Na Mwandishi Wetu
Benki
ya NMB imeshika nafasi ya tatu kwa ukubwa wa faida katika ukanda wa
Afrika Mashariki, hii ni kutokana na mafanikio yake kiutendaji hasa
ufanisi katika uendeshaji na utoaji wa huduma bora za kibenki nchini.
Katika
nusu ya kwanza ya mwaka huu benki hiyo imeweza kutengeneza faida baada
ya kodi ya Shilingi Bilioni 262 ikiwa ni ongezeko la asilimia 27
ukilinganisha na nusu ya kwanza ya mwaka 2022.
Kutokana na
kutengeneza kiasi hicho cha faida, NMB imeweza kushika nafasi ya tatu
kwa ukubwa wa faida kati ya mabenki yote ndani ya ukanda huu wa Afrika
Mashariki, ikitanguliwa na Benki ya Equity pamoja na Benki ya KCB zote
kutoka nchini Kenya ambazo zimepata faida ya TZS bilioni 430 na TZS
bilion 264 mtawalia. NMB imepanda kutoka nafasi ya 10 mwaka 2018 hadi
kufikia nafasi ya tatu sasa.
Takwimu na uchambuzi wa hivi
karibuni wa masoko ya hisa katika ukanda huu unaonyesha kuwa taasisi
hiyo kubwa ya fedha nchini yenye mali zenye thamani ya zaidi ya Tsh
Trilioni 11 imekua sana kiushindani na kuimarika sokoni katika miaka ya
hivi karibuni, huku bei ya hisa zake sokoni ikiongezeka kwa takribani
asilimia 28% tangu kutangazwa kwa matokeo yake ya kifedha ya nusu mwaka
2023 hadi kufikia shilingi 4,440 kwa kila hisa Septemba 8 2023.
Kutokana
na kufanya vizuri kifedha, mtaji wa Benki ya NMB katika soko la hisa
umekua kutoka Tsh 1.38 trilioni mwaka 2018 hadi kufikia mtaji wa kiasi
cha Tsh 2.22 trillion Tarehe 8 Septemba 2023, hivyo kuifanya NMB kuwa
kampuni ya pili kwa ukubwa katika soko la Tanzania ikitanguliwa na
kampuni ya TBL na pia kampuni ya sita kwa ukubwa ndani ya kanda ya
Afrika Mashariki, Shelisheli na Mauritus, ikitokea nafasi ya 14 mwaka
2019. Kampuni ya Safaricom Kenya ndiyo inayo ongoza katika ukanda huu
ikiwa na mtaji wa zaidi ya shilingi trilioni nne.
Kwa mujibu wa
Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, mafanikio haya makubwa
yanatokana na mazingira wezeshi ya kibiashara yanayowekwa na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na uimara wa uchumi wa Taifa kwa
ujumla.
Bi. Ruth aliongeza kuwa ufanisi wa taasisi hiyo pia
umechangiwa na miaka mingi ya ukuaji endelevu pamoja na utekelezaji
makini wa mpango mkakati wa uendeshaji wa benki hiyo.
Mwaka 2022,
NMB ilipata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 617 na kuweka
historia ya faida kubwa kuwahi kutengenezwa na taasisi yoyote ya fedha
nchini. Jarida la Euromoney limeitangaza benki ya NMB kama benki bora
Zaidi Tanzania 2023, hii ikiwa ni mara ya 10 ndani ya miaka 11 kwa benki
hiyo kubwa kupata tuzo hiyo inayo heshimika duniani kote.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Dkt. Edwin
Mhede, alisema wamejipanga kuendelea kuchangia kikamilifu ukuaji wa
uchumi wa nchi na ujenzi wa taifa kwa ujumla.



No comments:
Post a Comment