JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Airtel na TIC waingia Ubia kukuza sekta ya uwekezaji

Share This

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri na Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh wakibadilishana mikataba mara baada ya kusaini makubaliano ya miaka miwili ili kuvutia wawekezaji nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh akizungumza leo Oktoba 04, 2024 alipofika ofisi za TIC kwaajili ya kusaini makubaliano ambayo yatarahisisha TIC kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri akizungumza jijini Dar es Salaam leo Oktoba 04, 2024 wakati wa kusaini makubaliano kati ya TIC na Airtel ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa Wawekezaji nchini. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh.


Picha za pamoja.

KAMPUNI ya Airtel Tanzania imeingia ushirikiano wa miaka miwili na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kusaidia katika mchakato wa kuvutia wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.

Ushirikiano huu kati ya TIC na Airtel Tanzania unaonyesha dhamira ya taasisi hizi katika kuwezesha ukuaji wa kiuchumi wa Tanzania kwa kuweka mazingira bora `ya uwekezaji.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Oktoba 04,2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC, Gilead Teri amesema kuwa ushiriki wa Airtel Tanzania utaonyesha jinsi Kituo cha Uwekezaji Tanzania kitakavyotumia huduma za mawasiliano na TEHAMA kwa ufanisi kushughulikia maswala mbalimbali yanayolenga kuboresha uwekezaji nchini.

"Airtel Tanzania inamilikiwa na serikali kwa asilimia 49, hivyo ushirika huu unadhihirisha dhamira ya Airtel katika kuhudumia taasisi za serikali na kuchagiza ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia uwekezaji. Katika kipindi cha miaka miwili ijayo, kupitia ubia huu kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC na Airtel Tanzania utasaidia kuboresha matokeo chanya kwa taifa letu." Amesema Teri

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh, amesisitiza kwamba ushirikiano huo utasaidia ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kuwezesha maendeleo ya nchi katika uchumi wa kidijitali, kukuza mwingiliano mzuri na kuvutia wawekezaji wapya.

“Ushirikiano huu unakuja wakati muafaka baada ya Airtel kuwa tumeanzisha Mkongo wa chini ya bahari wa Airtel 2Africa kwa lengo la kuleta mapinduzi katika sekta ya teknolojia. Mkongo huu wa chini ya bahari wa Airtel 2 Africa utaifanya Tanzania kuwa kitovu cha kidijitali, na hivyo kuimarisha ushirikiano kati ya TIC na wawekezaji wapya duniani. Ameeleza Balsingh

Balsingh amesema kuwa kutokana na mawasiliano imara ya Airtel, TIC itakuwa katika nafasi nzuri ya kuvutia wawekezaji kwenye soko la Tanzania na kuongeza idadi ya miradi ya maendeleo iliyoandikishwa na kituo hicho cha uwekezaji.

Pia ameongeza kuwa ushirikiano wa TIC na Airtel unawawezesha wawekezaji wazawa kufanya malipo kwa urahisi ili kulipia gharama mbalimbali zinazohusiana na TIC kama vile usajili kupitia huduma ya Airtel Money.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad