JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


SHILINGI BILIONI 145.7 KUBORESHA HUDUMA YA MAJI MANISPAA YA SONGEA

Share This

 

Waziri wa maji Jumaa Aweso akishuka ngazi baada ya kukagua ujenzi wa tenki la kuhifahi lita milioni 2 za maji linalojengwa kupitia mradi wa maji wa miji 28 katika manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.


Na Mwandishi wetu, Songea
WIZARA ya maji,imepanga kutumia kiasi cha Sh.bilioni 145.77 ili kujenga mradi wa maji wa miji 28 ambao utaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.


Hayo yamesemwa jana na Waziri wa maji Jumaa Aweso, baada ya kukagua ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi takribani lita milioni mbili linalojengwa katika mtaa wa Mahenge kata ya Mjini Manispaa ya Songea.

Waziri Aweso,amewapongeza watumishi wa wizara ya maji wakiwemo wa mkoa wa Ruvuma kwa kazi nzuri ya kutatua kero pamoja kuboresha huduma ya maji safi na salama katika maeneo mbalimbali.

Alisema,siku za nyuma mkoa wa Ruvuma ulikuwa kama kichaka kwa watendaji kula fedha zinazoletwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji,na kutolea mfano mradi wa maji Litola-Kumbara ambao ulisimama zaidi ya miaka 12 bila kukamilika wakati Serikali ilishatoa fedha ili kukamilisha ujenzi wake.

“Tangu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani ameleta mapinduzi makubwa kuhusu huduma ya maji kwani sasa miradi mingi ya imetekelezwa na wananchi wanapata maji kwenye maeneo yao,haya ni mafanikio makubwa kwetu sisi kama Serikali”alisema Aweso.

Aidha alisema,katika mkoa wa Ruvuma kuna miradi zaidi ya 30 inayoendelea kutekelezwa na itakapokamilika itafikisha malengo ya Serikali ya kufikisha asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini ifikapo mwaka 2030.


Alitaja baadhi ya miradi hiyo ni mradi wa maji wa Mtyangimbole uliopo katika Halmashauri ya wilaya Madaba,mradi wa maji Misechela wilaya ya Tunduru na mradi wa maji Liuli uliopo wilaya ya Nyasa.

Waziri Aweso,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa magari ya kuchimba visima kwenye mikoa yote yenye changamoto kubwa ya upatikaji maji wa maji,vifaa vya utafiti vya maji na kuchimba mabwawa kwenye maeneo yasiyokuwa na vyanzo vya uhakika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Songea(Souwasa)Mhandisi Patrick Kibasa alisema,mradi ulianza kutekelezwa mwezi Januari 2024 na mpaka kufikia mwezi Julai utekelezaji wake umefikia asilimia 3.9.

Kibasa alisema,Serikali imemlipa mkandarasi fedha za awali Sh.bilioni 21,865,952,341.45 sawa na asilimia 15 kati ya Sh.bilioni 154,773,015,609.69 ambazo ziko kwenye mkataba wa ujenzi.

Kibasa alitaja kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa miundombinu ya kudaka maji katika mto Njuga uliopo kijiji cha Kikunja katika Halmashauri ya wilaya Songea ili kuzalisha maji lita milioni 16.5 kwa siku.

Alitaja kazi nyingine zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa matenki matatu ya kuhifadhi maji yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 9,kujenga miundombinu ya mabomba ya kusafirisha maji kilometa 30.2 na kujenga miundombinuya bomba za usambazaji maji km 34.1.

Aliongeza kuwa,mradi huo ukikamilika utaongeza upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Manispaa ya Songea kwa zaidi ya asilimia 95,hivyo kutosheleza mahaitaji ya maji safi na salama kwa wakazi wa Manispaa hiyo.

Alieleza kuwa,katika utekelezaji wa mardi huo changamoto kubwa ni mabadiliko ya chanzo cha maji kutoka bwawa ambalo awali lilionyesha kuwa na kiwango kikubwa cha cha maji yanayohitajika kwenda kwenye mto,lakini sasa yamepungua na kuchelewesha utekelezaji wa mradi.

Alisema baada ya mabadiliko hayo kwenye chanzo cha maji,mkandarasi amewasilisha upya gharama za ujenzi wa ambazo zinazidi gharama awali ambazo ni Sh.bilioni 145,773,015,609.69.

Kibasa alieleza kuwa, chanzo cha maji kimegharimu Sh.bilioni 58.6 wakati ujenzi wa bwawa umegharimu Sh.bilioni 62.5 na ujenzi wa mtambo wa kuchuja na kutibu maji gharama ni Sh.bilioni 48.8 wakati gharama za awali kama ilivyo kwenye mkataba ilikuwa Sh.bilioni 22.6.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas alisema,mradi wa maji wa miji 28 utakapokamilika utakuwa na mafanikio makubwa kwa kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Manispaa ya Songea.


Rc Abbas,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,kwa kutoa zaidi ya Sh.bilioni 3 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika manispaa ya Songea na Sh.bilioni 20.1 kwa ajili ya miradi ya maji inayotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa).

Naye Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Dkt Daamas Ndumbaro alisema,huduma ya maji inaendelea vizuri,lakini changamoto kubwa ni kukua kwa mji wa Songea na ongezeko kubwa la watu wanaohitaji huduma ya maji kwa matumizi mbalimbali.

Dkt Ndumbaro alisema,kwa sasa mahitaji ya maji katika manispaa ya Songea ni lita milioni 21,278,000 wakati uzalishaji wa maji kwa sasa ni lita milioni 12,030,000.

Alieleza kuwa,mradi huo ukikamilika utaongeza upatikanaji wa maji hadi kufikia lita milioni 27 ambazo zitatosheleza kwa mahitaji ya wakazi wa mji huo.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad