JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Muhongo ataka watendaji watangulize maslahi ya Taifa.

Share This
Wajumbe wa mkutano baina ya Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zilizo chini yake pamoja na muwekezaji, kampuni ya Mkonge Energy Systems (MeS) Ltd ya jijini Tanga. Mikutano baina ya wizara hiyo na wawekezaji wa uzalishaji umeme inaendelea chini ya uenyekiti wa Profesa Sospeter Muhongo.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akizungumza jambo wakati wa kikao chake na muwekezaji kutoka kampuni ya Mkonge Energy Systems (MeS) Limited ya jijini Tanga. Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Salum Shamte.
Wawakilishi kutoka kampuni ya Mkonge Energy Systems wakiagana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia). Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa kampuni ya MeS, Juma Shamte akifuatiwa na Mwenyekiti wa MeS, Salum Shamte.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka watendaji wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kufanya kazi kwa kutanguliza maslahi ya Taifa.

Aliagiza hayo hivi karibuni katika kikao chake na wawekezaji wa kampuni ya Mkonge Energy Systems (MeS) Limited ya jijini Tanga kupitia kampuni tanzu ya Tanzania Masigira Power Limited (TMPL) ambao wameonesha nia ya kuzalisha umeme kiasi cha Megawati 71 wilayani Songea mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na kampuni ya China ya Sino Hydro Hong Kong Holding Limited (SHKHL) inayomilikiwa na Power China.

Katika kikao hicho Waziri Muhongo Alizitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha wanashirikiana katika majadiliano mbalimbali ya miradi ya umeme nchini ili kuharakisha utekelezaji wake.

“EWURA na TANESCO fanyeni kazi kwa pamoja ili miradi iende kwa kasi; tulipende Taifa letu na tufanye maamuzi kwa maslahi ya Taifa. Kaeni pamoja mjadiliane na sio kila mmoja kivyake,” alisisitiza.

Alisema kuwa Serikali haitokubali miradi ikwame kwa uzembe na hivyo aliagiza hadi kufikia tarehe 15 mwezi Machi mwaka huu majadiliano kuhusu miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme yawe yamekamilika. “Na ndani ya miezi mitatu ijayo lazima miradi mipya ya kuzalisha umeme iwe imejulikana na kuanza kutekelezwa,” alisema.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Kampuni ya Mkonge Energy Systems (MeS), Salum Shamte alisema kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 2008 baada ya Serikali kutangaza kuwa kampuni binafsi nazo zinaruhusiwa kuzalisha umeme na kuiuzia TANESCO.

Alisema awali kampuni hiyo ilikuwa inazalisha umeme wa maji kiasi cha kilowati 300 kwa matumizi yake ya kiwanda cha Mkonge na kufuatia tangazo hilo la Serikali, ndipo kampuni tanzu ya MeS ikaanzishwa.

Alisema kuwa tayari upembuzi yakinifu umekamilika na kwamba kupitia mradi huo wa Masigira, kampuni tanzu ya TMPL itajenga njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 ya kilomita 14 kutoka Mahanje hadi Madaba ambapo kutakuwa na kituo cha kupoozea umeme.

Aidha, mbali na mradi wa Masigira, Shamte alieleza kuwa wanayo miradi mingine midogo ya kuzalisha umeme ambayo ni mradi wa Kiwira wa Megawati 43.2 uliopo wilayani Tukuyu, Mkoani Mbeya ulio chini ya kampuni tanzu ya Kiwira Energy Limited (KEL) ya ubia wa MeS na kampuni ya Frontier Investment Management ya Denmark. 

Mradi mwingine ambao Shamte aliuzungumzia katika kikao hicho ni mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia mabaki ya mkonge kiasi cha megawati 11.2 ambao alisema upo chini ya kampuni mama ya MeS.


Mkutano huo ni moja kati ya mikutano inayoendelea kwa wiki hii baina ya Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake pamoja na wawekezaji lengo likiwa ni kuwawezesha kupata maelezo ya kina kuhusu fursa zilizopo nchini na pia kuiwezesha Wizara kupata maelezo kutoka kwa Wawekezaji hao kuhusu uwezo wao wa kutekeleza miradi wanayokusudia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad