Novemba 29, 2024 hadi Januari 17,2025. Idhini hiyo ilitolewa na CMSA baada ya Benki ya CRDB kukidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana inayohusu utoaji wa Hatifungani kwa umma.
Aidha ametoa mwito kwa Benki zingine za Biashara, Taasisi za Fedha, kampuni binafsi, Taasisi na Mashirika ya Umma kutumia fursa zilizopo katika masoko ya mitaji kama ambavyo Benki ya CRDB na TARURA wametumia fursa ya kupata shilingi bilioni 323.09 kupitia masoko ya mitaji kwa kuuza hatifungani.





No comments:
Post a Comment