Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akisalimiana na wafanyakazi wa TTCL mkoa wa Morogoro. Mkuu wa Biasahara Kanda, Nyanda za Juu Kusini Juvenal Utafu akitoa maelezo kuhusu utendaji kazi wa TTCL mbele ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akikagua mitambo ya TTCL na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano mkoa wa Morogoro. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akikagua mitambo ya TTCL na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano mkoa wa Morogoro.
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, ameipongeza Kampuni ya simu TTCL kwa juhudi inazofanya katika kutoa huduma za Mawasiliano nchini na kuitaka kutumia kikamilifu fursa ilizonazo ili kujiendesha kibiashara na kutoa gawio kwa Serikali.
Waziri Mbarawa ameyasema hayo Mkoani Morogoro Jumatatu hii alipokuwa katika ziara yake ya kukagua kazi zinazofanywa na Taasisi zilizo chini ya Wizara yake na kutoa maelekezo mbalimbali ya kuboresha utendaji wa taasisi hizo. Ziara ya Profesa Mbarawa katika Kampuni ya simu TTCL ilimwezesha kupata taarifa fupi ya utendaji wa Kampuni ya TTCL Mkoa wa Morogoro kwa mwaka 2015 pamoja na mipango na malengo ya Mkoa huo kwa mwaka 2016 ikiwa ni pamoja na mikakati itakayowezesha kuyafikia malengo hayo.
Aidha Waziri Mbarawa alipata taarifa kuhusu utendaji wa Mkongo wa Taifa wa mawasiliano na changamoto zinazokwamisha Mkongo huo kufanya kazi kwa ufanisi. Uongozi wa TTCL Mkoa wa Morogoro ulimjulisha Waziri Profesa Mbarawa kuwa, kikwazo kikubwa kinachokwamisha utendaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano uharibifu wa kukatwa kwa mtandao wa Mkongo huo kunakofanywa na baadhi ya wakandarasi wa barabara na wakandarasi wanaojenga mkongo wa kampuni ya simu ya Haloteli pamoja maporomoko ya ardhi huko Njombe na Igavisenga.
Akijibu hoja hizo, Profesa Mbarawa aliahidi kushirikiana na Menejimenti na bodi ya TTCL katika kuzifanyia kazi changamoto hizo na kuwataka Wafanyakazi wote kubadilika, kufanya kazi kwa juhudi kubwa na moyo wa uzalendo ili kuiwezesha TTCL kuwa namba moja katika kutoa huduma za Mawasiliano nchini na kumudu ushindani ulipo katika sekta hiyo hivi sasa. Aidha, Waziri Mbarawa aliiagiza Menejimenti ya TTCL kuongeza kasi ya kupanua huduma zote zinazotolewa na kampuni hiyo na hasa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kukidhi mahitaji makubwa ya huduma hiyo na fursa kubwa ya kibiashara iliyopo kutoka kwa makampuni yanayotoa huduma za tehema.
Baadhi ya Wafanyakazi wa TTCL walimuuliza Waziri Mbarawa kuhusu tetesi zilizopo kuwa anakusudia kuanzisha taasisi nyingine na kuikabidhi jukumu la kusimamia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao tangu kuanzishwa kwake, umekuwa chini ya usimamizi wa TTCL ambapo Waziri Mbarawa alikanusha tetesi hizo na kusema kuwa, Serikali ilishafanya uamuzi kwa kuikabidhi TTCL jukumu la kuusimamia na kuuendesha Mkongo wa Taifa wa Mawasiano na hivyo hakuna mpango mwingine tofauti na uamuzi huo.
Waziri Mbarawa aliongeza kuwa kuwa, Serikali itaiongezea TTCL jukumu jingine la kusimamia kituo cha kutunzia kumbukumbu (Data Center) kinachotarajia kuanza kazi muda mfupi ujao pamoja na na kuahidi kusaidia kuiwezsha TTCL kupata masafa ili kuongeza uwezo wake wa kutoa huduma.
No comments:
Post a Comment