JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


KESI YA MIKOPO CHECHEFU YAUNGURUMA MAHAKAMANI

Share This

 

*Ni baina ya KAHAMA OIL MILLERS na Benki ya Equity wanaodaiwa kukopa zaidi ya bilioni 80 na kukataa kulipa

*Ushahidi waendelea kutolewa

Na Chalila Kibuda,Michuzi TV
MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Biashara imeendelea na usikilizwaji wa kesi ya mgogoro wa malipo ya mikopo wa Dola za Marekani 32 milioni baina ya Benki za Equity Tanzania Limited (EBT) na Equity Kenya Limited (EBK) na kampuni ya Kahama Oil Mills Limited na wenzake.

Kwa sasa kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Profesa Agatho Ubena imeingia katika hatua ya pili ambapo mahakama hiyo sasa inapokea ushahidi wa wadaiwa katika kesi hiyo ambao ni EBT na EBK wanaowakilishwa na wakili Zaharani Sinare, baada ya wadai kumaliza kutoa ushahidi wake.

Kesi hiyo ni mwendelezo wa kesi mbalimbali zilizofunguliwa dhidi ya benki hizo na kampuni mbalimbali zinazodaiwa kukopeshwa na benki hizo mabilioni ya pesa kisha , zikakataa kulipa badala yake zikazifungulia kesi benki hizo zikipinga kudaiwa kwa madai kwamba hazikukopeshwa na benki hizo.

Wadai (waliofungua kesi hiyo) katika kesi hiyo namba 78 ya mwaka 2023 ni kampuni za Kahama Oil Mills Limited na Kamahama Import & Export Commercial Agency Limited, zinazodaiwa kukopeshwa pesa hizo na benki hizo.

Wengine ni wadhamini wa mkopo unaobishwaniwa; Kom Group of Companies Limited, Shinyanga Royal Pharmacy (2015) Limited, Royal Supermarket (2008) Limited na Mhoja Nkwabi Kabalo, mkurugenzi wa kampuni hizo.

Kampuni hizo zinazowakilishwa na wakili Frank Mwalongo zilifungua kesi hiyo baada ya kuandikiwa barua na benki hizo zikiwataka kulipa Dola za Marekani 46,658,395.81 (zaidi ya Dola za Marekani 46.6 milioni sawa na zaidi ya Sh122.54 bilioni).

Kiasi hicho kinajumuisha deni la msingi la mkopo wa Dola 32 milioni (zaidi ya Sh84 bilioni) ambao benki hizo zinadai kuwa zilizikopesha kampuni hizo, pamoja na riba.

Benki hizo zimeanza kutoa ushahidi wake unaolenga kupangua hoja na madai ya wadai kuwa hazikuwakopesha pesa hizo, na kuthibitisha madai yake kinzani kuwa zilizikopesha kampuni hizo kiasi hicho cha fedha na zimekataa kurejesha.

Jana Julai 22, 2024, wakili wa wadai, Mwalongo alianza kumhoji shahidi wa kwanza wa upande wa utetezi (benki hizo), Michael Kessy, ofisa wa Equity Bank Kenya kutoka idara ya mikopo.

Wakili Mwalongo ameanza kumhoji shahidi huyo kuhusiana na ushahidi wake aliokwishauwasilisha mahakamani hapo kwa njia ya maandishi pamoja na nyaraka mbalimbali alizoziwasilisha kama vielelezo vya ushahidi wake.

Hata hivyo, shahidi huyo ameieleza mahakama hiyo kuwa hakushiriki katika mchakato wa utolewaji wala usimamizi wa mikopo hiyo kutoka EBK kwenda Kom Group of Companies, kwa kuwa wakati huo alikuwa bado hajaajiriwa na benki hizo.

Huku akirejeshwa na wakili Mwalongo katika nyaraka mbalimbali zilizopokewa na mahakama kama vielelezo vya ushahidi katika kesi hiyo, ameieleza mahakama kuwa jumla ya Dola 30.7 milioni zimeingia kwenye akaunti ya mdaiwa wa kwanza (Kahama Oil Mills) kutoka kwa Kom Group of Companies Limited- Escrow account.

Wakili Mwalongo katika maswali yake hayo yalilenga kuvunja madai ya benki hizo kuwa zilizikopesha kampuni hizo jumla ya Dola 32 milioni kwa awamu kutoka katika akaunti ya mdaiwa wa pili Equity Bank Kenya Limited (EBK)

Hata hivyo alipoulizwa kuwa ni nini ambacho kinaonesha kuwa pesa hizo ambazo benki hizo zinadai kuwa ziliizikopesha kampuni hizo zilitolewa na EBK (kwenda kwa wadai wa kwanza na wa pili, Kahaka Oil Mills na Kahakama Import & Export alijibu kuwa kuna nyaraka zingine zinaonesha hivyo.

Baada ya mahojiano hayo, kesi hiyo imeahirishwa mpaka Alhamisi Julai 25, 2024, ambapo shahidi huyo ataendelea kuhojiwa maswali ya dodoso, kabla ya mashahidi wengine wa utetezi kuitwa.

Katika kesi hiyo kampuni hizo zinakiri kuingia mikataba na benki hizo wa mkopo wa jumla ya Dola za Marekani 32 milioni iliyosainiwa na pande zote Mei 28, 2018 na Juni 19, 2020, zinapinga kupokea mkopo huo kutoka kwa benki hizo.

Hata hivyo zinadai kuwa benki hizo zilitoa kiasi hicho cha pesa Dola za Marekani 32 milioni kwa kampuni ya Kom Group of Companies ya Nairobi Kenya na kwamba zenyewe zilipokea mkopo wa jumla ya Dola 30 milioni kutoka kwa Kom Group of Companies ya Nairobi Kenya na si kwa benki hizo.

Pia zinadai kwamba zimeshalipa sehemu ya mkopo huo kwa kampuni hiyo, huku wakitaja nyaraka za uthibitisho wa malipo hayo ambazo watazitumia kama vielelezo vya ushahidi wao.

Hivyo zinaiomba Mahakama itamke kuwa mkataba wa makubaliano ya mkopo wa Kibenki baina yao na benki hizo uliosainiwa Mei 28, 2018 na Juni 19, 2020 haukutekelezwa na kwamba benki hizo zilikiuka mkataba wa makubaliano ya mkopo huo kwa kushindwa kuwapatia mkopo huo.

Pia wanaiomba Mahakama itamke kuwa benki hizo hazina madai yoyote dhidi yao na kwamba dhamana za mkopo walizozikabidhi Kwa benki hizo zinashikiliwa isivyo halali na iamuru benki hizo ziziachilie dhamana hizo pamoja na kuwarejeshea hati mmiliki za amana hizo.

Hata hivyo benki hizo nazo zimefungua madai kinzani dhidi ya wadai, zikipinga madai ya kukiuka masharti ya mkataba wa mkopo wa kibenki kwa kushindwa kuutekeleza na kwamba zilitoa mkopo huo kwa kampuni ya Kom Group of Companies Limited ya Nairobi Kenya na si kwako,.

Benki hizo zinawataka kuthibitisha madai hayo na uwepo wa kampuni inayojulikana kama Kom Group of Companies Limited ya Nairobi Kenya ambayo wanadai kuwa ndivyo EBK iliipatia mkopo wa Dola za Marekani 32 milioni.

Badala yake benki hizo zinadai kuwa zilitimiza wajibu wake wa kimkataba kama kama walivyokubaliana lakini wadai hao (wakopaji) waliokiuka masharti ya mkataba wa mkopo na kwamba hivyo zinadai kuwa zinastahili kushikilia amana zote zilizowekwa kama dhamana ya mkopo huo.

Zinadai kuwa zilitoa mkopo huo wa Dola za Marekani 32 milioni kwa mdaiwa wa kwanza na wa pili na kwamba zina ushahidi wa nyaraka kuthibitisha hayo madai.

Kwa mujibu wa madai yake mpaka kufikia Julai 26, 2023 deni la msingi lilikuwa limeshafikia Dola za Marekani 47, 228,592.53 (sawa na zaidi ya Sh124 bilioni), ambalo riba inazidi kuongezeka kwa kiwango kilichokubaliwa kimkataba mpaka malipo yote yatakapokamilika.

Hivyo zinaomba Mahakama hiyo iitupilie mbali shauri la madai ya wadai na itoe amri kwamba mdai wa kwanza na wa pili (wakopaji) wamekiuka vigezo na masharti ya mkataba wa mkopo uliosainiwa na pande zote Mei 28, 2028.

Vilevile zinaomba amri ya Mahakama kwa wakopaji na wadhamini kulipa jumla ya Dola za Marekani 47, 228,592.53 (zaidi ya Dola za Marekani 47.2 milioni sawa na zaidi ya Sh124 bilioni)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad