JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LAKAMATA WATUHUMIA 176, WAKIWEMO WA MATUKIO YA MAUAJI

Share This

 


JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao katika maeneo yote ya Mkoa kwa kufanya misako na doria zenye tija na kupata mafanikio ikiwa ni pamoja na kukamata watuhumiwa 176 wakiwemo wa matukio ya mauaji, dawa za kulevya, uvunjaji na wizi, nyara za serikali na pombe haramu ya moshi.

Katika taarifa ya Jeshi hilo iliyotelewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya,  Benjamin Kuzaga – SACP leo Novemba 5, 2024 imeeleza kuwa linawashikilia watuhumiwa watatu, Kenedy Richard maarufu Majiulaya [26] mkazi wa Kijiji cha Galula Wilaya ya Songwe mkoani Songwe, Msafiri Peter Mwahonje maarufu Wakwetu [48] mkazi wa matundasi na Uhuru Ulaya Sukwa [63] mkazi wa Magamba Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara ya madini Peter Bruno Mteta [59] mkazi wa matundasi Wilayani Chunya ambayo yalitokea Oktoba 12, 2024 saa 2:00 usiku kwa kumpiga risasi mgongoni akiwa nyumbani kwake.

Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza upelelezi wa tukio hilo na Novemba 01, 2024 Kijiji cha Ubaruku Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya watuhumiwa watatu walikamatwa kuhusiana na tukio hilo wakiwa na silaha iliyotumika katika tukio hilo pamoja na risasi zake tano.

Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi linamshikilia Hamis Shizya Kasunga [50] mkazi wa maghorofani Jijini Mbeya kwa tuhuma za kumuua mke wake aitwaye Emmy Fred Mwasile [35] mkazi wa Forest Maghorofani Jijini Mbeya kwa kumpiga kwa kitu kizito sehemu mbalimbali za mwili wake katika tukio lililotokea Novemba 20, 2024 saa 6:30 mchana huko Mtaa wa Foresy mpya, Jijini Mbeya kutokana na wivu wa kimapenzi akimtuhumu mke wake kuwa na mahusiano na mwanaume mwingine.

taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alikimbia na katika ufuatiliaji alikamatwa Novemba 23, 2024 saa 9:00 alasiri katika mji mdogo wa Tunduma Mkoani Songwe akiwa katika harakati za kuvuka mpaka kwenda nchini Zambia.

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya vile vile, linawashikilia watuhumiwa 23 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya uvunjaji wa nyumba na kuiba katika maeneo tofauti ya Mkoa wa Mbeya.

Mbali ya kukamata watuhumiwa hao, zipo mali mbalimbali walizokutwa nazo ambazo ni Televisheni 16, redio 5, spika za redio 8, majiko ya gesi 3, mitungi 2 ya gesi, mita 2 za Mamlaka ya maji safi na maji taka, mifuko ya saruji 62 na Air Compressor 1, goroli 47 za Karasha na mashine moja ya kuchomelea.

Pia, katika muendelezo wa misako iliyofanywa na Jeshi la Polisi mkoani hapa watuhumiwa wengine 31 walikamatwa kwa nyakati tofauti kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya Bhangi yenye uzito wa kilo 18 na gramu 820, pombe haramu ya moshi maarufu gongo ujazo wa lita 104 na mtambo mmoja wa kutengenezea pombe hiyo.

Pia watuhumiwa 8 wanashikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya wizi kwa njia ya mtandao pamoja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu. Watuhumiwa walikutwa na nyaraka mbalimbali vikiwemo vitambulisho vya kupigia kura, laini za mitandao tofauti na mihuri.

Itakumbukwa Oktoba 01, 2024 Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe.Mhandisi Hamad Masauni na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura walitangaza kuanza kwa zoezi la usalimishaji silaha kwa hiari zinazomilikiwa kinyume cha sheria kuanzia Oktoba 01 hadi 31, 2024 nchini kote.

Baada ya muda uliotolewa kuisha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilianza msako katika maeneo mbalimbali na Novemba 01, 2024 huko Wilaya ya Chunya ndani ya Pori la akiba la Piti Mwise lilimkamata John Zakayo maarufu Mpigangoma [52] mkazi wa Kijiji cha Mazimbo akiwa na silaha aina ya Gobole kinyume cha sheria.

Mtuhumiwa alikuwa akiitumia silaha hiyo katika matukio ya uwindaji haramu na katika msako huo alikutwa na nyara za serikali zikiwemo nyama za wanyamapori zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni moja.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa yeyote aliyevunjiwa nyumba yake na kuibiwa kufika kituo cha Polisi Mbeya kwa ajili ya utambuzi wa mali zake. Aidha, linatoa rai kwa wananchi kufanya shughuli halali ili kujipatia kipato kwani uhalifu haulipi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad