JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


HALMASHAURI KIBAHA MJI YAFIKIA ASILIMIA 64 YA UANDIKISHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA

Share This

 





Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha Oktoba 17, 2024
HALMASHAURI ya Mji wa Kibaha, mkoani Pwani, imepiga hatua kubwa katika zoezi la uandikishaji wa daftari la wapiga kura, ikiwa imefikia asilimia 64 ya malengo yake.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, Zoezi hili linaendelea kwa lengo la kufikia asilimia 100 ifikapo Oktoba 20, 2024.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha Oktoba 17, Simon aliwapongeza watendaji wa wilaya hiyo kwa ushirikiano mzuri uliosaidia sio tu kuimarisha zoezi la uandikishaji, bali pia kuongeza makusanyo ya mapato kwa asilimia 125.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, alieleza kuwa halmashauri hiyo imeongeza mapato yake ya ndani kutoka asilimia 23 hadi asilimia 33 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Alisema lengo lilikuwa kukusanya shilingi bilioni 8, ikiwa ni ongezeko kutoka bilioni 7 zilizokusanywa mwaka wa fedha 2023/2024.

Kuhusu miradi ya maendeleo, Dkt. Shemwelekwa alibainisha kuwa ujenzi wa Sekondari za Msangani, Tangini, na Viziwaziwa, pamoja na Shule ya Msingi ya Tangini, uko katika hatua za mwisho.

Vilevile, Kituo cha Afya cha Pangani kiko tayari na kinatarajiwa kuzinduliwa kuanza kutoa huduma rasmi ifikapo Oktoba 18, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mussa Ndomba, aliongeza kuwa baadhi ya kata kama Pichandege na Misugusugu tayari zimevuka malengo ya uandikishaji, kwa kufikia asilimia 105.3 na 100.9 mtawalia.

Hata hivyo, kata ya Viziwaziwa inaonekana kuwa nyuma katika zoezi hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad