-Yasisitiza kuchukua hatua kuhakikisha uchumi wa nchi hauathiriwi
Na Mwandishi Wetu,
BENKI ya Tanzania (BoT) imesema inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa upatikanaji wa dola na sarafu nyingine na kigeni, na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi yetu hauathiriwi sana na changamoto hiyo ya uhaba wa fedha za kigeni inayoikabili nchi mbalimbali duniani.
Aidha imesema licha ya changamoto hiyo ya kidunia, nchi yetu imeendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni (kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi isiyopungua minne) huku ikifafanua hadi Julai 14 Julai 2023, nchi yetu ilikuwa na akiba ya fedha za kigeni kiasi cha dola za Marekani bilioni 5.55, ambacho kinakidhi uagizaji wa bidhaa na huduma kwa takriban miezi 5.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania( BoT)Emmanuel Tutuba wakati wa mkutano wa wadau wa biashara ya ubadilishaji fedha za kigeni ametumia nafasi hiyo kuzungumzia mwenendo wa upatikanaji wa dola na fedha nyingine za kigeni nchini.
"Mjadala wa leo ni muhimu kwa maslahi ya biashara zenu, sekta ya fedha na kwa uchumi wa nchi yetu kwa ujumla.Katika mkutano huu tutajadiliana juu ya namna bora zaidi ya kusimamia na kuendesha biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali iliyotolewa na Benki Kuu.
"Lengo la kufanya hivyo ni kuongeza ufanisi katika biashara na upatikanaji wa huduma hii muhimu, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi nyingi duniani zimekumbwa na uhaba wa dola ya Marekani, " amesema.
Amefafanua uhaba wa dola ya Marekani umesababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa mahitaji ya dola kutokana na uchumi kufunguka baada ya janga la UVIKO-19; vita kati ya Urusi na Ukraine iliyosababisha kupanda kwa bei za bidhaa na huduma mbalimbali ikiwemo usafirishaji
Ameongeza na hivyo kuongeza mahitaji ya dola; mabadiliko ya tabia ya nchi yaliyosababisha mahitaji makubwa zaidi ya dola; na sera ya fedha ya Marekani
(kupandisha riba) iliyovutia wawekezaji wengi kuwekeza dola zao Marekani na
kusababisha uhaba kwingineko duniani.
Hata hivyo, amesema mafanikio hayo hayatufanyi tubweteke; ndiyo maana wameitisha mkutano huo leo ili wajadiliane namna bora zaidi ya kuwafikishia wananchi wetu huduma ya kubadilisha fedha za kigeni.
"Kama mnavyofahamu mwaka 2018/2019, Benki Kuu kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine za Serikali ilifanya operesheni maalum nchini kwenye maduka ya kubadilisha fedha za kigeni.
"Operesheni hizi zilifuatiwa na uchunguzi uliokuwa na lengo la kubaini maduka ambayo yalikuwa yanaendesha biashara kinyume na Kanuni na Sheria za Nchi. Uchunguzi huu ulisababisha baadhi ya maduka kufutiwa leseni kutokana na kubainika kutozingatia matakwa ya Sheria na Kanuni, " amesema.
Aidha amesema baada ya operesheni hizo, Benki Kuu ilichukua hatua kadhaa ikiwemo kufanya mapitio ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni kwa lengo la kurekebisha mapungufu yaliyogundulika.
Gavana Tutuba amesema katika kanuni mpya za mwaka 2019, mtaji wa leseni ya daraja A uliokuwa Sh.milioni 300 ulifutwa na hivyo kubakiza aina moja tu ya leseni ambayo mtaji wake ulikuwa shilingi bilioni moja, iliyokuwa inatumika kwa leseni za daraja B.
Amefafanua katika kipindi cha matumizi ya Kanuni za Kubadilisha Fedha za Kigeni za mwaka 2019, Benki Kuu imebaini changamoto kadhaa ambazo zimeathiri utoaji wa huduma hiyo nchini.
"Miongoni wa changamoto ni wawekezaji wengi kushindwa kukidhi matakwa ya Kanuni, hususan mtaji wa shilingi bilioni 1, hivyo kusababisha kuwepo kwa watoa huduma wachache. Hali hii imepelekea upatikanaji hafifu au kukosekana kwa huduma hii katika baadhi ya maeneo yenye uhitaji huo.
"Katika kukabiliana na changamoto hii, Benki Kuu ilifanya mkutano na wadau wa biashara ya kubadilisha fedha za kigeni nchini mwezi Januari na Aprili 2023 ili kupata maoni ya namna ya kuboresha mazingira ya biashara hii, " amesema.
Vilevile, Benki Kuu kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikutana na wadau wa sekta ya hoteli Zanzibar mnamo mwezi Januari 2023 na kujadili namna ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni katika maeneo ya hoteli za kitalii.
Amesema baada ya kupokea maoni ya wadau mbalimbali, Benki Kuu ilianzisha mchakato wa kupitia upya Kanuni za Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni za 2019 kwa lengo la kurekebisha baadhi ya masharti ili wawekezaji wengi zaidi waweze kuhamasika kuanzisha biashara hiyo na wale waliokuwepo waweze kurejea katika biashara hiyo
"Marekebisho haya yanajumuisha kupunguza kiwango cha mtaji ili kuwawezesha wawekezaji wengi wazawa kufungua maduka mapya ya kubadilisha fedha za kigeni.Kanuni mpya zinalenga kuweka utaratibu utakaowezesha hoteli za kitalii nchini kutoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni kwa wateja wao.
"Pamoja na marekebisho ya Kanuni, Benki Kuu inaendelea kuhamasisha benki na taasisi za fedha kuboresha utoaji wa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni. Hadi Juni 2023 benki za bishara zipatazo 37 zenye mtandao wa matawi zaidi ya 900 yaliyosambaa nchi nzima yameendelea kutoa huduma hizo."
Aidha amesema jumla ya maduka ya kubadilisha fedha yapatayo 8 yalikuwa yamepewa leseni. Maduka hayo yana jumla ya matawi 36 nchini kote.Pamoja na hali hiyo bado ipo changamoto ya huduma za kubadilisha fedha za kigeni kutokupatikana katika muda ambao zinahitajika zaidi hususan kuanzia saa tisa alasiri, siku za mwisho wa juma (Jumamosi na Jumapili) na sikukuu.
Gavana Tutuba amesema hivyo Benki Kuu inapenda kutoa rai kwa wadau wote kulitazama hili ili kuweza kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma ya kubadilisha fedha kote nchini.
Amesema Benki Kuu itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu elimu ya fedha ikiwemo madhara yatokanayo na ubadilishaji fedha za kigeni kupitia watoa huduma wasio rasmi.
Aidha, Benki Kuu itaendelea kushirikiana na Vyombo vya Dola nchini katika kupambana na wale wote wanajihusisha na biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na leseni rasmi inayotolewa na Benki Kuu.
"Benki Kuu inatoa rai kwa wadau wa sekta hii kutoa ushirikiano ikiwemo kutoa taarifa pale wanapobaini uwepo wa biashara ya kubadilisha fedha za kigeni isiyo rasmi. Benki Kuu imekuwa ikipata taarifa za kuwepo upungufu wa fedha za kigeni katika soko letu.
"Kama nilivyosema hapo awali, ni kweli kuwa kuna upungufu wa fedha za kigeni katika nchi nyingi duniani kutokana na sababu nilizoziainisha.Naomba niwatoe hofu Watanzania kuwa upungufu huo haujafikia kiwango cha kutia hofu kama inavyoelezwa na baadhi ya wadau."
Aidha, Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali na itaendelea kuchukua hatua mahsusi zenye lengo la kuhakikisha kuwa upungufu huo wa fedha za kigeni, ambao upo dunia nzima, hauathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wetu huku akisisitiza wako makini na kwa nguvu za Mwenyezi Mungu watavuka.
Gavana Tutuba ametoa rai kwa wadau hao kuendelea kudumisha ushirikiano huo ili waweze kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo kwa manufaa yetu na taifa letu kwa ujumla.
"Kwa kufanya hivi tutakuwa tunamuunga mkono Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika jitihada zake za kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi yetu unakua kwa kasi na wananchi wetu walio wengi wananufaika na ukuaji huo wa uchumi."
Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba akiongoza kikao cha wadau wa biashara ya ubadilishaji fedha za kigeni pamoja na mambo mengine pia kilihusu mwenendo wa upatikanaji wa dola na fedha nyingine za kigeni nchini.
Baadhi ya viongozi Waandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakishiriki kikao hicho cha wadau wa biashara ya ubadilishaji fedha za kigeni pamoja na mambo mengine pia kilihusu mwenendo wa upatikanaji wa dola na fedha nyingine za kigeni nchini.
Baadhi ya wafanyabiashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni (Bureau de Change) wakiwa kwenye kikao hicho cha majadiliano na BoT Julai 17, 2023.
Baadhi ya wafanyabiashara ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni (Bureau de Change) wakiwa kwenye kikao hicho cha majadiliano na BoT Julai 17, 2023.
No comments:
Post a Comment