JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Serikali yatoa shilingi bilioni 3.6 kuboresha miundombinu JKCI

Share This

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimuelezea Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe maendeleo ya ujenzi wa jengo la Utawala na vipimo alipotembelea jengo hilo leo kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya ujenzi.

Na Mwandishi Maalum
SHILINGI  bilioni 3.6 zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suhulu Hassan kujenga jengo la Utawala na vipimo ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Jengo hilo linalotarajiwa kumalizika mwezi Agosti mwaka huu linatarajiwa kutoa huduma za vipimo kwa wagonjwa zaidi ya 200 kwa siku hivyo kupunguza muda wa kusubiri huduma za vipimo na matibabu ya moyo.

Akizungumza alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuangalia maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe alisema kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za matibabu ya moyo Mhe. Rais alitoa fedha hizo ili kuhakikisha kuwa huduma za matibabu ya moyo zinaboreshwa hapa nchini

“Jengo moja lililopo kwa sasa linahudumia wagonjwa wa nje, linatoa huduma za vipimo, kutoa huduma za upasuaji wa moyo pamoja na kulaza wagonjwa hivyo kuleta msongamano mkubwa kwa wagonjwa wanaopata huduma JKCI”, alisema Dkt. Shekalaghe

Dkt. Shekalaghe alisema Wizara inafuatilia hela zinazotolewa na Mhe. Rais ili ziweze kukidhi mahitaji yaliyokusudiwa kwa wakati hivyo kuwataka wakandarasi wa ujenzi huo kufanya kazi usiku na mchana ili ujenzi uweze kukamilika kwani Mhe. Rais anapenda anapotoa fedha zitumike kama zilivyopangwa ili aweze kutoa tena fedha nyingine katika kuboresha sekta ya afya.

“Hadi sasa jengo hili limekamilika kwa asilimia 71, natambua kwamba ujenzi huu upo nyuma ndani ya mwezi mmoja kwani lilitakiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu, baada ya ziara ya leo naomba kusiwe na changamoto nyingene tena kuzuia jengo hilo kukamilika mwezi Agosti”, alisema Dkt. Shekalaghe

Aidha Dkt. Shekalaghe amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI kuhakikisha kuwa vifaa vinavyohitajika katika jengo hilo vinaandaliwa mapema ili jengo linapokamilika mwezi wa nane lianze kutumika hapo hapo na kusiwe na changamoto za kusubiria vitendea kazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kumekuwa na uhaba mkubwa wa ofisi pamoja na vyumba vinavyotoa huduma za vipimo vya moyo hivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotembelea Taasisi hiyo mwaka 2021 kwa ajili ya kuzindua mtambo wa Cathlab akawiwa kutoa fedha hizo lengo likiwa kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo.

Dkt. Kisenge alisema wagonjwa wa moyo wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kupata huduma za vipimo vya moyo hivyo kumalizika kwa jengo hilo kutawapa nafuu wagonjwa kutokusubiri huduma za vipimo hasa upande wa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO).

“Mitambo itakayowekwa katika jengo la utawala na vipimo vya moyo itakuwa mikubwa na ambayo inachukua muda mfupi kutoa huduma za vipimo na majibu ambapo tunatarajia ndani ya masaa mawili mgonjwa anaweza kuwa ameshafanyiwa vipimo, kupatiwa majibu yake, na kumuona daktari”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema jengo la utawala na vipimo litatoa huduma za maabara, huduma za vipimo vya ECHO na ECG, eneo maalum kwa ajili ya wagonjwa wanaotoka nje ya nchi (Medical Tourism), lakini pia kama alivyoshauri Katibu Mkuu Wizara ya Afya kutakuwa na vyumba vya madaktari kwa ajili ya kuwaona wagojwa ili kuwapunguzia mzunguko wagonjwa.

Naye Mkandarasi wa jengo hilo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Baraka Killungu alisema jengo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 1400 lina ghorofa 4 ambapo kila ghorofa lina ukubwa wa mita za mraba kati ya 290 hadi 330.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad