JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


MWANZA YAZINDUA KAMPENI ELIMU KWA UMMA MRADI WA UJENZI WA MINARA 758 MAWASILIANO

Share This

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala,kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, akizungumza na viongozi wa serikali wakiwemo wa vyama vya siasa wakiongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM),leo katika uzinduzi wa kampeni ya Elimu kwa Umma kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Minara 758 ya Mawasiliano nchini.

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SERIKALI mkoani Mwanza kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), imezindua kampeni ya elimu kwa umma kuhusu utekelezaji wa miradi ya mawasiliano inayolenga kufikisha huduma hiyo kwa wananchi waishio maeneo yaliyo mbali vijijini yasiyo na mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma.

Pia,imewataka wadau wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa minara ya mawasiliano vijijini washirikiane na UCSAF kuhakikisha minara hiyo inakamilika kwa wakati wananchi wafikiwe na huduma hiyo.

Akizindua kampeni hiyo,leo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Hassan Masala kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda,amesema lengo ni kuelimisha wananchi wengi wa Kanda ya Ziwa,hatua zilizofikiwa na serikali katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara ya mawasiliano vijijini na maeneo machache ya mijini.

Pia, kampeni hiyo inalenga kuweka msukumo wa kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi waishio vijijini,hivyo wadau na UCSAF wakishirikiana kukamilisha mradi wa ujenzi wa minara 758,huduma za mawasiliano ya simu (Sauti na intenet/data),zitapatikana za uhakika maeneo yote.

Masala amesema huduma za mawasiliano ya simu zinagusa maisha ya watu,ni nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa mtu mmoja moja na taifa kwa ujumla,hivyo viongozi walioshikiri uzinduzi huo wawe mabalozi wazuri wa kuisemea serikali vizuri kwa wananchi utokana na elimu waliyoipata.

“Tunazindua kampeni hii kuhakikisha jamii ya Watanzania maeneo mbalimbali wanapata taarifa muhimu za utekelezaji wa ujenzi wa minara ya mawasiliano,licha ya kuzinduliwa Mwanza,itaendelea mikoa yote ya Kanda ya Ziwa (Shinyanga,Mara,Simiyu,Geita na Kagera),iliyofaidika na mradi huu na mengine ya mawasiliano, ”amesema.

Masala amesema serikali kupitia UCSAF iliingia makataba na makampuni (watoa huduma ya mawasiliano ya simu) kufikisha mawasiliano katika kata 713 kwa kujenga minara 758, inayopaswa kukamilika 2024/25.

“UCSAF imewaita viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali mnaowakilisha Watanzania mpate elimu hii nanyi mkaisambaze,mkaisemee vizuri serikali kuhusu utekelezaji wa mradi huu, wananchi wafahamu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anavyotekeleza masuala ya mawasiliano bila ubaguzi kwa Mtanzania yeyote,”amesema .

MKuu huyo wa Wilaya ya Ilemela amesema Ibara ya 61 ya Ilani ya CCM inaelekeza katika kipindi cha miaka mitano,sekta ya mawasiliano itajikita kuimarisha ubora wa mawasiliano nchini na kuhakikisha wigo unaongezeka na kuwafikia wananchi wote,katika kutekeleza hilo, Rais Dk.Samia alishudia utiaji saini mikataba ya ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano.

Pia,alishuhudia utiaji saini wa kuboresha na kuongeza nguvu minara 304 kutoka teknolojia ya 2G ya sauti pekee kwenda teknolojia ya intaneti/data ya 3G,4G na zaidi,hivyo kujengwa kwa minara hiyo vijijini ni utekelezaji wa ilani hiyo ya uchaguzi 2020-2025.
Naye Mratibu wa UCSAF Kanda ya Ziwa,Benard Buremo amesema baada ya makubaliano ya ujenzi wa minara hiyo kati ya wadau hao na serikali,watoa huduma walipewa miezi 24 ya kuikamilisha,kabla ya uchaguzi mkuu 2025 na kufafanua idadi ya minara hiyo 758 kwa kila kampuni ambapo Airtel inajenga 169,TTCL 104,Vodacom 190,Tigo 261 na Halotel 34.
Awali Ofisa Uhusiano wa UCSAF,Celina Mwakabwale amesema katika kuongeza ushindani katika soko la mawasiliano lilijitokeza ombwe lililosababishwa na nguvu za ushindani kujikita kupeleka mawasiliano maeneo yenye mvuto wa kibiashara na kuyaacha maeneo ya vijijini na ya mijini yasio na mvuto huo.

Amesema makampuni ya simu ni wabia wa serikali katika kutekeleza mradi huo unaogharimu sh.bilioni 126,ushirikiano huo umekuwa imara katika kufikisha huduma za mawasiliano hadi vijijini.


“Changamoto ya wananchi hawaufahamu Mfuko wa UCSAF,ulioanzishwa na Serikali kwa Sheria ya Bunge Namba 11 ya mwaka 2006 sura ya 422,kuwezesha na kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi waishio maeneo machache mijini na mengine ya mbali vijijini yasio na mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma wakihofia hasara,”ameeleza Mwakabwale.
Kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano huyo serikali kupitia UCSAF imeingia mikataba na watoa huduma ya mawasiliano kufikisha huduma hiyo katika kata 1,974 zenye vijiji 5,111 kwa kujenga minara 2,158,ikikamilika wananchi 23,978,848 watapata huduma ya mawasiliano ya simu kwa uhakika.sssss
Ofisa Uhusiano wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF),Celina Mwakabwale,leo akizungumza na wadau (hawapo pichani) waliodhuria uzinduzi wa kampeni ya Elimu kwa Umma kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Minara 758 ya Mawasiliano nchini.
Wakuu wa Wilaya za Misungwi na Sengerema,Johari Samizi (kushoto) na Senyi Ngaga (katikati), wakiwa katika uzinduzi wa kampeni hiyo ya elimu kwa umma leo.Walioketi nyuma ni makatibu tawala wa wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mwanza.
Maofisa Tarafa na Watendaji Kata mbalimbali mkoani Mwanza,wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa,leo wakifuatilia uzinduzi wa kampeni ya Elimu kwa Umma kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Minara 758 ya Mawasiliano nchini.
Picha zote na Baltazar Mashaka

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad