jlogo

Karibuni Jamvini Wanajamii

topads

Post Top Ad

demo-image

RAIS wa Zanzibar - Suala la kuimarisha utawala bora ni jambo la msingi

Share This

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema suala la kuimarisha utawala bora ni jambo la msingi kuleta maendeleo ya nchi, hivyo amewasihi watumishi wa umma na binafsi kuongeza juhudi, uzalendo na uadilifu katika kulitumikia Taifa.

Dk. Mwinyi amesema, wajibu wa kuimarisha Utawala Bora hasa kwa matumizi ya rasilimali za umma si wa Serikali na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali pekee bali ni kwa kila mtumishi.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo, ukumbi wa Ziwani Polisi Zanzibar kwenye maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Ukaguzi ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Zanzibar.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza juhudi za kuijengea mazingira mazuri Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili itekeleze vizuri kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni, na taratibu zilizopo kitaifa na kimataifa na kwenda sambamba na mabadiliko ya mara kwa mara ya ukaguzi duniani.

Dk. Mwinyi amebainisha kuwa, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imefanikiwa kuisaidia Serikali kutekeleza kwa ufanisi malengo na mipango yake, na kuongeza kuwa Maendeleo makubwa yaliyofikiwa Serikalini yanatokana na mchango wa udhibiti na ukaguzi bora wenye kuzingatia uwajibikaji, nidhamu na uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma nchini.


Aidha, Rais Dk. Mwinyi amesema, miongoni mwa faida zinazopatikana kwenye Ofisi ya CAG ni pamoja na kusaidia kuongeza Pato la Serikali ambapo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kupitia ripoti yake ya kila mwaka, huishauri Serikali juu ya mbinu bora za kuziba mianya ya upotevu wa makusanyo ya mapato ya Serikali, kuibua vyanzo vipya vya mapato pamoja na kuwepo kwa usimamizi bora wa rasilimali za umma.


Ameeleza, ufanisi unaotokana na utekelezaji wa kazi za ukaguzi una mchango mkubwa kwa serikali hasa kuimarisha uchumi wa Zanzibar, ambapo hadi kufikia mwaka 2023 kasi ya ukuaji wa uchumi umefikia wastani wa 7.4% ikilinganishwa na 1.3% ya mwaka 2020.


Dk. Mwinyi ameongeza kuwa, mafanikio ya kazi za ukaguzi wa rasilimali za umma, yameimarisha utoaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, maji safi na salama, nishati ya umeme na huduma nyengine.


Pia Rais Dk. Mwinyi ameongeza kuwa, kazi za ukaguzi wa rasilimali fedha na rasilimali nyegine zimeimarisha utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, viwanja vya Michezo na masoko.


Amebainisha kuwa mafanikio hayo yamechangiwa sana na udhibiti na ukaguzi bora wa rasilimali za umma, ambapo Serikali hupokea na kuzifanyia kazi hoja, ushauri na mapendekezo yanayotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kupitia ripoti zake za kila mwaka.


Pia Dk. Mwinyi ameahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kuendelea kufanikisha malengo na mipango ya sasa na baadae ya Ofisi hiyo kwa kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu.


Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi amepongeza ushirikiano wa karibu uliopo baina ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ya Tanzania kwa kufanikisha kazi za ukaguzi wa hesabu za Serikali nchini.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi Ofisi ya Rais Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, amepongeza juhudi za rais Dk. Mwinyi za kuimarisha Umoja, amani na maendeleo na mshikamao kumeifanya Zanzibar kuwa nchi ya mfano kwa kasi ya Maendeleo yanayowashangaza wageni kutoka mataifa mbalimbali.
Amekiri kuwepo kwa mabadiliko makubwa kwenye Ofisi ya CAG kwa kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya nane ambayo yamekuwa kielelezo cha mafanikio ya miradi mbalimbali katika sekta tofauti.


Naye, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar (CAG), Dk. Othman Abbas Ali amebainisha kuwa maadhimisho hayo ni fursa adhimu kwa taasisi za Umma kuwatumia wataalamu wao kuongeza uwajibikaji kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za kukabiliana na uhujumu wa Uchumi, kuongeza uwazi na uwajibikaji pamoja na kutoa nafasi kwa watendaji wa Ofisi ya CAG kuwafikia walengwa na kuwafariji katika makundi mbalimbali wakiwemo wazee wasiojiweza, yatima, na wenye watu wenye mahitaji maalumu.


Ameongoza kuwa kujadiliwa kwa tipoti za CAG kila mwaka katika Baraza la Wawakilishi kumbeendelea kuleta tija ya usimamizi wa rasilimali na matuimizi ya fedha za umma kwa taasisi mbalimbali na kujenga uelewa kwa wananchi juu ya utendaji wa Ofisi hiyo.


Maadhimisho ya Wiki ya Ukaguzi ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Zanzibar kwa mwaka 2024, yenye kauli mbiu isemayo, *Kuimarika kwa Ukaguzi wa Rasilimali za Umma Kunaongeza Ufanisi na Kuleta Tija Nchini*. yalianza rasmi tangu Disemba, 12 kufikia kilele chake Disemba 18 mwaka huu kwa kushiriki mambo mbalimbali ya kijamii ikiwemo kutoa elimu ya ukaguzi kwa jamii.


Kuwatembelea na kuwafariji watoto waliolazwa katika hospitali ya Kitogani, Unguja na Vitongoji kwa Pemba, kuwatembelea na kuwafariji wazee wetu waliopo Sebleni, Unguja na Limbani Wete Pemba.


Kuwatembelea na kuwafariji Wanafunzi wenye mahitaji Maalum katika Skuli ya Pujini, Pemba na Jendele kwa Upande wa Unguja, kuwatembelea na kuwafariji Watoto yatima waliopo katika Kituo cha Mazizini pamoja na Kuwatembelea na kuwafariji watumishi na wastaafu wagonjwa wa Afisi hii ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.


IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

Comment Using!!

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad