Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza neema kwa waendesha bodaboda katika jiji la Dar es Salaam kwa kuwadhamini pikipiki kutoka kwa kampuni zinazofanya biashara hiyo.
Hayo ameyasema leo jijini Dar es Salaam wakati alipokutana waendesha bodaboda kwa ajili ya kuboresha kazi hiyo katika kuwaletea maendeleo ya uchumi, amesema kuwa udhamini wa pikipiki kwa atakayekopeshwa kulipa sh.25,000 kila wiki na baadae kumiliki pikipiki hizo.
Makonda amesema umefika wakati wa vijana kumiliki pikipiki zao na sio kufanya biashara hiyo za watu ambao wanachukua fedha nyingi na wao kuendelea kuwa na maisha magumu.
Amesema tayari kampuni ameshapata ambayo itatoa pikipiki 5,000 kazi ya kuwadhamini haitakuwa ngumu kutokana kila atakayekopa lazima awe katika kituo kilichosajiliwa na kuwa na uongozi kamili.
Makonda amesema kuzuiwa kwa bodaboda mjini huku baadhi bodaboda zikifanya biashara hiyo inatokana na watumishi wachache kumiliki bodaboda hizo na kuwakingia kifua waendeshaji pindi wanapokamatwa.
Katika utatuzi wa changamoto za waendesha bodaboda Makonda ameunda timu ya watu 13 itayofanya kazi miezi mitatu na kuweza kupata ufumbuzi na kazi hiyo ofisi yake itatoa sh.milioni moja kila mwezi katika kusaidia timu hiyo kushughulikia matatizo.
Katibu wa Kamati waendesha bodaboda, Daud Laurian amesema kuwa kuna chama cha kukopa na kulipa kilianzishwa lakini matokeo yake viongozi wamehujumu sh.milioni 50.
Amesema kuwa waendesha bodaboda wamekuwa wakilipishwa faini zisizo na kichwa ikiwa ni pamoja na kuibuka watu wengi kufanya kazi ya kuwakamata ikiwemo na matapeli.
No comments:
Post a Comment