*Mkurugenzi Mkuu amueleza Naibu Waziri Mkuu jinsi wanavyowafikia wachimbaji wadogo,
*Amesema Mkoa wa Geita pekee walikusanya bilioni 56 kwa mwaka fedha ulioishia juni 2023
Na MWANDISHI WETU, GEITA
Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba,
amemueleza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
kuwa NSSF inashiriki Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya
Madini kwa sababu ndio Mfuko pekee wenye jukumu la kuandikisha wanachama
kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi wakiwemo wachimbaji wadogo wa
madini ili waweze kujiunga na kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao
ya sasa na baadaye.
Mshomba amesema hayo tarehe 23 Septemba, 2023
alipokuwa akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Mkuu alipotembelea banda la
NSSF katika maonesho hayo yenye kauli mbiu isemayo ‘Matumizi ya
Teknolojia Sahihi katika Kuinua Wachimbaji Wadogo Kiuchumi na Kuhifadhi
Mazingira’ yanayoendelea katika viwanja vya EPZA, Bombambili Mkoani
Geita.
Amesema tokea maonesho hayo yalipoanza mwaka 2018, NSSF
imekuwa na mafanikio makubwa kwani ushiriki wake umechangia ukuaji wa
Mfuko ambapo kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2023, walikusanya
michango ya takribani shilingi bilioni 56.
“Wakati Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani, hapa Mkoani Geita
pekee NSSF ilikuwa inakusanya michango ya shilingi bilioni 29 ambayo ni
mara mbili katika kipindi hiki cha miaka miwili na nusu ya uongozi wa
Mheshimiwa Rais, kwa hiyo kwetu sisi ni mafanikio makubwa sana na
tunaamini tutaendelea kufanya vizuri zaidi,” ameeleza Mshomba.
Aidha,
amesema mafanikio ya NSSF kwa ujumla ni mazuri ambapo katika mwaka wa
fedha ulioishia Juni 2023, thamani ya michango iliyokusanywa ilikuwa ni
ya shilingi trilioni 1.66 na katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2022,
thamani ya michango iliyokusanywa ilikuwa ni shilingi trilioni 1.48.
Mshomba
amesema hilo ni ongezeko kubwa na kwamba thamani ya NSSF imeendelea
kukua kwa kasi ambapo kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa mwezi Juni
2022, thamani ya Mfuko ilikuwa trilioni 6.08 na kuwa mpaka kufikia mwezi
Juni 2023 thamani ya Mfuko imefikia trilioni 7.6 kwa hesabu ambazo
zinaendelea kukaguliwa.
“Huo ni ukuaji mkubwa mno hasa
ukizingatia kabla ya hapo na baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kuingia madarakani thamani ya Mfuko ilikuwa ni trilioni 4.8 hivyo
mafanikio hayo ni kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais ya kuvutia
wawekezaji,” amesema Mshomba.
Amesisitiza kuwa, maonesho hayo ya
madini tokea yalipoanza yamekuwa chachu ya ongezeko hilo la wanachama na
michango, ambapo ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Geita chini ya Mkuu wa
Mkoa huo, Mhe. Martine Shigela kwa ushirikiano mkubwa wanaowapatia.
Kuhusu
matumizi ya TEHAMA, Mshomba amesema NSSF imeweka kipaumbele kikubwa
katika matumizi ya TEHAMA ili kurahisisha huduma za wanachama wao jambo
ambalo linaendana na kauli mbiu ya maonesho ya madini.
Mshomba
amesema NSSF inaendelea kusajili wanachama wapya kutoka sekta binafsi na
sekta isiyo rasmi hususan wachimbaji wadogo ambao ndio lengo la Mfuko
kushiriki katika maonesho hayo ya madini.
No comments:
Post a Comment