JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


CMSA YAZINDUA MPANGO UWEKEZAJI WA KAMPUNI SANLAM UNAOJUMUISHA MIFUKO MIWILI

Share This

 Na Mwandishi Wetu


MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA) imezindua mpango wa Uwekezaji wa Pamoja wa Kampuni ya Sanlam Investment East Africa Limited unajomuisha mifuko miwili ya Sanlam Pesa Money Market Fund na Sanlam USD Fixed Income Fund.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo CPA Nicodemus Mkama amesema hatua hiyo ni muhimu katika maendeleo ya sekta ya fedha hususan masoko ya mitaji hapa nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.

"Tumejumuika katika hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Uwekezaji wa Pamoja wa kampuni ya Sanlam Investments East Africa Limited, unaojumuisha mifuko miwili iitwayo Sanlam Pesa Money Market Fund na Sanlam USD Fixed Income Fund; na uzinduzi wa ofisi za Sanlam Investments East Africa Limited katika jiji la Dar es Salaam – Tanzania.

"Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli katika masoko ya mitaji zinafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta uwazi na haki kwa washiriki wote."

Amefafanua Masoko ya mitaji ni sehemu ya mfumo wa sekta ya fedha inayowezesha upatikanaji wa fedha za muda mrefu, yaani zaidi ya mwaka mmoja, kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo. 

Amesema fedha za kugharamia shughuli za maendeleo hupatikana kwa kuuza hisa za kampuni (shares), hatifungani za kampuni (corporate bonds), hatifungani za taasisi (Subnational Bonds), hatifungani za Serikali (Government bonds) na vipande katika Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (Collective Investment Schemes). 

Ameongeza kuwa fedha hupatikana kutoka kwa wawekezaji, ambao ni watu binafsi, taasisi na kampuni na hatimaye fedha hizo huwekezwa katika sekta za uzalishaji na hivyo kuchochea ustawi na maendeleo ya uchumi.

CPA Mkama amesema Aprili 16,2024, CMSA iliidhinisha Waraka wa Matarajio na Mkataba wa kuendesha Mifuko ya uwekezaji wa pamoja ya kampuni ya Sanlam Investments East Africa Limited yaani Sanlam Pesa Money Market Fund na Sanlam USD Fixed Income Fund Trust Deed.

" Idhini ilitolewa na CMSA baada ya Sanlam Investments East Africa Limited kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya uanzishaji na uendeshaji wa Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.

"Naujulisha umma kuwa, Sanlam Pesa Money Market Fund na Sanlam USD Fixed Income Fund ni mifuko ambayo imekidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.

"Sanlam Pesa Money Market Fund na Sanlam USD Fixed Income Fund ni mifuko inayoendeshwa na kampuni ya Sanlam Investments East Africa Limited ambayo ni kampuni yenye jukumu la kuendesha na kusimamia mifuko hii (Fund Manager) na Benki ya CRDB ina jukumu la Mtunza Dhamana wa Mifuko (Custodian Bank)." amesema CPA.Mkama.

Amesema lengo kuu la Mifuko hiyo ya Uwekezaji wa Pamoja ni kuhamasisha wawekezaji wadogo, wa kati, na wakubwa kuunganisha nguvu zao na kuwekeza kwa pamoja ili kunufaika na fursa zinazopatikana katika sekta ya fedha, hususan masoko ya mitaji.

Aidha, malengo mahsusi ya Mifuko hiyo ni kuwawezesha watanzania wa kada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vijana, wanawake, makundi maalum, taasisi na mifuko ya hifadhi ya jamii kunufaika na uwekezaji unaosimamiwa na wataalamu waliopewa leseni ya kutoa huduma ya katika masoko ya mitaji; kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza.

Pia na kuwawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za uchumi na kuongeza kipato na kuongeza uanzishwa kwa Mifuko hii ya Uwekezaji ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi wengi zaidi mijini na vijijini na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

"Utekelezaji wa azma hiyo umeainishwa katika Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha yaani the Third National Financial Inclusion Framework (NFIF III) 2023-2028 wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta rasmi ya fedha ikiwa ni pamoja na masoko ya mitaji.

" Katika juhudi za kuwezesha kufikia malengo ya kuanzishwa kwa Mifuko hii, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), imeidhinisha kushusha kiwango cha chini cha ushiriki katika uwekezaji kwenye Mifuko hii kutoka Shilingi milioni moja.

"Hatua hii ni muhimu kwani inalenga kuwezesha ushiriki wa wawekezaji wa kada mbalimbali katika Mifuko hii, ikiwa ni pamoja na wananchi wenye vipato vya chini na vya kati.Kwamujibu wa Sera na Miongozo ya uwekezaji wa Mifuko hii ya Uwekezaji, fedha zitakazopatikana kutoka kwa wawekezaji zitawekezwa katika masoko ya fedha na masoko ya mitaji...

"Ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika Kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa (Listed Equities), Hatifungani za Serikali (Treasury Bonds), Hatifungani za Kampuni (Corporate Bonds) na Dhamana za Serikali za muda mfupi.Lengo la uwekezaji wa aina hii ni kuifanya mifuko kuwa na ukwasi unaotosha ili kukidhi mahitaji ya fedha za wawekezaji pindi mahitaji yanapotokea,"amesisitiza.

Pia amesema uwekezaji katika Mifuko hiyo una manufaa mbalimbali katika ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi hapa nchini. Kwanza, unachangia katika utekelezaji wa Sera ya Serikali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kuwezesha makundi mbalimbali ya jamii, ikiwa ni pamoja na watu wa kipato cha chini kuwekeza kwa pamoja katika dhamana za Serikali (Treasury Bonds)

Hata hivyo ameipongeza Bodi na Menejimenti ya Sanlam Investments East Africa Limited kwa kufanya uamuzi wa kufungua ofisi yao mpya jijini Dar es Salaam, Tanzania kwa ajili ya kutoa huduma ya usimamizi wa uwekezaji, hususan usimamizi wa mifuko yao hii ya uwekezaji, ambayo leo hii tunaizindua rasmi

Pamoja na hayo ametoa Rai kwa wadau wote wa masoko ya mitaji kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwezesha wananchi kiuchumi na kutekeleza Mpango Kazi wa Serikali wa njia mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo.

Amesema lengo la kuwezesha Serikali na Sekta Binafsi kupata rasilimali fedha za kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo, na hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na ukuaji wa uchumi hapa nchini.

Pia amesema CMSA itaendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuchagiza na kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad