Na Saidina Msangi, WF, Karatu, Arusha.
Serikali
kupitia Wizara ya Fedha, imebainisha kuwa itaendelea na utoaji wa elimu
ya fedha na kuhamasisha utumiaji wa huduma za fedha vijijini ili
kuwawezesha wananchi katika maeneo ya vijijini kuwa na uelewa wa elimu
ya fedha pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya fedha na kuweka akiba.
Hayo
yamebainishwa na Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji
Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, wakati Timu ya
Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, iliyoambatana na Maafisa kutoka
taasisi na wadau mbalimbali ilipowasili kwa ajili ya kutoa elimu ya
fedha kwa wakulima, waendesha bodaboda na wafugaji, katika ukumbi wa
mikutano wa Tarafa ya Endabash, wilaya ya Karatu, mkoani Arusha.
Bw.
Kibakaya alieleza kuwa mfumo wa filamu unaotumiwa kutoa elimu ya fedha
umewavutia wananchi kwa kuwa umekuwa mfumo rahisi utakaowawezesha
kukumbuka kwa urahisi mafunzo waliyopata ya elimu ya fedha.
‘‘Kumekuwa
na mwitikio mkubwa wa wananchi kuhudhuria mafunzo ya elimu ya fedha
inayotolewa kwa njia ya filamu yenye mada mbalimbali ikiwemo uwekaji
akiba, bima, utunzaji wa fedha na mada ya masuala ya uwekezaji wa
masuala ya kifedha,’’ alieleza Bw. Kibaya.
Alisema kuwa Serikali
iliona kuwa ni muhimu kuwapatia wananchi elimu ya fedha ili kuwawezesha
kuwa na uelewa wa elimu ya fedha ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi
sahihi ikiwemo kutumia vema mikopo inayotolewa na Serikali kuwawezesha
wananchi kiuchumi.
Bw. Kibakaya alifafanua kuwa elimu hiyo ya
fedha italeta mabadiliko kwa wananchi hasa ikizingatiwa kuwa njia ya
uwasilishaji kwa filamu itabaki kuwa kumbukumbu ya muda mrefu hivyo
kuendelea kujenga mabadiliko ya usimamizi wa fedha binafsi.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Endabash, Bw. Boisa Mandoo,
aliishukuru Serikali kwa kuwawezesha kupata elimu ya fedha katika maeneo
yao ambayo itawasaidia katika kusimamia matumizi ya fedha pamoja na
kutumia huduma za fedha zinazotolewa na watoa huduma waliosajiliwa kwa
mujibu wa sheria.
‘’Naipongeza Serikali ya Rais Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kutuletea wataalamu kuja kutoa elimu ya fedha kwa
wananchi na sisi kama Serikali tutaendelea kuzihamasisha taasisi za
fedha ambazo hazijasajiliwa ziweze kusajiliwa ili wananchi waweze kupata
huduma katika taasisi rasmi’’, alisema Bw. Mandoo.
Program ya
kutoa elimu kwa Umma ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo Sekta ya
Fedha 2020/21 - 2029/30 ambapo unalenga kufikia wananchi asimia 80 hadi
kufikia mwaka 2025/26 pamoja na utekelezaji wa Programu ya Elimu ya
Fedha kwa Umma ya mwaka 2020/21 - 2025/26.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF- Karatu, Arusha)
No comments:
Post a Comment