NA MWANDISHI WETU
MAELFU
ya wananchi wa wilaya ya Temeke, hususani wakazi wa Mbagala na
vitongoji vyake, wamefurika vilivyo katika Tamasha la Kuhamasisha
Ufunguaji wa Akaunti Nafuu Isiyo na Makato ya Mwezi inayotolewa na Benki
ya NMB ‘NMB Pesa Day.’
Tamasha hilo limefanyika mwishoni mwa
wiki kwenye Viwanja vya Mbagala Zakhiem, likienda sambamba na uzinduzi
wa Kampeni ya Weka Akiba na Ushinde itakayodumu kwa miezi mitatu, ambako
mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda.
Katika
tamasha hilo lililotanguliwa na mbio za taratibu ‘jogging’ na burudani
za muziki kutoka kwa wasanii kama Miso Misondo na Wazee wa Makoti, Mr
Blue, Dulla Makabila na wengineo, DC Mapunda aliipongeza NMB kwa ubunifu
katika kusambaza Huduma Jumuishi za Kifedha kwa wananchi.
DC
Mapunda alisema kwamba NMB Pesa inaenda kuwa chachu ya maisha bora kwa
wana Temeke na Watanzania kwa ujumla, ambako licha ya ‘jogging,’
wahudhuriaji walipewa elimu na huduma za kifedha, mashindano ya vipaji
vya muziki, ambako zawadi mbalimbali zilitolewa na DC huyo kwa washindi.
“Tupo
hapa kwa ajili ya NMB, ambayo inafanya kitu kikubwa sana leo kwa ustawi
wa maisha yetu. Kwa kutuletea NMB Pesa, ambayo kwa shilingi 1000 tu,
unafungua akaunti hata ukiwa na simu ya kitochi, akaunti ambayo
itakuwezesha kupata huduma zote za kifedha, ikiwemo mikopo, kutuma,
kupokea, kutoa fedha na kulipia bili mbalimbali.
“Sasa, mimi
niwaombe kitu kimoja Wana Mbagala, sisi tupo wengi sana na ‘buku buku’
zipo nyingi sana miongoni mwenu, changamkieni fursa kwa kufungua akaunti
za NMB Pesa ili mujiwekee akiba, lakini mpate kunufaika na huduma za
kifedha za benki hii.
“Hapa kuna droo nyingi zinaendelea kwa wote
wanaofungua akaunti sasa, ambapo watajishindia pesa taslimu, majiko na
mitungi ya gesi, baiskeli za tairi tatu ‘guta,’ na zawadi kubwa zaidi ya
bodaboda ambayo nitaikabidhi mwishoni mwa tamasha hili. Kwa hiyo
changamkieni fursa,” alibainisha.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa
NMB, Bi Ruth Zaipuna, aliwahakikishia Wana Mbagala na Watanzania kwa
ujumla, kwamba NMB imewaletea fursa inayoenda kubadili maisha yao,
kupitia NMB Pesa Akaunti, ambayo ni ya kidigitali unayofunguliwa kwa
Shilingi 1,000 tu, ikiwafikia ikiwa na fursa nyingi.
“Fursa ya
kwanza inayokuja na akaunti hii ni kuwa unaingia moja kwa moja kwenye
Huduma Jumuishi za Kifedha kupitia NMB, watoa huduma wametapakaa kote
kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa sehemu ya huduma hii inayokuja chini
ya kaulimbiu ya ‘Haachwi Mtu.’
“Kupitia NMB Pesa, utakuwa
umeingia moja kwa moja katika huduma ya NMB Mkononi, inayokupa wigo
mpana wa kujihudumia na kuhudumiwa kibenki bila kuja matawini ama katika
ofisi za benki yetu ambako utafanya miamala na malipo na manunuzi
kidigitali.
“Pia, rekodi zako kipesa kupitia NMB Pesa Akaunti,
zitakuongezea fursa, kwani kubwa kuliko yote utaweza kukopa hadi
shilingi 500,000 kupitia Mshiko Fasta, huduma ya mikopo isiyohitaji
dhamana yoyote wala kujaza fomu. Hapo vipi, haujabadilisha maisha yako?
“Mheshimiwa
Mkuu wa Wilaya, hii kampeni tunayoianza leo, ni kampeni ya Weka Akiba
na Ushinde, kwahiyo pamoja kufungua akaunti ya NMB Pesa, lakini pia
tunazindua Kampeni ya Weka Akiba na Ushinde, yaani unaweka 50,000 na
unajishindia zawadi mbalimbali,” alisisitiza.
Bi. Zaipuna
alibainisha kwamba, kila wiki kutakuwa na droo zitakazozalisha washindi
10 wa watakaojishindia Sh. 500,000 kila mmoja, washindi watano wa kila
mwezi watazoa Sh. Mil. 1 na katika droo ya fainali, mshindi
atajinyakulia Sh. Mil. 10, washindi nane wa Sh. Mil. 3, mashine ya
kufulia, tv, friji, bodaboda tano pikipiki nane za mizigo
“Kwa
mantiki hiyo, tunawakaribisha Watanzania wote wajiwekee akiba, lakini
pia wabadilishe maisha na kuboresha biashara zao kupitia akiba na zawadi
watakazoshinda,” alisema Bi Zaipuna alipozungumza na maelfu ya
waliohudhuria tamasha hilo, lililofungwa kwa Agnes Maujundu kujinyakulia
bodaboda ya Sky Mark.




.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment