Waziri wa Kazi,Uwezeshaji,Wazee,Vijana,Wanawake na Watoto Mh,Maudline Cyrus
Castico akibeba Watoto Njiti katika Maadhimisho ya mtoto Njiti Duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Baraza
la Wawakilishi la zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee , Vijana ,Wanawake na Watoto Maudline
Castico akizinduwa Kitabu cha huduma muhimu kwa Watoto Wachanga wakati wa
Maadhimisho ya watoto Njiti yaliyofanyika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la
zamani Kikwajuni (kushoto) Naibu Waziri wa Afya Harusi Saidi Suleiman na wapili
(kulia) Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Ali Abdalla.
Na Kijakazi Abdalla - Maelezo Zanzibar. 17/11/2017.
WAZIRI wa
Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Maudline Cyrus Castico amesema
kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa kabla ya kufika wakati (watoto njiti) Zanzibar
imeongezeka kutoka 206 mwaka 2016 hadi
kufikia 335 kwa mwaka 2017.
Akizungumza katika
maadhimisho ya siku ya mtoto njiti Duniani huko ukumbi wa Baraza la Wawakilishi
la zamani Kikwajuni, Waziri Castico alisema kuwa idadi hiyo ni ya kutisha hivyo
jamii inapaswa kufanya juhudi kupunguza tatizo hilo .
Alisema ongezeko
hilo la watoto njiti limekuwa likisababisha vifo vingi vya watoto wachanga hasa
ndani ya siku saba za awali baada ya kuzaliwa.
Aliipongeza Wizara
ya Afya kwa kuchukuwa juhudi kubwa za kuboresha
huduma za afya kwa mama na watoto ambapo hivi sasa huduma hizo zinapatikana kila pahala mijini na vijijini.
Alizitaja huduma
hizo kuwa ni pamoja na kuongeza wataalamu na vifaa muhimu za kuhudumia mama
wajawazito na wakati wa kujifunguwa
pamoja na kusisitiza umuhimu wa kunyonyesha ziwa la mama pekee kwa muda wa miezi
sita.
Hata hivyo
alisema kuwa katika kuhakikisha huduma hizo zinaboreshwa kwa watoto njiti, Wizara
imefanikiwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa wafanyakazi wanaoshughulikia watoto
hao na kwa wazazi.
Alisema jumla
ya wafanyakazi 300 wamepatiwa huduma za watoto njiti Unguja na Pemba ili kuhakikisha
watoto hao wanakuwa katika mazingira ya afya bora.
Mapema Naibu
Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman
amesema kuwa sababu kubwa zinazopelekea kuzaliwa watoto njiti ni pamoja na msongo wa mawazo wakati wa ujauzito,
kujifungua katika umri mdogo chini ya miaka 20 na umri mkubwa zaidi ya miaka
40.
Aliwataka kinababa
kuongeza mapenzi kwa wake zao wakati wa ujauzito
na kuacha kuwatelekeza ili kumpa nafasi kujifungua akiwa salama na mtoto mwenye
afya nzuri.
“Kuna baadhi
ya kinababa wanapogundua wake zao wanaujauzito huona ndio fursa ya kutafuta mke mwengine na
kumuongezea mke mkubwa matatizo zaidi,’’ alisema Naibu Waziri wa Afya.
Alisema kizazi
cha mtoto njiti ni kizazi hai ambacho kinazaliwa kabla ya kutimia umri wa
kuzaliwa hivyo ni muhimu kwa wazazi wote wawili kushirikiana katika malezi
kuhakikisha kinakuwa vizuri.
Nao wazazi wenye
watoto Njiti wamewashukuru wafanyakazi wa
Wizara ya Afya kwa huduma wanazozipata wakati wanapofika vituoni jambo ambalo linawapa
faraja ya kuendelea kuwalea watoto wao katika misingi mizuri.
Hata
hivyo
wamesema wapo baadhi ya watu wanaona kuzaa mtoto akiwana hali kama hiyo
ni mitihani jambo ambalo linawatia huzuni sana hivyo wameitaka
jamii kuondokana na dhana hiyo.
IMETOLEWA NA
IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment