NA MWANDISHI WETU, KIBAHA
MAFUNZO ya
Uongozi na Usimamizi Jumuishi kwa Wanawake yaliyofanyika katika Shule ya
Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani, yamefungwa Ijumaa
Septemba 27, huku washiriki wakitakiwa kuweka alama chanya kwenye maisha
ya wanaowaongoza, pamoja na kuwapa nafasi ya kuonesha uwezo wao.
Mafunzo
hayo yaliyoshirikisha wanawake viongozi kutoka Taasisi za Umma, Taasisi
Binafsi, Wizara na Idara za Serikali, Jeshi la Ulinzi wa Wanznchi
Tanzania (WTZ) na Halmshauri, yalifungwa Afisa Mkuu wa Rasirimali Watu
wa Benki ya NMB, Emmanuel Akoonay akimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu, Bi.
Ruth Zaipuna.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Akoonay alisema
anaamini mafunzo hayo yanaenda kuwa chachu ya kutengeneza viongozi bora
zaidi miongoni mwa wanawake, na hivyo hayakuwa tu ya kuwajengea nyinyi
uwezo, bali kuongeza amasa ya wanawake kuchangamkia nafasi za uongozi
katika taasisi mbalimbali.
“Kupitia elimu mliyopata katika
mafunzo haya ya wiki nzima, mmejengewa uwezo wa kukabiliana na
changamoto zinazokwaza mchango wa wanawake katika ukuaji kiuchumi na
uendelezaji wa taifa, tunajua mmepikwa na mmeiva tayari kwa majukumu
kwenye taasisi zenu,” alisema
Akoonay akafafanua kuwa: “Dhana ya
uongozi ni kuongoza wengine kufika mahali ambapo hawakuamini kama
inawezekana, kwani mara nyingi inaaminika kuwa kiongozi unapaswa kuwa na
dira na maono makubwa kuliko unaowaongoza
“Na kwa sababu hiyo,
ili uwe kiongozi mzuri lazima ujifunze kuweka alama chanya kwenye maisha
ya wengi, hususani unaowaongoza, mjifunze kuwapa watu nafasi ya
kuonesha uwezo wao, pamoja na kuongezea uwezo walionao. Nawasihi nyinyi
wote mkawe aina hiyo ya viongozi huko muendako,” alisema.
Alitoa
wito kwa wanawake hao kuwa wasiache kujifunza, na kwamba mafunzo
waliyopewa yameambatana na mifano na maelezo kutoka kwa viongozi
mbalimbali, wakiwemo wanawake waliopigania uhuru, ambao wameacha vitabu
na machapisho ambayo yana nyongeza ya kujifunza kwao.
“Mfano hai,
mimi niko chini ya kiongozi mwanamke (Bi. Zaipuna), lakini kiutendaji
shatumtazami wala kumuona kama ni mwanamke, bali ni kiongozi imara,
shupavu na madhubuti, ambaye tukikaa kwenye mikutano inayojumuisha
wanaume wengi, sauti yake ndio inayotuunganisha na kutupa dira ya
pamoja,” alimaliza.
Kwa upande wake, Naomi Zegezege Mtemba
aliyekuwa Mwenyekiti wa Wahitimu wa Mafunzo hayo, akitokea Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambako ni Mkurugenzi
Msaidizi Idara ya Ulaya na Amerika, aliishukuru Serikali kwa elimu kubwa
waliyowapa.
“Kwa niaba ya wahitimu, tunawashukuru walimu na
wakufunzia wa shule hii, lakini pia tunaishukuru Serikali ya Rais Dk.
Samia Suluhu Hassan, kwa mpango madhubuti wa kutoa mafunzo mbalimbali ya
kuwaongezea uwezo wanawake ili washiriki ngazi mbalimbali za uongozi.
“Mafunzo
haya yametuwezesha kupata maarifa makubwa, ujuzi na uzoefu muhimu
katika uongozi na usimamizi wa rasirimali watu, usimamizi wa majukumu
yaliyo mbele yetu, usimamizi wa utekelezaji wa maelekezo mbalimbali ili
kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa na jamii.”
Naye
Kaimu Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kabula Igambwa,
alisema kuwa mafunzo hayo yalilenga maeneo mbalimbali, ikiwemo Uzalendo,
Maslahi ya Taifa, Usalama, Historia na Harakati za Ukombozi, Kuongeza
uwezo wa Kufikiri Kimkakati na Misingi ya Uongozi.
“Pia ni mafunzo yaliyoawapa nafasi ya Kuongeza Ujuzi wa Kuongza Taasisi Kimkakati, Utatuzi wa Migogoro, Masuala ya Itifaki, Kufanya Maamuzi Bora na Kujiandaa Kuchukua Nafasi za Juu Kiuongozi,” alibainisha Igambwa katika hafla hiyo.
No comments:
Post a Comment