Msemaji wa Wizara ya Kilimo cha Chakula na Ushirika, Richard Yasini akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya pembejeo za kilimo zenye thamani zaidi ya Sh. Bilioni 78 ambazo zimesambazwa katika mikoa 24 ya Tanzania Bara ili zitumike kufidia gharama ya mbolea na mbegu bora katika msimu wa 2015/2016.Vocha hizo zitawanufaisha wakulima 999,926 wanaojihusisha na kilimo cha mazao ya mahindi na mpunga. Mkutano huo umefanyika leo jijini Dar es salaam kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa MAELEZO, Zamaradi Kawawa.
Baadhi ya waadnishi wa habari wakimsikiliza Msemaji wa Wizara ya Kilimo cha Chakula na Ushirika, Richard Yasini.
Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya Jamii.
Na. Georgina Misama - MAELEZO
WAKULIMA wapatao milioni moja wameanza kunufaika na usambazaji wa vocha za pembejeo za kilimo ambazo Serikali inazitolea ruzuku kwa ajili ya wakulima katika mikoa 24 ya Tanzania bara (ukitoa mkoa wa Dar es Salaam) ili zitumike kufidia gharama ya mbolea na mbegu bora kwa mwaka 2015/2016.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bw. Richard Kasuga amesema kwamba pembejeo za kilimo zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 78 zitawanufaisha wakulima wanaojishughulisha na kilimo cha mazao ya mahindi na mpunga.
“Usambazaji wa vocha hizo umeshaanza, Serikali kwa kushirikiana na makampuni 23 ya mbolea na 27 ya mbegu bora ya mahindi na mpunga yanaendelea kutoa huduma ya usambazaji wa pembejeo katika mikoa husika” amesema Bw Kasuga.
Bw. Kasuga amesema kwamba ili kuhakikisha mbolea na pembejeo zinatumika ipasavyo, Serikali inatekeleza jukumu hilo kwa kugawa majukumu kwa ngazi mbalimbali ikianza na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Kamati ya Taifa ya Uendeshaji wa Utaratibu wa Vocha, Mikoa, Wilaya, Kata mpaka Vijiji.
Akijibu swali la mwandishi aliyetaka kujua Serikali inafanya juhudi gani katika kudhibiti ubora wa pembejeo hizo, Kaimu Mkurugenzi, Mamlaka ya udhibiti wa Ubora wa Mbolea Bw. Lazaro Kitandu amesema toka kuundwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea tatizo la ubora limepungua kwa kiasi kikubwa kwani mamlaka hiyo inasimamia zoezi zima la utengenezwaji na usambazaji wa mbolea na pia wakulima wanapewa elimu ya matumizi sahihi na namna bora ya kuhifadhi.
Aidha, Serikali imetoa rai kwa wakulima kutumia ruzuku inayotolewa ili waweze kujikomboa kiuchumi kwa kuboresha kilimo, na kuwasihi baadhi ya wakulima wanaouza vocha zao wasidanganyike kwa kupokea hela na kuuza haki yao.
Serikali ilianzisha utaratibu wa matumizi ya vocha mwaka 2008/2009 ili kuboresha mfumo wa usambazaji mbejeo kwa wakulima. Utaratibu huu umesaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula, hivyo Taifa kufaidika na kujitosheleza kwa chakula.
No comments:
Post a Comment