Na Mwandishi Wetu. Michuzi tv
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka ambapo Mvua za wastani hadi Juu ya wastani vikitarajiwa katika Mikoa ya Njombe, Ruvuma Mtwara, maeneo ya Kusini na Magharibi mwa mkoa wa Lindi na Kusini mwa Mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro .
Pia amesema kipindi cha nusu ya kwanza ya msimu (Novemba 2024 hadi Januari, 2025) kinatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani ukilinganisha na nusu ya pili (Februari hadi Aprili 2025), ambacho kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi.
Dkt. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA ameyasema hayo leo Oktoba 31,2024 wakati akitoa utabiri wa muelekeo wa mvua za msimu Novemba hadi Aprili 2024/2025 na kusema athari zinazoweza kujitokeza ni vipindi vya unyevu nyevu wa kuzidi kiasi pamoja na maafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
“Mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi,Rukwa,Songwe, Singida,na Dodoma, Kaskazini na Mshariki mwa mkoa wa Lindi na Kaskazini mwa Mikoa ya Mbeya na Iringa huku Mvua za wastani hadi juu ya wastani zikitarajiwa katika mikoa ya Njombe,
Amesema, mvua za Wastani hadi chini ya Wastani zimeanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba 2024 katika mkoa wa Kigoma na zinatarajiwa kusambaa katika mikoa mingine katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba 2024 na zinatarajiwa kuisha wiki ya kwanza ya mwezi Mei 2025.
Katika Mikoa ya Singida na Dodoma zinatarajiwa kunyesha mvua wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2024 na kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili 2025 huku mvua za wastani hadi juu ya wastani zikitarajiwa kuanza wiki wa ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2024 na kuisha wiki ya kwanza ua mwezi Mei 2025 katika Mkoa wa Njombe, Kusini mwa mikoa ya Mbeya, Iringa, na Morogoro.
Dkt. Chang’a amesema joto la bahari la chini ya wastani linatarajiwa kuendelea hali inayoashiria uwepo wa lanina hafifu huku pia joto la bahari la wastani linatarajiwa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya msimu ( Novemba,2024 hadi Januari 2025) hali inayotarajiwa kupunguza kasi ya msukumo wa unyevunyevu kutoka bahari ya Hindi kuelekea nchini.
"Joto la wastani hadi juu kidogo ya Wastani linatarajiwa katika eneo la mashariki mwa bahari ya Atlantiki ( Pwani ya Angola).
Pia, Dkt. Chang’a ametoa ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali kama vile kilimo, afya,chakula, uvuvi mifugo na nyinginezo.
Katika sekta ya kilimo wakulima wameshauriwa kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa kuzingatia hali ya unyevu katika udongo na kutumia mbinu bora za kuzuia maji kutuama shambani.
"Ongezeko katika vina vya maji, mabwawa na mito vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani hivyo kuongeza hatari ya mafuriko hususani katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko.
Katika maeneo yanayotarajiwa mvua za wastani hadi chini ya wastani wananchi wanashauriwa kutibu maji kabla ya kuyatumia kwani wanaweza kulazimika kutumia maji yasiyo safi, hivyo sekta ya Afya inashauriwa kuchua hatua stahiki ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
"Menejimenti za maafa zinashauriwa kuchukua hatua stahiki ikiwemo kutoa elimu na miongozo itakayohamasisha kuzuia au kupunguza madhara na kuhamsisha uhifadhi wa chakula kwani vipindi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi yanayoweza kusababishisha uharibifu wa miundombinu mazingira na kupoteza mali.
No comments:
Post a Comment