JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Dkt. Samia kuongoza mkutano wa 14 wa TNBC Dar kesho

Share This

 



Na Mwandishi Wetu. Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ataongoza Kikao cha 14 cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kitakachofanyika Kesho (Ijumaa) Ikulu Jijini Dar es Salam.

Katibu Mtendaji wa TNBC Dkt. Godwill Wanga, aliwaambia waandishi wa habari kuwa maandalizi ya mkutano wa 14 wa TNBC yameshakamilika na wajumbe wa mkutano huo wamewasili Dar es Salaam.

“Kaulimbiu ya Mkutano huu ni “Mazingira Bora ya Biashara kwa Uchumi Himilivu na Shirikishi,” alisema Dkt.Wanga.

Kwa mujibu wa Dkt. Wanga, moja ya mambo makubwa yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) au [Blueprint for Regulatory Reforms] nchini ambapo wajumbe watapata fursa ya kujadili mafanikio, changamoto na mapendekezo ya mpboresho ya utekelezaji wake. “Kadhalika mkutano utaeleza jinsi Serikali inavyoshirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha nchi kiuchumi,” alisema.

Dkt. Wanga alisema wajumbe wa TNBC pia watapata nafasi ya kupitia ripoti za utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano wa 13 wa TNBC ambao ulifanyika Jijini Dodoma, tarehe 7 Juni mwaka 2022.

“TNBC chini ya uwenyekiti wake, Dkt Samia, TNBC imepata mafanikio makubwa ikiwemo kuimarika kwa mahusiano na kuaminiana baina ya sekta za umma na binafsi sambamba na kufunguka na kuimarika kwa nchi kibiashara na uwekezaji,” alisema.

Dkt. Wanga alisema mazingira ya biashara na uwekezaji yameendelea kuboreshwa nchini Tanzania. Vikwazo vingi vya kufanya biashara na uwekezaji vimeondelewa na kwa sababu hiyo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt Samia inaaminiwa na wafanyabiashara na wawekezaji ndani nan je ya nchi.

“Mabaraza ya Biashara ya Wizara, Mikoa na Wilaya yaani MPPDs, RBCs na DBCs yamekuwa chachu kubwa ya kuibua fursa za kibiashara na uwekezaji katika uchumi wetu. Na, kupitia mabaraza hayo kero, tozo na makato mbalimbali yaliyokwaza biashara na uwekezaji zimetatuliwa” alisema.

TNBC kimekuwa ni chombo muhimu cha majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kufikia maazimio ya pamoja (Consensus Resolutions) kuhusu masuala ya kuchochea biashara, uwekezaji kwa ajili ya kukuza uchumi na maendeleo ya kijamii kwa ajili ya mustakabali wa ustawi, maslahi mapana na maendeleo jumuishi ya Taifa letu.

Kupitia mikutano ya TNBC, Tanzania kama taifa tumeweza kusonga mbele na kujenga misingi imara ya uchumi, Amani, umoja na maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad