Na -Nihifadhi Abdulla
Zanzibar: Takriban miaka miwili sasa tangu kumalizika zoezi la kuhesabu idadi ya watu na makaazi nchini Tanzania, zoezi hilo linaonesha dhahiri wingi wa wanawake huku kwa upande wa Zanzibar ambapo asilimia 52 ni wanawake na 48 kwa wanaume.
Takwimu hazina uwiano juu ya maana ya kujua idadi ya watu na kuishia hapo bali ni pamoja na kuzingatia misingi ya utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia ambayo inategemea uhuru na haki.
Katiba ya Zanzibar sehemu ya 21 inaeleza kwamba kila mtu apewe nafasi sawa katika kupata nafasi za uongozi kwenye serikali, aidha kwa njia ya moja kwa moja ama kupitia wawakilishi wao waliochaguliwa kwa njia ya huru na haki.
Mwenyekiti wanawake taifa wa chama cha Sauti ya Umma SAU,Safia Mussa amesema wanawake wengi wanaogopa kugombea kutokana na unyanyasaji wakijinsia uliokithiri na sio kama hawataki kuwa viongozi.“Mwanamke anapoamua kugombea ili apitishwe huombwa rushwa ya ngono, hapohapo kuna maneno ya kashfa ambao ni udhalilishaji sasa mambo kama hayo huwarejesha nyuma” Amesema Safia.
Akiwa kama mgombea makamo wa Rais 2020 kupitia SAU anaongeza kuwa hadi kufikia hapo amevuka vikwazo kutokana na kujiamini kwake na kujua sheria.“Sheria zinaruhusu mwanamke kugombea lakini lazima kwanza ujiamini,uthubutu na usikubali kutetereshwa hii itakupa nafasi kwa wanamke ameumbwa kuwa kiongozi”Amemalizia Safia.
Amina Awesu kutoka Chama cha ACT WAZALENDO amesema hivi sasa wanawake wameamka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi hususan majimboni lakini wanakwamishwa kutokana na mifumo iliyopo.”Tume ya uchaguzi ZEC,pale kuna sheria nzuri na za wazi,lakini ikifika wakati wa uchaguzi hazitekelezeki na hiyo inatokea kwa vile huyu wa chama x na mwengine chama y”. Amesema Amina.
Kwa Zanzibar baraza la wawakilishi 2015 wanawake walikuwa ni asilimia 36 ambao ni wawakilishi 28 tu kati ya 54 na kati ya majimbo 54 wanawake walichaguliwa katika majimbo sita tu na ubunge ni watatu dhidi ya 50.
Na kwa mwaka 2020 idadi ya madiwani ni 110 wanaume 85 sawa na asilimia 77% na asilimia 23 ni wanawake ambao 25 kwa upande wa wawakilishi wanawake wakuchaguliwa ni wanane kati ya 50 sawa na asilimia 16.
Kwa upande wa wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar kwenye majimbo 50 ni wanne sawa na asilimia 8 hii ikiwani idadi ya kuchaguliwa majimboni.
Hali hio inaonesha kuwa mjumbe wa Baraza kuu Taifa la akina Mama Chama Cha Mapinduzi UWT CCM,Salma Ibada amesema akiwa mgombea uwakilishi viti maalum Mkoa wa Mjini kichama 2020 alikumbana na vitisho kwa vile yeye hakuwa na pesa na si mzoefu.“Niliambiwa nawezaje kugombea kwa vile wenzangu niliogombea nao walikua madarakani mimi nikathunutu na nikatokea mtu wa tatu kutokana na hatua hiyo anaona nimefanikiwa” Amejinasibu Salma ambaye anaona suala la ukatili na udhalilishaji kwa wanawake wanapojitoa kugombea ni vyema kusimamiwa kwa mujibu wa sheria ili kupunguza hofu kwa wanawake.
Wanaharakati na wadau wa masuala ya wanawake na watoto wanaliona suala la rushwa ya ngono,ukosefu wa fedha na kashfa ya maneno kama vikwazo vinawapa woga wanawake waliopo kwenye siasa kuwa viongozi.
Hawra shamte kutoka Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar -JUWAUZA amesema changamoto nyingi zinakwamisha ushirki wa wanawake wenye ulemavu ni kutokana na baadhi ya wanajamii kutowaunga mkono.“Ukosefu wa uhamasishaji na mfumo ya kijamii unawapuuza wanawake husuan wenye ulemavu”. Hawra ameongeza kuwa hali hiyo inachangia nafasi ndogo ya ushiriki wao katika uongozi wa kisiasa Zanzibar.
Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania upande wa Zanzibar wamekuwa na program mbalimbali za kuwapatia elimu na kuendelea kuhamasisha wanawake wajitoke kugombea nafasi za uongozi kwenye vyama vya siasa.Dkt. Mzuri Issa amesema kwa mujibu wa takwimu zilizopo inaonesha dhahiri utekelezaji wa usawa wa kijinsi bado ni kitendawili kinachohitaji kuteguliwa.“Ikiwa Zanzibar imetia saini makubaliano mbalimbali kuna wajibu kupitia hili serikali, vyama vya siasa, Tume na kila chombo kinachohusika viweke kipaumbele kwa wanawake na kuondoa vikwazo ili kuhakikisha wanawake wanaingia kwenye ngazi za maamuzi na kufikia 50/50 tuliyokubaliana nayo”Amesema Dkt Mzuri ambaye analiona suala la 50/50 ni suala lililopo kwenye mpango wa utekelezaji wa mikataba mengi ya kimataifa.
Mkuu wa Mkurugenzi ya huduma za sheria Tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC- Maulid Mohamed amesema Tume imetoa fursa kwa mwanamke kushiriki kugombea uongozi kwa nafasi za kisiasa. “Kuna sheria na sera ya uchaguzi inavyomlinda mwanamke sheria ya uchaguzi ya Zanzibar no. 4 ya mwaka 2018 na Sera ya Jinsia na ushirikishwaji wa jamii ya Tume ya uchaguzi ya Zanzibar iliyoanzishwa mwaka 2015”Amesema Maulid.
No comments:
Post a Comment