Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
JUMLA ya wananchi 367 wanaoishi katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuendelea leo tarehe 22 Agosti, 2024 wakiwa na mifugo 995 wamehama kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro na kuelekea katika kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni na maeneo mengine waliyochagua wenyewe.
Hamasa hiyo ya wananchi kuhama kwa hiyari imeongezeka kutokana na uhamaishaji unaofanywa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na watendaji wa wilaya ya Ngorongoro chini ya usimamizi wa ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha Naiyobi tarafa ya Ngorongoro bwana bwana Meleji Sikoony Laiza amesema wameamua kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro baada ya kugundua kuwa kuna fursa kubwa katika kijiji cha Msomera na maeneo mengine nje ya hifadhi.
“Wengi wetu hapa nikiwemo mimi mwenyewe kabla ya kuamua kufanya maamuzi haya nilikwenda katika kijiji cha Msomera na kujionea hali ya mambo ilivyo na kwa kweli tumeridhika kuhama kwa hiyari na kutoka ndani ya hifadhi ambapo hakuna fursa yoyote”,alisema bwana Meleji.
Wananchi hao wameishukuru serikali ya awamu ya sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya kuendesha zoezi hilo ambalo lina lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kulinda uhifadhi.
Akiwaaga wananchi hao Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii (anayesimamia maliasili) CP Benedict Wakulyamba amesema kuwa kuondoka kwa kundi hilo leo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kulinusuru eneo la hifadhi ya Ngorongoro ambapo wananchi wameendelea kuelimishwa na kuhama kwa hiari kwa ajili ya kuboresha maisha yao na kunufaika na fursa za kiuchumi zilizoko nje ya hifadhi.
Ametoa tahadhari kuwa wapo baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakihamia Msomera kinyemela bila kufuata utaratibu uliowekwa na kuleta changamoto kwa ndugu zao wanaowakuta huko na kuwasihi kuwa kufuata utaratibu na miongozo iliyowekwa ili wawe wakazi halali wa maeneo wanayopenda kuhamia.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kuhamisha wananchi wa Ngorongoro kwa hiari, Afisa Uhifadhi mkuu na Meneja mradi wa kuhamisha wananchi kwa hiari PCO Flora Assey amebainisha kuwa tangu zoezi hilo lilipoanza mwezi Juni, 2022 hadi kufikia mwezi Agosti, 2024 takriban kaya 1,598 zenye watu 9,618 na mifugo 39,779 imeshahama ndani ya hifadhi kwenda Kijiji cha Msomera na maeneo mengine.
Serikali inatekeleza zoezi la kuwahamisha wananchi wanaoishi tarafa ya Ngorongoro kwa hiari ili kuboresha maisha ya wananchi hao na kulinda shughuli za hifadhi hasa kutokana na ongezeko la watu ma mifugo.
Akiongea kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Kamishna msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Mhandisi Daniel Chegere ameeleza kuwa NCAA inaendelea na zoezi la kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuhama kwa hiari katika eneo la hifadhi na kwenda maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa kujengewa miundombinu ya kisasa
mmyenye huduma zote muhimu za kijamii ambazo ni salama zaidi tofauti na ilivyo ndani ya ya hifadhi.
Mhandisi Chegere ameongeza kuwa hali ya usalama katika hifadhi hiyo inaendelea vizuri, ambapo ulinzi umeimarishwa na wageni mbalimbali wanaotembelea hifadhi hiyo wanaendelea na shughuli za utalii bila changamoto.
No comments:
Post a Comment