JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Jaji (Mst.) Mwangesi: hauwezi kuwa mwangalizi wa maadili ya watu wengine kama wewe huna maadili

Share This

  



RAI imetolewa kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na weledi wa hali ya juu wanapotekeleza majukumu yao.

Rai hiyo imetolewa na Kamshina wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi wakati akiakifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi cha Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Cate mjini Morogoro Septemba 23, 2024.

‘’Hauwezi kuwa mwangalizi wa maadili ya wengine wakati wewe mwenyewe hauna maadili, hivyo kama mfanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma unatakiwa kuwa mfano wa kuigwa na watumishi wengine wa Umma katika nyanja ya uadilifu,’’alisema Mhe. Mwangesi.

Jaji (Mst.) Mwangesi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo la Wafanyakazi wa ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ameongeza kuwa uadilifu unajengwa kwa nguzo kuu tatu.

Alizitaja nguzo hizo kuwa ni utaalamu, uaminifu na uwajibikaji na kuongeza kuwa ni wajibu kwa kila mtumishi wa Sekretarieti kuzingatia nguzo hizo.

‘’Ninawaasa kuzingatia nidhamu na kujituma katika kutekeleza majukumu yenu na yeyote atakayeenda kinyume na hayo, atakua si miongoni mwetu na hatutasita kumchukulia hatua kutokana na mwenendo wake,’’alisema.

Katika hatua nyingine, Kamishna huyo wa Maadili, amezungumzia umuhimu wa watumishi kutunza na kulinda rasilimali za Taasisi na kuacha uzembe katika matumizi ya mali na vitendea kazi vya ofisi kutokana na upatikanaji wake kuwa wa gharama.

‘’Niwaombe kuacha uzembe na kuwa makini katika matumizi ya vitendea kazi na kuvitunza kwa hali na mali kwani vitendea kazi tulivyonavyo ni vichache na upatikanaji wake ni washida sana,’’amesisitiza.

Kuhusu kuufanyaji kazi kwa ushirikaiano, Mwenyekiti huyo wa Baraza la Wafanya kazi, aliwapongeza watumishi wa Sekretarieti ya Maadili kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuomba hali hiyo iwe endelevu na amesisitiza kuwa kwake milango ipo wazi kwa yeyote mwenye jambo kumuona na kujadili kwa pamoja.

‘’Niwapongeza kwa ushirikiano wenu katika utendaji kazi na ninawaomba ushirikiano huo mnaonionyesha mimi pia uwe endelevu miongoni mwenu ili tuweze kuifikisha mbali Taasisi yetu,’’ alisisitiza.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad