Baada ya miezi sita ya uzoefu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kutoa mikopo kwa wasanii nchini, umeingia mkataba na Benki ya CRDB kutanua wigo wa fursa hizo ili ziwanufaishe wananchi wengi zaidi kupitia mtandao wake mpana wa matawina mawakala.
Mpaka sasa, mfuko huo uliozinduliwa Desemba 2022 umeshakopesha shilingi bilioni 1.077 kwa miradi 45 ikiwamo 29 inayomilikiwa na kuendeshwa na wanaume, 12 ya wanawake na kikundi kimoja.
Akizungumza kwenye hafla ya kuingia makubaliano ya mkataba huo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Pindi Chana amesema kwa muda mfupi ambao mfuko huo umetoa fedha hizo, Serikali imeona mahitaji makubwa yaliyopo hivyo kuamua kuipeleka jirani na wananchi.
“Benki ya CRDB ina matawi nchini kote. Tunataka mikopo hii ipatikane kila mahali alipo msanii ili kukuza kipaji chake kwani sasa hivi jamii imeiona faida ya sanaa na wazazi wengi wapo tayari kuwaruhusu watoto wao kuingia kwenye usanii. Kwa mikopo hii kupatikana kwenye matawi ya benki, itawapunguzia wanufaika gharama za kuifuata Dar es Salaam,” amesema Waziri Pindi.
Licha ya kuwapa mikopo, waziri amesema wizara imeanza kuwatafutia wasanii fursa za nje ya nchi ambako wakishiriki matamasha hayo wanajiongezea mtandao wa washirika hivyo kutanua fursa za kipato zaidi.
“Mikopo hii itapatikana kwa riba ya asilimia tisa tu. Hiki ni kiwango cha chini kikilinganishwa na riba zilizopo sokoni kwa sababu Serikali imeweka mkono wake. Nawasihi wasanii popote walipo nchini wajitokeze kunufaika na fursa hii,” amesisitiza waziri.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Abdulmajid Nsekela amesema wanafanya kila wawezalo kuinua ubora wa kazi za utamaduni na sanaa ili ziweze kujiendesha kibiashara na kutengeneza ajira nyingi kwa vijana nchini kwa kuwapa mikopo na mafunzo tangu uliposajiliwa mwaka 2020.
“Kati ya mikopo tuliyoitoa, metoa wanaume wamepokea shilingi milioni 737 huku wanawake wakichukua shilingi milioni 275. Kikundi kimoja kilichojitokeza kimekopeshwa shilingi 10 pamoja na kampuni tatu zilizowezeshwa shilingi milioni 55. Kiwango cha marejesho kinaridhisha kwani ni asilimia 88 na tutazidi kusimamia ipasavyo ili kifikie asilimia 95 inayotakiwa,” amesema Nsekela.
Ili kuwawezesha wanufaika kuzitumia fedha za mikopo inayotolewa kwa malengo yaliyokusudiwa, Nsekela amesema mfuko umetoa mafunzo kwa wadau 7,216 katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Morogoro, Tanga na Pwani na kufanikisha ununuzi wa vitendea kazi kwa vyuo vitano ambavyo ni Simba Scratch Academy, Koshuma Training Institute, Mwanamboka Ujuzi-Hub, Dage School of Dressing na AM Fashion.
“Naomba kuwafahamisha wadau kuwa, mpango huu watakaoushuhudia leo utakuwa suluhisho la changamoto zilizokuwa zinawakumbuka wasanii hivyo nitaomba tuuamini, tuupokee na kutoa ushirikiano ili kutimiza ndoto za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Nsekela ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB.
Akisaini mkataba huo, Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema leo ni siku ya kihistoria kuona mkakati wa unatafsiriwa kwa vitendo kwa kuishirikisha sekta binafsi ili kuwafikia wasanii wengi kadriiwezekanavyo.
“Benki ya CRDB imeingia katika mpango huu kuhakikisha malengo ya mfuko yanafikiwa. Tuna imani kuwa kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, pamoja na taasisi za serikali, tutafanikisha kuyafikia malengo ya mfuko huu. Tumekuwa tukiona jitihada za serikali kujenga mazingira rafiki kwa wadau wa utamaduni, sanaa na michezo ili kuwawezesha kupata matunda ya kazi zao kupitia vipaji walivyonavyo kwa manufaa yao binafsi, familia zao hata jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema Raballa.
Ili msanii apate mkopo ambao ni kuanzia shilingi 200,000 mpaka shilingi milioni 100, Raballa amesemaa atatakiwa kupeleka maombi yake ofisi za mfuko huo zinazopatikana nchi nzima ili kufanya uhakiki wa awali kisha kupendekeza maombi hayo yaende Benki ya CRDB. Ombi likikidhi vigezo, mfuko utalipeleka kwenye tawi la Benki ya CRDB lililo Jirani na msanii husika.
Kwa kukamilisha utaratibu huo, Raballa amesema wasanii wanaojishughulisha na kazi za sanaa na utamaduni waliosajiliwa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Bodi ya Filamu na namlaka nyingine za serikali watakuwa wamejihakikishia kupata mkopo wanaoulenga.
Hata waliomo kwenye vikundi, vyama vya utamaduni na sanaa, vituo vya elimu na mafunzo yanayohusiana na utamaduni na sanaa pamoja na asasi za kiraia zinazojihusisha na utamaduni na sanaa zinaweza kunufaika hivyo wasanii wa filamu, muziki, sanaa za ufundi na maonyesho, lugha na fasii na fani nyingine zenye mlengo wa utamaduni na sanaa.
No comments:
Post a Comment