Nembo hiyo mpya ya TTCL na huduma ya 4G LTE vimezinduliwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa huku akiipongeza kwa hatua hiyo ya kuleta mabadiliko ya kiutendaji na uwajibikaji unaolenga kuonesha tija na ubora. Waziri Mbarawa alisema uzinduzi huo ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli la kufanya kazi kwa bidii, maarifa, uadilifu na kufikia viwango vya juu kabisa vya kutoa huduma kwa umma sambamba na mpango mkakati wa TTCL kibiashara kwa kipindi cha mwaka 2016-2018.
"Pamoja na pongezi hizi za dhati, naomba mtambue kuwa uzinduzi huu hautakuwa na maana yoyote pasipo mabadiliko ya kiutendaji utoaji huduma kwa wateja. Watumiaji wa huduma zenu wanahitaji mabadiliko ya dhati ya viwango vya huduma na utendaji ili kuwajengea imani juu ya uwezo wenu wa kuwahudumia," alisema Waziri Mbarawa.
Kushoto ni Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Bi. Edwina Lupembe akishiriki zoezi hilo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia) akimpongeza, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha Kazaura (kushoto) mara baada ya uzinduzi wa nembo mpya ya Kampuni ya TTCL pamoja na uzinduzi wa huduma ya mtandao wa kisasa wa 4G LTE leo jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Bi. Edwina Lupembe.
Alisema Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano itafarijika zaidi itakapoona huduma za TTCL kimawasiliano zinaongoza nchini huku zikisaidia kukua kwa sekta nyingine zinazotegemea TEHAMA kufanikisha malengo yao. Aidha aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na TTCL ili kuhakikisha inafanikiwa katika malengo yake bila kikwazo chochote, kwani hivi sasa sekta ya Habari na Mawasiliano inagusa shughuli nyingi za maisha ya wananchi ya kila siku, kijamii, kiuchumi na kimaendeleo. "Hivi sasa huduma hizi sio tena jambo la ziada katika maisha ya kila siku bali ni huduma za msingi zenye kipaumbele cha juu katika maisha," alisema Waziri Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto) pamoja na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Bi. Edwina Lupembe (kulia) wakifuatilia hotuba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha Kazaura (hayupo pichani)
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha Kazaura alisema uzinduzi wa nembo mpya ya TTCL unaleta muonekano mpya wa kampuni unaoenda sambamba na mageuzi ambayo yanaendelea katika kuboresha miundombinu ya mtandao wa simu na data. Alisema katika safari ya mageuzi TTCL imefanikiwa kuboresha miundombinu ya simu za mezani na mkononi kwa kuleta teknolojia ya 2G GSM, 3G, UMTS na LTE sokoni ili kwenda sambamba na ushindani wa soko la mawasiliano.
"...Teknolojia hizi zitaisaidia kuongeza ufanisi, ubunifu katika kutoa huduma ya simu za mezani, simu za mkononi na huduma ya intaneti zenye ubora wa hali ya juu na ya uhakika na gharama nafuu," alisema Dk. Kazaura. Alisema kwa sasa kampuni hiyo inaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya mawasiliano ya data nchi nzima, hali ambayo itaongeza ubora wa huduma zetu kwa wateja wetu wote ndani na nje ya nchi.
"...Teknolojia hizi zitaisaidia kuongeza ufanisi, ubunifu katika kutoa huduma ya simu za mezani, simu za mkononi na huduma ya intaneti zenye ubora wa hali ya juu na ya uhakika na gharama nafuu," alisema Dk. Kazaura. Alisema kwa sasa kampuni hiyo inaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya mawasiliano ya data nchi nzima, hali ambayo itaongeza ubora wa huduma zetu kwa wateja wetu wote ndani na nje ya nchi.


No comments:
Post a Comment