JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Serikali yazitaka Taasisi kuimarisha usimamizi katazo la mifuko ya plastiki

Share This

 


SERIKALI Serikali imezitaka Mamlaka na Taasisi zake zote kuimarisha na kuwezesha vitengo vyake vinavyosimamia utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki ili viweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 na kanuni zake.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Asha Abdullah Juma aliyeuliza Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki.

Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Khamis amesema kuwa Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mifuko ya plastiki ambayo ilipigwa marufuku inadhibitiwa.

Ametaja mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za matumizi ya mifuko ya plastiki zikiwemo za kiafya na kimazingira endapo itazagaa.

Halikadhalika, Naibu Waziri Khamis amesema Serikali ilipiga marufuku uzalishaji, matumizi uingizaji, usambazaji na usafirishaji nje ya nchi mifuko ya plastiki nchini kuanzia tarehe 01 Juni, 2019.

Pamoja na mikakati hiyo, pia Serikali ilitunga Kanuni za Kupiga Marufuku Mifuko ya Plastiki za Mwaka 2019 kupitia Tangazo la Serikali Na.394 la 2019 ili kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki isiyofaa.

Hivyo, Naibu Waziri Khamis ametoa wito kwa Asasi za Kiraia pamoja na wananchi kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika kupambana na matumizi ya mifuko ya plastiki

Akijibu swali la nyongeza kuhusu mpango wa Serikali wa kuwabana wanaozalisha vifungashio na mifuko isiyokidhi vigezo, Mhe. Khamis amesema sheria ipo na inafanya kazi kwa kusimamiwa kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

“Nichukue fursa hii kuwapongeza wenzetu wa NEMC wanafanya kazi kubwa ya utekelezaji wa sheria hii na kama kuna haja ya kuifanyia marekebisho sheria hii tutafanya hivyo,“ amesema.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia Baraza hilo imekuwa ikifanya doria katika viwanda kubaini wanaokiuka sheria sanjari na kutoa elimu kwa wamiliki hao ili kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kufuata sheria.


Pia, akijibu swali la Mbunge wa Pandani Mhe. Maryam Omar Said kuhusu Serikali kuhakikisha vifungashio na mifuko iliyoruhusiwa inapatikana kwa wingi, Naibu Waziri Khamis amesema kuwa Serikali inaendelea kuwahamasisha wawekezaji waendelea kuizalisha kwa wingi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad