Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini Bw.Lutengano Mwakahesya akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ambapo zaidi ya Bilioni 435 zinatarajiwa kutumika kutekeleza miradi ya kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali hapa nchini lengo likiwa kuwafikia watanzania wote. kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo bw. Frank Mvungi.
Meneja Wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Bw. Elineema Mkumbo akitoa wito kwa watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali kufikisha nishati ya Umeme kwa watanzania wote kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini Bw.Lutengano Mwakahesya.
Frank Mvungi-Maelezo
SERIKALI kutumia Bilioni 435 kutekeleza Miradi ya kupeleka Umeme Vijijini ikiwa ni utekelezaji wa Malengo yakuhakikisha kila mtanzania anafikiwa na nishati ya hiyo ili kukuza uchumi na kupanua wigo wa uzalishaji.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA)Dkt. Lutengano Mwakhesya wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliolenga kueleza hatua iliyofikiwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kupeleka umeme vijijini.
“Miradi inayotekelezwa hadi sasa kwa awamu ya pili imekamilika kwa asilimia 90 na tunatumaini kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi yote kwa awamu ya pili na yatatu itakapoanza itaongezeka zaidi “ alisisitiza Mwakhesya.
Akifafanua kuhusu idadi ya vijiji vilivyokwishanufaika Mwakhesya amesema kuwa vijiji 5200 vimepatiwa umeme sawa na asilimia 36 ya vijiji vyote vilivyopo hapa nchini ambavyo ni takribani 15,000.
Kwa upande wa kiwango cha fedha zilizotolewa wakati wakala huo unaanzishwa ni Bilioni 10 ambapo zimekuwa zikiongezaka mwaka hadi mwaka ili kufikisha huduma hiyo kwa watanzania walio wengi zaidi.
Akizungumzia Wilaya zilizonufaika na awamu ya kwanza Mwakhesya alizataja kuwa ni Uyui,Kilolo Kilindi na Bahi ambapo kwa Sasa lengo ni kufikisha huduma hiyo kwa wananchi wote.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Nishati Vijijini Bw. Elineema Mkumbo ametoa wito kwa watanzania kutumia fursa ya kuunganishiwa umeme kwa gharama ya 27,000 tu lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa watanzania wengi wanafikiwa na nishati hiyo.
REA imekuwa ikitoa kipaumbele kwenye huduma za jamii kama shule,Hosipitali na Visima vya Maji kwa kutumia sola ambazo ziko kwenya moja ya miradi inayotekelezwa na wakala huo.
No comments:
Post a Comment