-Azindua mfumo wa VAR kwa mechi za ligi kuu.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania walioajiriwa katika sekta binafsi kufanya kazi kwa weledi na uadilifu ili kuwawezesha wawekezaji kupata mafanikio na kupanua wigo wa ajira.
Ametoa wito huo leo (Jumatatu. Julai 15, 2024), wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa vifaa vya uzalishaji na urushaji matangazo vya Kampuni ya Azam Media Limited iliyofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
"Suala la ajira kwenye sekta binafsi tumeliweka mstari wa mbele, nyie ambao tayari mmeingia na mnafanya kazi zenu, nawasihi mtambue kwamba ninyi ni mabalozi kwa wengine ambao bado hawajaingia huko, tekelezeni majukumu yenu kwa weledi na uadilifu."
Akizungumza baada ya kukagua na kuzindua mitambo na vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi bilioni tano, Mheshimiwa Majaliwa amesema manunuzi ya vifaa hivyo ni mapinduzi makubwa katika tasnia ya habari kwani yanaifanya Tanzania kuwa nchi ya kipekee kwa kuwa na vifaa vya kisasa vya aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki.
"Uwekezaji uliofanywa na Azam media Limited ni mkubwa sana, tumeona mabadiliko ya kiteknolojia yaliyowezesha kupanua wigo katika nyanja mbalimbali na kufungua fursa kwa Watanzania wenye vipaji mbalimbali."
Vifaa hivyo ambavyo ni magari ya kisasa ya kurushia matangazo (OB Vans), kamera za kisasa pamoja na mfumo wa kusaidia maamuzi viwanjani (VAR) vitatumika kurushia matangazo mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara na Zanzibar, masumbwi, mpira wa kikapu na mashindano ya magari.
“Mfumo wa kusaidia maamuzi uwanjani (VAR) utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi kwa waamuzi pamoja na kuongeza thamani ya ligi kuu nchini.”
Mheshimiwa Majaliwa pia ameshuhudia uzinduzi wa chaneli mpya ya Azam 4 HD ambayo itatumika kurusha Ligi Kuu ya Ufaransa (League 1) na Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga)
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Hamisi Mwijuma amesema Wizara hiyo itaendelea kuunga mkono wawekezaji katika kukuza sekta za michezo, sanaa na utamaduni ili kuongeza ajira miongoni mwa Watanzania.
Awali, Mkurugenzi wa Azam Media Limited, Bw. Patrick Kahemele amesema kampuni hiyo itaendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika tasnia ya habari. “Vifaa vilivyonunuliwa na kampuni hii ni vya kisasa na vina uwezo mkubwa na vinatumia teknolojia ya kisasa kurusha matangazo.
No comments:
Post a Comment