Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema itaendelea kuwatazama kwa karibu wananchi wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani, walioathiriwa na mafuriko ikiwamo kupoteza malazi, vyakula na kusimamia kwa uzalishaji wa Mali.
Aidha, imesema kuwa imeandaa mpango wa muda mfupi na muda mrefu kuhakikisha kaya zote ambazo zimeathirika zinapata msaada na wale ambao hawana pakukaa yapo maeneo ambayo yametengwa na serikali kuwahifadhi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji mkoani Pwani alipokuwa kipokea misaada mbalimbali ikiwemo ya vyakula iliyotolewa na Oryx Gas kwa kushirikiana na ASAS.
"Tayari tumeshatoa mchango wa takribani milioni 50 kusaidia kununua vitu kama mbegu baada ya mafuriko, Wizara ya Kilimo haiko nyuma, Husein Bashe (Waziri wa Kilimo) ameniahidi atafika Rufiji kuona cha kufanya ikiwemo kutafuta mbegu kwa ajili ya wananchi wa Rufiji. Tunawashukuru Oryx Gas na ASAS kwa msaada ambao wameutoa kwa ajili ya wananchi wa Rufiji," amesema.
Awali, Meneja Mauzo wa Oryx Gas Shaban Fundi amesema kwa niaba ya Oryx Energies wametoa pole kwa waathirika wote wa mafuriko yaliyotokea nchini hususan watu wa Rufiji.
"Kampuni ya Oryx Gas ikishirikiana na wadau wenzetu ASAS tumeamua tuwashike mkono wenzetu wa Rufiji kwa kuwapa msaada wa vyakula na mitungi ya gas ili kusaidia watu waliopo katika makambi ya kutolea misaada ya kibinaadam.
"Tumetoa mchele, unga wa sembe, mafuta ya kupikia yenye thamani ya zaidi ya milioni 52. Zaidi tumetoa mitungi mikunwa 100 na majiko 100, pia tumetoa mitungi midogo 100 yenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 25.Tunampa pole muheshimiwa Waziri Mchengerwa, Wananchi wa Rufiji na Serikali kwa ujumla,"amesema Fundi.
Msaada uliokabidhiwa ni pamoja na mchele, unga wa sembe, mafuta ya kupikia vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 52 pamoja na mitungi mikubwa ya gesi 100 na majiko 100 pamoja na mitungi midogo 100 yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 25.
No comments:
Post a Comment