JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


VYOMBO VYA HABARI VYATAKIWA KUELIMISHA, KUHAMASISHA UMMA KUSHIRIKI ZOEZI LA UBORESHAJI WA DAFTARI LA WAPIGA KURA

Share This
Na Leandra Gabriel, Dar es Salaam

IMEELEZWA Kuwa vyombo vya habari ni nguzo muhimu ya mafanikio katika mchakato wa mzima wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na katika Uchaguzi ikiwa vitazingatia kanuni, taratibu na maadili katika kuhabarisha na kuhamasisha Umma kujitokeza kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Akitoa mada juu ya Wajibu na Majukumu ya Vyombo vya Habari na Utangazaji katika Kuelimisha Umma katika mkutano maalumu wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulioikutanisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC,) na waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam Meneja wa Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA,) Eng. Andrew Kisaka amesema;

“ Tunatambua nafasi na mchango wa vyombo vya habari katika kuelimisha Umma, Tumieni kalamu na sauti zenu kuelimisha, kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi hili la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili wapate haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka.” Amesema.

Kisaka amesema, Katika kuelimisha wananchi lazima wazingatie weledi na maadili ya taaluma yao ili kuhakikisha wananchi wanashiriki mchakato huo wa uboreshaji wa daftari ambao utazinduliwa rasmi Julai, Mosi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Pia amewataka waandishi hao kutoa taarifa kwa usahihi na kwa wakati kwa kuwa ni haki ya raia kupata taarifa mbalimbali ambazo zitawasaidi kushiriki shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa maoni, kushiriki michakato mbalimbali ikiwemo ya uboreshaji wa daftari hilo.

Akieleza namna ukuaji wa matumizi ya mitandao ya kijamii ulivyokua Eng. Kisaka amesema utangazaji kupitia mitandao ya kijamii nchini umekua na kufikia asilimia 33 huku mtandao wa WhatsApp ukiongoza kwa kuwa na watumiaji milioni 9.9, Facebook watumiaji milioni 8.1, Instagram watumiaji milioni 3.7, YouTube watumiaji milioni 2.9, Tik Tok watumiaji milioni 1.6 na Mtandao wa X ( awali Twitter) ukiwa na watumiaji wapatao laki saba.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Huduma ya Kisheria kutoka (INEC,) Seleman Mtibora
amewataka washiriki wa mkutano huo kufikisha ujumbe na kuhamasisha jamii kuhusu zoezi hilo la Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura utakaohusisha pia uandikishaji wa wapiga kura wapya.

“Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika kupitia vituo 40,126 vya kujiandikisha wapiga kura kwa mwaka 2024/2025 huku vituo 39,709 vikiwa Tanzania Bara na vituo 417 vikiwa visiwani Zanzibar.” Amesema.

Mkutano huo wa siku mbili ulioikutanisha INEC na waandishi wa habari 250 kutoka mkoani humo ni maandalizi kuelekea Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad