MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imetoa hukumu ya shauri la kikatiba la kupinga vifungu vya sheria ya ndoa, 1971 vilivyokua vinaruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa chini ya miaka 18.
Mahakama Kuu ya Dar es Salaam, Julai 8 mwaka huu kupitia shauri la Rebeca Z Gyumi vs A.G Miscellaneous case No. 5 of 2016, ilitamka kuwa vifungu vya sheria ya ndoa namba 13 na 17 vya sheria ya ndoa vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na kuweka umri wa miaka 18 kama umri wa chini wa kuoa/kuolewa. Vifungu hivyo vilikua vinaruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 14 kwa ridhaa ya mahakama na miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi wake, na hivyo kukinzana na sheria mbalimbali ambazo zinamlinda mtoto.
Mahakama Kuu pia imeipa serikali maagizo chini ya mwanasheria mkuu wa serikali, kuwa imeshabadili sheria hii ndani ya mwaka mmoja na kuweka umri wa miaka 18 kama umri wa chini kwa msichana na mvulana kuindia kwenye ndoa.
Kesi hii ya Kikatiba ilifunguliwa na Rebeca Gyumi, Mkurugenzi wa shirika la Msichana Initiative, linalofanya kazi ya kutetea haki ya mtoto wa kike kupata elimu na kujiendeleza, kupitia kwa wakili Jebra Kambole wa Law Guards Advocate.
Rebeca alikua akidai vifungu hivi vinamnyima msichana haki yake ya kusoma na ni kinyume na ibara ya 12, 13 na 18 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zinatoa haki ya usawa mbele ya sheria, kutobaguliwa , kuheshimu utu wa mtu na haki ya uhuru wa kujieleza.
Hukumu hii imesomwa na Jaji Ataulwa Munisi kwa niaba ya jopo la majaji watatu waliokua wanasikiliza kesi hii. Wengine ni Jaji Kiongozi Shaban Lila na Sakiet Kihiyo.
Jaji Munisi alisema vifungu hivyo ni batili na kwamba vinaenda kinyume na Katiba kwa kuwa mtoto wa miaka 14 hawezi kuingia katika ndoa na hana ufahamu wa kujihusisha na mambo ya ndoa. Jaji pia aliongeza kuwa vifungu hivyo vimepoteza thamani yake na havitimizi tena lengo lilikosudiwa wakati vinawekwa. Hivyo kuamuru umri wa kuolewa uwe kuanzia miaka 18 na kuendelea.
Tanzania ni moja ya nchi zenye idadi kubwa ya ndoa za utotoni duniani. UNFPA wanasema kwa wastani wasichana wawili kati ya watano nchini Tanzania huolewa kabla hawajatimiza miaka 18. Pia wanasema zaidi ya asilimia 37 ya wasichana wenye kati ya umri wa miaka 20 na 24 waliolewa au kuingia kwenye mahusiano ya kindoa kabla ya kutimiza miaka 18.
Ndoa za utotoni nchini Tanzania huathiri zaidi wasichana. Kwa wastani wanawake wa Tanzania huolewa zaidi ya miaka 5 mapema zaidi kuliko wanaume. Sheria ya ndoa, 1971 ilikua inaruhusu mwanaume kuoa kuanzia miaka 18 na wasichana waliruhusiwa kuolewa kuanzia miaka 14.
No comments:
Post a Comment