NAIBU Waziri wa Nishati Judith Kapinga ameipongeza Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania kwa kuendelea kutoa huduma bora katika sekta ya biashara ya mafuta nchini huku akiitaka kuendelea kupanua wigo wa kutoa huduma kwa kuongeza vituo vya mafuta nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kutoa tuzo kwa watoa huduma bora mwaka 2023 wa kampuni ya mafuta ya Puma, Naibu Waziri Kapinga ameeleza kampuni hiyo imekuwa ikifanya vizuri na Serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kampuni hiyo iweze kufikia malengo yake.
Pamoja na hayo ameitaka Puma kuendelea kuongeza vituo vya mafuta katika maeneo mbalimbali nchini na hasa maeneo ya pembezoni ambako huduma ya mafuta imekuwa changamoto na hivyo kusababisha watu kununua mafuta kwenye vidumu na kuficha.
"Kwa sasa mnavyo vituo 77 lakini umefika wakati kwa ukubwa wenu katika biashara ya mafuta mkaendelea kujenga vituo vingi zaidi maeneo ya pembezoni ambayo hayana vituo vya mafuta, lakini niwaombe wafanyabiashara ya mafuta msifiche mafuta."
Kuhusu tuzo za Puma mwaka 2023 , amepongeza ubunifu wa kampuni hiyo kuweka utaratibu wa kutambua watoa huduma bora na kuwapa tuzo lakini ametumia nafasi hiyo kuipongeza Puma kwa jinsi ambavyo imeweka mfumo wa kuhakikisha suala la usalama barabarani linapewa msisitizo mkubwa.
"Kwa nyakati tofauti tumeona mkitoa elimu ya usalama barabarani kwa mfano kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi, hili ni jambo nzuri sana kwani inaonesha mnavyorudisha fadhila kwa jamii ya Watanzania, " ameongeza Naibu Waziri Kapinga.
Awali Mkurugenzi wa Puma Energy Tanzania Fatma Abdallah amesema kampuni hiyo inajivunia kuendelea kuwa namba moja katika soko la mafuta nchini kwa kukamata asilimia 20 ya soko lakini kubwa zaidi wanalojivunia ni kuwa na bidhaa bora na iliyosalama.
Kuhusu tuzo za mwaka 2023 ambazo wamezitoa kwa watoa huduma wake amesama zinalenga kutambua na kuthamini mchango wao huku akisisitiza waliopata mwaka huu wanatakiwa kupongezwa na waliokosa wanatakiwa kuendelea kuboresha utoaji huduma.
Mkurugenzi Mkuu Fatma Abdallah amesisitiza kwamba mafanikio makubwa inayoyapata kampuni hiyo na kuendelea kuwa namba moja katika soko yanatokana weledi, kujituma na uwajibikaji unaofanyika vituoni.
Amefafanua watoa huduma wa kampuni hiyo wamekuwa wakiwapatia wateja wao huduma iliyobora kila wanapotembela vituoni, hivyo watoa huduma hao ndilo jicho la kampuni hiyo.
Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga( wa tatu kushoto) akimkabidhi tuzo Mkurugenzi wa Kituo cha Mafuta cha Puma Arusha,Husin Sjat baada ya kuibuka mshindi wa kwanza wa tuzo za Puma Energy Tanzania mwaka 2023.Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Puma Dk.Seleman Majige na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Puma nchini Tanzania Fatma Abdallah.
No comments:
Post a Comment