Mjasiriamali na Mtoleaji (Volunteer) Kampeni ya Let’s Do it Tanzania, Fortunatus Ekklesiah (Katikati) akiwaomba Watanzania kujitokeza siku ya mazingira duniani September 15, 2018 katika maeneo yapatayo 33 ya Tanzania. Pembeni ni waratibu wa Nipe Fagio, Catherine Nchimbi (kulia) na Navonaeli Kaniki (kushoto). Picha na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Tanzania itashiriki kwenye Siku ya Usafi Duniani ambayo itafanyika kwa mara ya kwanza Jumamosi tarehe 15 Septemba, 2018. Tukio hili litafanyika chini ya kauli mbiu ya “Let’s Do It”.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam Mjasiriamali na Mtoleaji (Volunteer) Kampeni ya Let’s Do it Tanzania, Fortunatus Ekklesiah amewaomba Watanzania kujitolea kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini na kujumuika na watu zaidi ya milioni 20 katika nchi 150 duniani kusherekea Siku ya Usafi Duniani ya kwanza kwa kusafisha maeneo mbalimbali ya umma hususani fukwe, njia za maji na mito.
Alisema usafi utafanyika katika maeneo 70 kwenye mikoa 16 hapa nchini ikiwemo Dar es salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Dodoma, Iringa, Morogoro, Mwanza, Mtwara, Simiyu, Mbeya, Shinyanga na baadhi ya maeneo visiwani Zanzibar.
Usafi utafanyika katika maeneo 33 yaliyopo katika manispaa zote za jiji la Dar es salaam na maeneo 37 yatafanyiwa usafi katika mikoa mingine. Baadhi ya maeneo ambayo yatafanyiwa usafi jijini Dar es salaam ni pamoja na Tandale Kwa Tumbo, Mto Mbezi, Mwembeyanga, Tabata Magengeni, Soko la Mikindu, na Mto Mlalakuwa.
“Let’s do It! Ni kampeni ya usafi ya kidunia iliyolenga kuondoa taka kutoka kwenye mazingira ya asili. Ni mpango mkubwa zaidi wa watu kufanya shughuli ya kiraia kwa kujitolea kuwahi kufanyika duniani. Wazo hili lilizaliwa nchini Estonia mwaka 2008 na Tanzania inashiriki katika kampeni hii kwa mara ya kwanza mwaka huu,” alisema Ekklesiah.
Nae mratibu wa Nipe Fagio, Navonaeli Kaniki amesisitiza kuwaomba wananchi wote wajitokeze na kujumuika na sisi katika kufanya usafi katika maeneo ambayo yameathiriwa na taka nchi nzima.
“Ushiriki wa kila mmoja ni muhimu kwani mafanikio ya tukio hili yanatokana na jinsi watu watakavyojitolea kushiriki kutokana na mapenzi tuliyonanyo kwa mazingira yetu na Tanzania yetu,” alisistiza.
Lengo la Siku ya Usafi Duniani sio tu kufanya usafi bali pia kuongeza uelewa wa madhara ya tatizo la taka na uchafuzi wa mazingira kutokana na plastiki hapa nchini na kidunia. Vilevile siku maadhimisho ya siku hii yamelenga kuandaa jamii ya kizazi kipya cha viongozi wa jamii ambao wanaweza kufanya kazi kwa pamoja na kumaliza tatizo la taka.
No comments:
Post a Comment