Na Said Mwishehe,Michuzi TV
TAASISI
inayojihusisha na utunzaji wa Mazingira 'Environment Conservation
Community of Tanzania(ECCT) kupitia Mradi wake wa 'ECO WEAR' inatoa
mafunzo ya ushonaji wa nguo,mifuko mbadala na urembo unaotokana taka
nguo kwa wasichana yenye lengo kubwa la kuwawezesha kuwa na ujuzi wa
kushona sambamba na utunzaji wa mazingira.
Kupitia Mradi huo
zaidi ya mabinti 15 kutoka Tabata Kimanga Jijini Dar es Salaam
watapatiwa mafunzo hayo kwa Kipindi cha miezi sita na pindi ambapo
watamaliza mafunzo hayo wataendelea kusaidiwa katika kuendeleza shughuli
zao kwani tayari watakuwa na ujuzi unaowezesha kujiajiri au kuajiriwa.
Akizungumza
leo Desemba 11,2024 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Taasisi ya ECCT
Lucky Michael amesisitiza kuwa Mradi huo wa ECO WEAR unaohusisha mabinti
wa kike ukilenga kuwapa mafunzo ya ushonaji pamoja na kuwafundisha
kutunza mazingira kwa kupunguza uchafuzi wa taka nguo.
“Takwimu
zinaonesha kwamba taka zinazotokana na nguo ni namba mbili kuchafua
mazingira duniani ,ukiachana na viwanda vya plastiki.Kwa kutambua hilo
taasisi ya ECCT tumeona ni vema kuwezesha mabinti hawa ambao wanatokea
katika mazingira magumu lakini pia wanatoka katika namna mbalimbali
katika jamii ili waweze kupata mafunzo haya na hatimaye waweze
kujikwamua kiuchumi lakini watunze na mazingira…
“Kwani
tunawafundisha pia suala zima la uchambuzi wa taka kwani sio kila nguo
ambayo tunaipata ama mabaki ya vitambaa yanayoshonwa tunatumia yote au
nguo zote tunarudisha katika urejeshaji bali tunachambua ili kuona nguo
au vitambaa gani tunatumia.
“Pia tunatoa elimu kwa jamii kuhusu
utunzaji wa mazingira kwani tunaamini suala utunzaji mazingira ni
mtambuka lakini Jamii yetu bado inahitaji elimu zaidi ili wawe wakwetu
katika kutunza mazingira,”amesema na kutumia nafasi hiyo kutoa shukrani
kwa Serikali za Mitaa yote mitano iliyopo katika Kata ya Kimanga, ofisi
ya Kata na Ofisa maendeleo kata kwa kufanikisha kuwapata Wanufaika hao.
Vilevile
Michael amesema kupitia hao wasichana wanashirikiana na taasisi ya
Arizona Vocational Training Center ambayo imesajiliwa chini ya VETA,
hivyo wanatoa mafunzo ya ushonaji pamoja na kuangalia namna wanaweza
wakawa wanapata nyenzo za ushonaji.
Pia amesema wanashirikiana na
taasisi ya Leaders joint forum kuwezesha mabinti hao kufahamu haki zao
hasa katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa mtoto wa kike,haki
zake lakini wanawafundisha ujasiriamali , biashara na kurasimisha
biashara zao na kusisitiza baada ya mafunzo hayo watakwenda kuanzisha
biashara zao.
Hata hivyo amesema katika kuhakikisha wanasimamia
biashara zao Taasisi hiyo wanatoa mafunzo ya ujasiriamali kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali na hasa Women Fund Tanzania (WFT-
T)ambao kwa sehemu ya wanafanikisha mafunzo hayo.
Ametoa rai kwa
wananchi na wadau mbalimbali waweze kutusaidia kuchangia nguo,
kuchangia mabaki ya nguo na vitambaa.Pia wanaomba washonaji,wauza
mitumba,taasisi na watu mbalimbali kusaidia kuwapatia mabaki ya nguo na
nguo ambazo zimeshatumika ili ziwasaidie katika kufanikisha jitihada
zao.
“Kwahiyo tumekuwa sehemu ya kutunza mazingira lakini kama
wanawake tunakwenda kutengeneza nguo kwa kuziongezea thamani lakini sio
nguo tu tunatengeneza urembo unaovaliwa kwa mfano hereni ,kibanio cha
Nywele, tunatengeneza mifuko mifuko ya kubebea laptop.
“Kwahiyo
sisi kama wadau wa mazingira tunasaidia hawa mabinti waweze kupata ujuzi
wa kuzalisha mifuko ambayo inatumika katika mikutano yetu mbalimbali
na unaponunua bidhaa zetu tayari unakuwa umemkomboa kiuchumi lakini
umeyatunza mazingira
“ECCT huwa tunakauli mbiu yetu inasema
Pamoja tuyatunze mazingira tukimaanisha kila mmoja wetu anayo nafasi na
anapaswa kuyatunza mazingira,sio Serikali,sio taasisi au Kampuni fulani
bali ni jukumu letu wote.”
Kwa upande wake Nyanzobe Makwaiya
ambaye ni Mratibu wa Mradi wa ECO WEAR amesema kuwa mabinti walioko
katika Mradi huo ni wenye umri kuanzia miaka 18 mpaka miaka 35 na wote
wametoka Kata ya Kimanga kwasababu ndio Kata ambayo wameichagua kufanya
mradi huo.
Ameongeza kuwa kupitia Mradi huo walilenga mabinti
ambao wanapitia ukatili au wako nyumbani na hawajishughulishi na
shughuli yoyote kwa kipindi hiki ,hivyo wameamua ujuzi huo ambao
utawawezesha kujikwamua kiuchumi .
Amefafanua wameamua kujikita
katika taka Nguo kwasababu ni taka ambazo hazijapewa kipaumbele na
Taasisi nyingine lakini takwimu zinaonesha asilimia 0.8 ya nguo ambazo
zinapelekwa dampo la Pugu ni taka nguo na mwisho wa siku zinaishia
kuchomwa ambapo hiyo inakuja kuleta madhara katika mazingira.
Kwa
upande wa wanufaika wa Mradi huo Hamisa Hussein , Aneth Benezeth na
Salma Mwishehe wamesema wanaaamini baada ya mafunzo hayo watakuwa na
ujuzi wa kushona na hivyo kuwa na fursa ya kujiendeleza kiuchumi
sambamba na kutunza Mazingira.
Wamesema tayari wameshaanza
kufahamu kushona na wanaamini baada ya miezi sita watakuwa na uwezo
mkubwa katika ushonaji wa nguo na mifuko mbadala huku wakiishukuru
Taasisi hiyo kwa kuwapa nafasi hiyo kwani walikuwa mtaani na hawakuwa na
shughuli yoyote ya kuwaingizia kipato.
Mkurugenzi wa Taasisi ya ECCT Lucky Michael akizungumza kuhusu umuhimu wa Mradi wa ECO WEAR katika kuwakomboa mabinti kiuchumi pamoja na kutunza mazingira.
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment