JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


TPSF KUZINDUA MFUMO WA HABARI KWA AJILI YA WAFANYABIASHARA WADOGO

Share This
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye akiongea na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa mfumo mpya wa habari uliobuniwa na taasisi hiyo kuwasaidia wafanyabishara ndogo na wa kati kupata taarifa muhimu, ujuzi na huduma za maendeleo ya biashara. Kulia kwake ni Meneja wa Mradi Huo wa Habari, Celestine Mkama. Picha na Cathbert Angelo Kajuna.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye akiongea na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa mfumo mpya wa habari uliobuniwa na taasisi hiyo kuwasaidia wafanyabishara ndogo na wa kati kupata taarifa muhimu, ujuzi na huduma za maendeleo ya biashara. Kulia kwake ni Meneja wa Mradi Huo wa Habari, Celestine Mkama.

TAASISI ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imebuni mfumo maalum wa taarifa kupitia mtandao wa intaneti na simu za mkononi utakaotumiwa na wafanyabishara ndogo na wa kati kupata taarifa muhimu, ujuzi na huduma za maendeleo ya biashara. Mfumo huu utazinduliwa wiki ijayo jijini Dar es Salaam.


Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye amewambia waandishi wa habari kwamba ikiwa ni muendelezo wa jitihada za serikali ya awamu ya tano kuziwezesha biashara ndogo ndogo, kushawishi wananchi kuanzisha biashara na vilevile kurasimisha biashara hizo, mfumo huu utazisaidia biashara ndogo ndogo kutimiza malengo yake.

 Alisisitiza kwamba mfumo huo wa habari ni wa aina ya kipekee kwani unawaruhusu watumiaji wa intaneti kupitia kompyta na simu kutumia na vilevile watumiaji wa simu zisizo na intaneti wataweza kutumia mfumo huu hususani katika kuboresha uelewa wa masuala ya fedha na ujuzi katika ujasiriamali huku ukiwawezesha wajasiriamali kujua namna ya kupata huduma sahihi za kifedha.

 Mfumo huu wa habari umetengenezwa mahususi ili kuwa kituo cha taarifa zote muhimu ambazo biashara ndogo inahitaji kuweza kukua. “Mfumo huu ni rafiki kwa mtumiaji, unapatikana kirahisi, na utawafikia walio na huduma ya intaneti na wasio na intaneti na umelenga katika kuwajengea uwezo wafanyabiashara kupitia taarifa mbalimbali muhimu kibiashara.” 

 Simbeye alisema kuwa mfumo huo wa habari utapunguza vizingiti vya uelewa ambavyo vimekuwa vikifanya biashara ndogo zishindwe kupata huduma na bidhaa za kifedha zitolewazo na taasisi mbalimbali, na vilevile mfumo huu utawapatia wafanyabiashara ndogo jukwaa la kutoa maoni na kujadiliana masuala mbalimbali. 

Hii itasaidia katika kutengeneza sera ambazo zinakidhi mahitaji yao huku mfumo huo ukitoa mafunzo mbalimbali na nyenzo za kufanya biashara. Vilevile mfumo huu wa habari utasaidia kuanzishwa n kuendelezwa kwa mawazo mapya ya biashara na fursa mbalimbali, utaleta fursa kwa watoa huduma za fedha kupata taarifa za soko bure hususani kuhusu mahitaji ya wateja wao. 

 “Uboreshaji elimu kuhusu fedha na ujasiriamali kwa wafanyabiashara wadogo na wadau katika sekta ya ya fedha utasaidia kuleta tabaka la watumiaji huduma waelevu ambao watahitaji kupewa bidhaa na huduma zinazoendana na mahitaji yao ya muda mfupi na muda mrefu, wakati huo huo taasisi za kifedha zikishindana kubuni bidhaa na huduma zinazoendana na mahitaji ya wateja. Vilevile taasisi zinazosimamia huduma hizi na watunga sera wataweka mazingira mazuri kwa kila mdau kunufaika kutokana na huduma za mwenzake. 

Hii ni hali ambayo itampa faida kila mmoja ambapo waombaji mikopo wataweza kuchagua mikopo ipi inafaa kwa biashara zao jambo ambalo litapunguza uwezekano wa kushindwa kurudisha mikopo huku taasisi za kifedha zikiweza kutoa mikopo zaidi na kupata faida zaidi,” alisema. Meneja Mradi wa Mfumo huo wa Habari, Celestine Mkama alisema kwamba baadhi ya huduma muhimu zitakazotolewa na mfumo huo ni pamoja na muongozo kamili juu a kupata huduma za kifedha, kuanzisha biashara, kuendesha na kukuza biashara, msaada wa kitaalamu katika maeneo mbalimbali, majukwaa ya majadiliano, taarifa za masoko na uwezeshaji wafanyabiashara kuyafikia masoko hayo, taarifa za fursa mbalimbali pamoja na mafunzo mbalimbali kupitia mtandao ikiwa ni pamoja na utoaji habari za biashara kupitia machapisho na majarida mbalimbali.

 Mfumo huu wa habari pia utatoa muongozo wa mchakato wa kufanya biashara na sheria husika, taarifa za fedha za nje na utatoa mfano wa nyaraka za kuendesha biashara. 

 Mkama pia alitaja baadhi ya huduma nyingine muhimu zitakazosaidia biashara kukua kuwa ni pamoja na mafunzo juu ya ujasiriamali kupitia mtandao, miundombinu ya kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara kupitia mtandao ambapo wataweza kuuza bidhaa na huduma, na huduma ya mawasiliano ambapo wafanyabiashara wataweza kupatiwa majibu na wahusika kupitia mtandao.

 Vilevile Taasisi ya Sekta Binafsi itafanya vipindi vya redio na warsha za mafunzo zikiwahusisha zikiwahusisha wajasiriamali na wadau mbalimbali nchi nzima ili kuongeza uelewa kuhusu mfumo huu wa habari na kuwashauri wajasiriamali namna ya kuanzisha na kukuza biashara kufata misingi sahihi ya biashara.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad