Benki
ya Biashara ya DCB imezindua mikopo ya boda boda na bajaji yenye
masharti nafuu, ikiwa na lengo la kuwaondolea adha na usumbufu vijana
wanaojishughulisha na biashara ya usafiri wa boda boda wanayoipata
kutoka baadhi ya watu wanaotoa mikopo yenye masharti magumu maarufu kama
‘mikopo umiza ama kausha damu’.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Mbagala, Temeke, jijini Dar es Salaam leo,
Mkurugenzi wa Biashara wa DCB, Bw. Ramadhan Mganga akimwakilisha
Mkurugenzi Mtendaji wake Bw. Sabasaba Moshingi alisema, mikopo hiyo
huwafanya vijana wakiiishi kwa hofu na mashaka na kijikuta muda wote
wakiendesha pikipiki bila tahadhari hivyo kuhatarisha usalama wao na
abiria zao.
“Mtu
anakupa pikipiki anakupa marejesho ya zaidi ya miezi 14, unatoa elfu 12
kwa siku, unajikuta umelipa zaidi ya shs milioni 4.5 kwa pikipiki moja,
sasa sisi DCB tukasema haiwezekani vijana hawa wa kitanzania waishi kwa
hofu na maumivu.
“Lakini
pia tunazindua mikopo hii ya pikipiki na bajaji, Ili pia kuunga mkono
juhudi za serikali yetu inayoongozwa na Rais, Mheshimiwa Dk. Samia
Suluhu Hassan katika azma yake ya kuendelea kupunguza tatizo la ajira
miongoni mwa vijana. Tutaendelea kusapoti juhudi zote za serikali na
tupo tayari wakati wowote kuitikia wito tutakapotakiwa kufanya hivyo”,
alisema Bwana Maganga.
Akizungumza
zaidi kuhusu mikopo hiyo, Mkurugenzi huyo alisema mikopo ya pikipiki na
bajaji imepata uitikio mkubwa kutoka kwa vijana kwani kwa kipindi
kifupi zaidi ya shs bilioni 1.5 zimekopeshwa huku wakitarajia kutoa
kiasi cha zaidi ya shs bilioni 5 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Temeke, Bw. Abdallah Mtinika, aliipongeza Benki ya
DCB Kwa kuja na huduma hiyo akisema kuwa mikopo hiyo imelenga kundi
sahihi lenye uhitaji.
“Benki
ya DCB ni Benki yetu, ilianzishwa na halmashauri za Dar es Salaam,
wanahisa waanzilishi wakiwa Halmashauri za Temeke Kinondoni na Ilala,
nina furaha kubwa kuona benki hii ikisonga mbele.
“Nawaasa
vijana wenzangu nendeni mkachape kazi, rudisheni mikopo yenu kwa wakati
ili muweze kutunza heshima yangu na naambiwa kuna vijana zaidi ya 300
wameshanufaika na mikopo hii, nitafurahi endapo nitaitwa tena kushuhudia
kundi la vijana wengine wakipokea mikopo ya boda boda.
“Kwa
namna ya kipekee niwaase pia kama mfahamuvyo hiki ni kipindi kuelekea
uchaguzi wa serikali za mitaa, kujiandikisha kwenu ni ishara kuwa
mnataka kuweka viongozi wazuri, mjitokeze kushiriki katika harakati zote
za uchaguzi ili muweze kutuletea viongozi bora kwa mustakabali mzuri wa
Taifa letu”, alisema Meya huyo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Bw. Abdallah Mtinika ( katikati) akikata utepe kuzindua rasmi mikopo ya bajaji na bodaboda inayotolewa na Benki ya Biashara ya DCB, ikiwahusisha Wanachama wa Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki Dar es Salaam ( CMPD ), katika hafla iliyofanyika Mbagala, Temeke, Dar es Salaam leo. Kulia ni Mkurugenzi wa Biashara wa benki hiyo, Bw. Ramadhan Mganga.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Bw. Abdallah Mtinika ( wa pili kulia) akikabidhi funguo ya pikipiki aina ya TVS 125 kwa Dereva wa Bodaboda, Pascal Fungo ( wa pili kushoto) baada ya kupata mkopo kutoka Benki ya Biashara ya DCB mara baada ya uzinduzi rasmi wa mikopo ya boda boda na bajaji ya benki hiyo, katika hafla iliyofanyika Mbagala, Temeke, Dar es Salaam leo. Kulia ni Mkurugenzi wa Biashara wa benki hiyo, Bw. Ramadhan Mganga.
Mkurugenzi wa Tehama na Uendeshaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Bw. Leonard katamba ( wa pili kushoto) na Mwenyekiti wa Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki Dar es Salaam ( CMPD ), Bw. Michael Massawe wakipiga picha baada ya kusaini mkataba wa ushirikiano, muda mfupi baada ya uzinduzi rasmi wa mikopo ya bajaji na bodaboda inayotolewa na benki hiyo, Mbagala, Temeke, Dar es Salaam, leo. Kutoka kushoto ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Bw. Abdallah Mtinika na Meneja wa Mikopo ya Wajasiriamali Wadogowadogo, Bi. Sheila Nicas Banzi.
Mwanachama wa Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki Dar es Salaam ( CMPD ), Bw. Pascal Fungo, akimpakia Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Bw. Abdallah Mtinika kwenye bodaboda aliyoipapata kwa mkopo kutoka Benki ya DCB, muda mfupi mara baada ya uzinduzi rasmi wa mikopo ya bajaji na bodaboda ya benki hiyo, katika hafla iliyofanyika Mbagala, Temeke, Dar es Salaam leo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Bw. Abdallah Mtinika akisindikizwa na wanachama wa Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki Dar es Salaam ( CMPD ) baada ya kuzindua rasmi mikopo ya bajaji na bodaboda ya Benki ya Biashara ya DCB, Mbagala, Temeke, Dar es Salaam, leo.
No comments:
Post a Comment