JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


WAANDISHI WA HABARI TUMIENI WELEDI KURIPOTI TAARIFA ZA UBORESHAJI DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA - INEC

Share This
Na Leandra Gabriel, Dar es Salaam

TUME Huru ya Uchaguzi (INEC,) imewataka waandishi wa habari nchini kuripoti taarifa za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa weledi, usahihi na kwa wakati ili wananchi waweze kujiandikisha pamoja na kuboresha Daftari hilo.

 Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulioikutanisha Tume hiyo na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji (Rufaa,) Jacobs Mwambegele amesema; Tume hiyo imekuwa ikishirikiana kwa ukaribu na vyombo vya habari hususani katika wakati wa kabla na kipindi cha uchaguzi.

 “Lengo la kukutana hapa ni kupeana taarifa kuhusiana na maandalizi ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pamoja na masuala mengine ikiwemo uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura, uboreshaji wa majaribio, ushirikishwaji wa wadau mbalimbali kama tufanyavyo hapa pamoja na ununuzi wa vifaa… Tunatambua umuhimu na nafasi ya vyombo vya habari na nafasi yake kubwa ya kufikia jamii tunaomba ujumbe na hamasa hii iwafikie wananchi kwa wakati na usahihi kupitia kalamu zenu.” Ameeleza.

 Amesema, Tume hiyo imeanza mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na rasmi uboreshaji huo utazinduliwa rasmi Julai, Mosi mwaka huu mkoani Kigoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kueleza kuwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2024/2025 umeboreshwa zaidi kwa kutumia teknolojia ya BVR (Biometric Voter’s Registration) ya kisasa zaidi kwa kuwekwa program endishi na hiyo ni pamoja na kupunguzwa uzito kwa vifaa na kubebeka kiurahisi hali itakayorahisisha kazi kwa watendaji katika maeneo mbalimbali hususani maeneo ya vijijiji.

 Aidha amesema wamefanikiwa kukutana  na makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, wawakilishi wa makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu ili kuhakikisha elimu na taarifa zinawafikia wananchi kwa wakati na usahihi.
 
Akitoa Mada kuhusiana na Maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura  Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhani Kailima amesema, idadi ya vituo 40,126 vya kujiandikisha wapiga kura vitatumika katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2024/2025 huku vituo 39,709 vikiwa Tanzania Bara na vituo 417 vikiwa Zanzibar na kufafanua kuwa kuna ongezeko la vituo 2312 ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika 2019/2020.

 “Tunataraji daftari litakuwa na wapiga kura 34,746,638 na idadi inaweza kuongezeka zaidi huku idadi ya wapiga kura 594, 494 itaondolewa kwa kupoteza sifa ya kuwa wapiga kura kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo, uraia na magonjwa ya akili yaliyothibitishwa na Daktari.” Ameongeza.  

Kailima amesema, kwa mujibu wa kanuni 15 (2) (c) za uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura; Tume imeweka utaratibu wa kuandikisha wanafunzi waliopo vyuoni, magereza, mahabusu na wafungwa ambao wamehukumiwa kifungo cha chini ya miezi sita kujiandikisha kuwa wapiga kura.

Kuhusiana na vifaa vitakavyotumika katika zoezi hilo amesema;  BVR 6000 pamoja na vishikwambi vitakavyotumika kuchukulia taarifa za wapiga kura, picha na saini vimenunuliwa huku BVR hizo zikiwa na mfumo endeshi wa Android zikiwa na kilogram 18 ukilinganisha na BVR za awali zilizokuwa na mfumo wa Windows na Kilogram 35.
 
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wameeleza kuwa mikutano ya namna hiyo ni muhimu kwa kuwa inatoa fursa ya kujadili kwa kina mambo yanayohusu Taifa na kuahidi kuibeba ajenda hiyo na kuifikisha kwa watanzania kwa msisitizo wa kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili wapate fursa ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka kupitia kalamu na sauti zao katika vyombo mbalimbali vya habari walivyoviwakilisha.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jocobs Mwambegele akizungumza katika warsha ya waandishi wa habari kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura iliyofanyika leo Juni 13, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhan Kailima akizungumza katika warsha ya waandishi wa habari kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura iliyofanyika leo Juni 13, 2024 Jijini Dar es Salaam.


Baadhi ya waandishi wa habari kutoka Vyombo mbalimbali wakiwa katika warsha iliyoandaliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inayohusu  Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura iliyofanyika leo Juni 13, 2024 Jijini Dar es Salaam.


Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jocobs Mwambegele, Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhan Kailima pamoja na viongozi wengine wa INEC wakiwa kwenye picha ya pamoja na waandishi wa habari wakati wa warsha ya waandishi wa habari kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura iliyofanyika leo Juni 13, 2024 Jijini Dar es Salaam.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad