Na Dixon Busagaga wa Michuzi Blog,aliyekua Muleba, Kagera.
JUMLA ya Sh. Milioni 226 zimetumika kwa ajili ya kujenga zahanati katika kijiji cha Ikuza wilayani Muleba mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa Diwani wa kata ya Ikuza, Fortunatus Matta ni kwamba Zahanati hiyo ilijengwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Muleba na Wananchi.
Alisema ili kukamilisha ujenzi huo, TANAPA ilitoa Sh. Milioni 101, halmashauri ikatoa Sh. Milioni 80 huku wananchi wakichangia Sh. Milioni 22.
“Tunaishukuru sana TANAPA kwa kupitia Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, ambayo inapakana na kijiji chetu kwa kuonyesha nia kusaidia mradi huu wa ujenzi kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi wetu,” alisema.
Alisema ujenzi wa jengo hilo kutaleta matumaini kwa wananchi ambao walikuwa wanatumia kilomita 83 kwa ajili ya kufuata huduma za afya kwenye kituo cha Afya cha Kanisa la AICT kilichopo Kasenyi.
Aidha, alisema licha ya jengo hilo kukamilika lakini bado kumekuwa na tatizo la kupata watumishi, vifaa tiba na dawa.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi wa kijiji cha Ikuza, wameishukuru TANAPA kwa kuwajengea Zahanati hiyo.
Mkazi wa kijiji hicho, William Lugaga alisema: “Nashukuru Mungu, hakuna mwanamke yeyote ambaye aliwahi kuzama kwenye ziwa kwa ajili ya kufuata huduma za afya.”
Kwa upande wake, Peragia Samson alisema wakinamama wanapata shida sana wanatumia muda wa saa tatu kwa ajili ya kufuata huduma ya Afya.
“Wakinamama wanajifungulia njia kabla hata ya kufika hospitali na wengine kwenye boti,” alisema.
Naye, Kisanti Joseph alisema naona uchungu kuona wanawake wajawazito wanapotaka kujifungua lazima wapande boti kwenda Kasenyi.
“Kuna wanawake wengine wanajifungulia kwenye boti…hii yote ni kukosa huduma ya Afya,”alisema.


No comments:
Post a Comment