WANACHAMA wathaminiwa wa AMSHA, Salamu nyingi zilizojaa upendo.
Ni moyo ulioje, kwamba kila mwanachama wa Chama chetu cha wanafunzi waliojaaliwa kupitia shule kongwe yenye kipaji cha kusuka viongozi ya Milambo, CHEM CHEM, anatanguliza kuweka kando muda wake na kuchagua viongozi wa kuleta tofauti katika familia zetu, shule yetu, Taifa na Afrika yetu. Asante sana.
Hakika hii ni hatua ya kimapinduzi. WEWE na mimi, tunaandika historia. Na hii ndio hasa historia yenyewe. NA, AMSHA yetu ingeweza, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu wetu, kuamsha upya moyo unaopungua wa kujitolea katika utume wa kulijenga taifa letu. NDIYO, tunaweza na dhamira zetu zimeelekezwa huko. Kuleta mabadili ya kiuchumi na kijamii kwa WANACHAMA wetu, Taifa na Afrika.
Kwa Neema ya Mungu, tutafufua moyo huo wa kujitolea na kusababisha vyama vya Wahitimu katika nchi yetu kumaanisha biashara kubwa. Tutaviunganisha pamoja na kuwa na mtandao mpana wa TANZANIA na baadaye Afrika, kutokea Milambo yetu.
Kwa hivyo, tumechukua changamoto hii mabegani mwetu. Kwa NEEMA YA MUNGU, iko karibu kutimia. Tuanze kuhesabu.
Ni kwa sababu ya hatua hii ya kipekee katika siku hii iliyorekodiwa, nimejawa na shukurani nyingi za kukonga nyoyo za walio wengi, kunichagua mimi na timu yangu kushika wadhifa wa Mwenyekiti taasisi ya AMSHA. Huu ni uongozi wa kwanza rasmi, baada ya viongozi wa muda kumaliza muda wa uongozi wa mpito. Ninawashukuru sana kwa mafanikio yaliyotufikisha hapa leo. Ahsante sana Wanaume.
Ni kwa sababu ya imani hii mliyo nayo kwangu na kwa Viongozi wenzangu, Mimi, ninawashukuru sana kwa dhati kabisa kwa imani mliyoionesha kwetu. Hili si jambo dogo na tunalipokea kwa umakini mkubwa. Tutatenga muda kwa kazi mliyotupatia. Huenda hata sisi tukaanza kuiuzia umeme TANESCO, ni nani ajuaye, ila, yapo makubwa yanakuja na kila mmoja ni mfaidika.
Mwenyekiti Emmanuel Amasi, umefanya kazi nzuri sana ya kupigiwa mara hii tena. Tazama, kazi yako ni ya kusifiwa, isiyoweza kulinganishwa hata kidogo.
Hakuna mtu angefanya vizuri zaidi. Unastahili sifa zisizo na kipimo. Asante kwa kuandika historia yetu. Nyuma ya pazia lako, ulikuwa na timu ya wabobezi. Ni wanazuoni na watendaji wenye uzoefu na wenye kuaminiwa. Ni watendaji hodari na tena wa kipekee. Profesa David Muwowo, Wakili msomi Mringi Mkucha (Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa NDC), na CPA Nuru Abdallahmed (tuliwasiliana yapata wiki tatu kuhusu TUZO ulikuwa kwenye ziara ya kikazi kwenye mataifa ya Ulaya), hakuna aliyedhani hamtatenda sawa. Tumekuwa na imani kwenu nanyi mmeilinda.
Ninaelewa uchaguzi haukuwa mkamilifu (perfect). Tunauweka ukamilifu kwa Mungu pekee. Johari moja dhahiri yenye thamani iliyoandikwa na kalamu ya dhahabu, ni ukweli unaokubalika na wengi kwamba uchaguzi huu haukuwa huru na wa haki tu, bali pia ulikuwa wa uwazi na wa kuaminika. Asante Wanaume.
Monsieur Jumanne Mwakalinga the Great, mgombea mwenzangu katika nafasi ya Mwenyekiti, asante kwa changamoto uliyonipa kwa takwa la demokrasia. Mimi na wewe tumetokea kusogezwa pamoja. Leo nitakupugia simu. Mimi na wewe sote tumeshinda kwa sababu nitakutegemea sana. Hii inatutia nguvu zaidi tunaposherehekea ushindi wa AMSHA sio wa Murusuri au Mtobela. SOTE TUMESHINDA. Leo, sisi ni muungano kamili na viongozi waliochaguliwa. Hongera. Utukufu wote apewe Mwenyezi Mungu.
AMSHA ingebakia kuwa ni matamanio ya milele, tena butu, laiti isingekuwa mchakato wa urasimishaji kutokea.
Wanachama wote wa AMSHA wanashiriki kipande cha sifa hizi njema. Tumetoka mbali sana. Hata hivyo, itakuwa si haki ikiwa tutajiepusha kuthamini kazi nzuri na iliyojenga msingi wa mafanikio ya leo, bila Katiba ya Chama.
Bila kuandaa katiba nzuri haya yangebaki ndoto. Historia haitawasahau ndugu zetu Wanasheria Wasomi, walioongoza jopo la kutengeneza Katiba yetu. Wakili Msomi Mheshimiwa Evarist Paul Sekaboyi na Wakili Msomi Mheshimiwa Alfred Machumu, historia ya AMSHA tayari imesharekodi. Barabara ingekuwa mbovu na ngumu bila kujitolea kwenu. Sote tunawapigia makofi. Endeleeni kutupatia tafsiri ya kisheria, mnaposhirikiana na Wasomi wenzenu Wana AMSHA humu. Ahsante sana.
Bwana Innocent Mungy, Esq., Mwanafamilia wa TCRA mwenzangu, unatisha Kaka. Ni chini ya uongozi wako, tukawa taasisi inayotambulika. Jina lako, daima, linashuka kwenye kumbukumbu ya uongozi. Tafadhali kuwa karibu nami kwa ushauri ulioombwa au ambao haujaombwa. Sikio langu tayari ni karimu kwako na kwa kila Mwana AMSHA. Ninashukuru pasipo muhali. Asante sana Kaka Inno Prim, Waziri wa Starehe wa enzi zilee.
Sasa Wana AMSHA Wapendwa sana, kwa unyenyekevu mkubwa na mioyo ya unyenyekevu, tunakubali heshima, upendeleo na majukumu tuliyopewa ya kuwatumikia ninyi kwa bidii, kwa UNYENYEKEVU, kwa miaka minne ijayo ya kikatiba, kwa Neema ya Mwenyezi Mungu, chanzo cha maisha na mtoaji wa mahitaji ya kiroho na kimwili.
Najua mnayo matarajio mbalimbali. Vivyo hivyo na mimi. Tunakula kiapo cha dhati cha kuweka ahadi yetu ya kukutumikia kwa bidii, uaminifu, unyenyekevu na upole. Tutaweka uhusiano wetu mzuri kwa kila Mwanachama. Daima tutaweka mbele maslahi ya Chama. Uwekezaji, kuwanufaisha WANACHAMA, wenye uhitaji, misaada kwa shule yetu, kujitoa kwa Taifa letu na Afrika. Yote tumeanza kuyazingatia. Hii kamwe si Serikali ya wanafunzi ambapo tulikuwa tukihudumiwa top layer kwenye state house ya Milambo. Wakati huu sisi viongozi ndiyo tunakuhudumia wewe Mwanachama. Tutakutumikia kwa heshima, uangalifu na unyenyekevu mkubwa. Sisi ni watumishi wako. Nipigie simu au utume ujumbe kwa yeyote kati yetu wakati wowote. KWA PAMOJA TUTAFANYA HIVYO NDUGU.
Kwa hiyo, tunaahidi utiifu wetu katika kujitahidi kuvuka matarajio yenu katika kuendeleza maslahi ya Chama chetu na kujiletea maendeleo kama taasisi, shule, Taifa na Afrika.
Viongozi wenzangu na mimi mwenyewe, katika kipindi hiki cha uongozi wetu, hakika tunawajibika kwenu nyote. ASANTE SANA. Tunatoa shukrani zetu za dhati na kina kwa wale wote waliopiga kura ya NDIYO kwa ajili yetu. Nitakuwa nakosa fadhila ikiwa sitawashukuru kwa dhati wale waliopiga kura dhidi yetu. Ni kwa sababu walitupatia uhalali wa kushinda. Tunapothamini haki yao muhimu ya kidemokrasia ya kufikiria njia mbadala, tunatoa wito kwa kila mtu kufanya kazi pamoja kama ZIXI MOJA LA USHINDI. Sote tulishinda. Yaliyopita si ndwele. Tugange yajayo yanayofurahisha zaidi.
Ni wazi kwamba sote tumeshinda katika uchaguzi huu. Lengo letu limefikiwa. Sasa tuna uongozi ofisini. Basi, tuvunje kambi zetu, kama zipo, na tuimarishe ushirikiano wetu katika kujenga AMSHA imara na yenye kuheshimika.
Viongozi wenzangu wote, nawapongeza kwa kukonga nyoyo na akili za wenzetu. Wana matarajio yao tena makubwa sana. Wana imani na sisi marafiki. HATUTAWAANGUSHA. Wana ushirikiano sana. Hebu tuwarudishie ushirikiano sawa unaojali. Tufanye kazi kupita matarajio yao wakati wa kipindi walichotuamini kukaa madarakani.
Ninaliita jina la BWANA, MWENYEZI MUNGU WETU, ili yeye pekee afanye kazi pamoja nasi, kwa njia ya Malaika na Roho wake, ili kuwezesha timu yote kufikia matokeo hayo ya kustaajabisha kwa manufaa ya WAMILAMBO wote na, WADAU wetu wanaotutaraji.
Tutafanya kila tuwezalo, si tu kuinua hadhi ya Chama chetu juu zaidi, bali pia kutafuta kuwa chanzo cha mawazo mazuri zaidi kuelekea mabadiliko ya miundombinu ya elimu, hasa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Milambo yetu wenyewe na kutuma mawimbi kwa wengine katika nchi hii kubwa. Uchumi wetu ni kipaumbele chetu nambari moja. AMSHA itakuwa taasisi itakayomlea kila Mwanachama.
Tutawasilisha mipango yetu ya muda ya kazi ya kila mwaka ya mwaka wa kalenda 2024 ili kupata maoni na ushauri wenu Wanachama tunapoanza mwaka tukikimbia. Tutaileta ndani ya siku siku 14 kuanzia leo.
Bila kusema, kama nilivyoleta mbele yenu Waheshimiwa Wajumbe, masuala ya ndani, yanayotuhusu sisi na yale ya mbali zaidi, yanayo wahusu wanajumuia pana ya Taifa, Afrika na Dunia, tafadhali niruhusu niwaombe, kila mmoja kwa umoja wetu, kwa dhati, tuweze kukipa Chama chetu taswira bora zaidi kadri tunachoweza kutoa.
Tubakie kuunganishwa kwa dhamira yetu ya pamoja - AMSHA ambayo inapaswa kuamsha na kamwe si kudhoofisha moyo wa umoja katika kujenga jamii iliyobadilika.
Mmoja wa wanafalsafa mashuhuri duniani kutoka Afrika, mwandishi wa kizazi cha wapigania uhuru wa Afrika, Frantz Fanon, anasema...
" kila kizazi lazima, kutokana na kufichwa kwa kiasi, kigundue utume wake, kiutimize, au kiusaliti."
Tunachagua kutosaliti kizazi chetu. Muda wetu uliosalia duniani upate kutumika vizuri. Wakati fulani, tutasimama kushtakiwa, tukiwa tumekufa au tuko hai.
Kinyume na hayo yaliyotajwa hapo juu, kwa Neema na Rehema za Mungu/Allah wetu, naomba mniruhusu kwa mara nyingine tena kuwashukuru Wanachama wote wa AMSHA waliompigia kura mgombea yeyote, bila kujali matokeo na wale ambao hawakufanikiwa kufika kwenye ukuta/kioo cha kupigia kura kwenye simu yako. WOTE ASANTENI SANA. PAMOJA TUTASIMAMA. Milambo Oyee.
MWENYEZI MUNGU NAKUSHI UIBARIKI TANZANIA, NAKUSIHI UIBARIKI MILAMBO NA KIZAZI CHAKE CHOTE. ASANTE SANA. AAMINA.
Derek Kaitira MURUSURI,
Mwenyekiti,
AMSHA.
0787 17 67 67.
Kwa unyenyekevu na upendo wote.
No comments:
Post a Comment