Na mwandishi wetu, Dar es Salaam.
WATEAFITI, Watungasera, Wanasheria na makundi mengine ya wataalam wamehimizwa kufanya jitihada ya kweli kuwaepusha wananchi na matumizi ya nishati hatarishi kwa mazingira na badala yake watumie nishati endelevu.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Josephat Itika, alisema Watanzania maskini wanalazimika kutumia nishati hatarishi kwa mazingira na kupunguza kipato chao kwa sababu hawapati nishati endelevu.
“Watu wenye kipato kizuri ndiyo kwa kiasi kikubwa wanaotumia nishati mbadala,” Prof.Itika alitoa wito huo mwishoni mwa wiki jijni Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa siku tatu uliokuwa unajadili namna ya kufikisha teknolojia za matumizi ya nishati mbadala kwa wanavijijini.
Prof. Itika aliwahimiza wanataaluma na watafiti kufanya bidii ya kuboresha upatikanaji, uhifadhi na utumiaji wa nishati endelevu kwa Watanzania maskini ili hata wao wakuze kipato chao na kuinua uchumi wa taifa.
Alisema mkutano huu uwe chachu ya kumkomboa mwananchi maskini ili aweze kutumia nishati mbadala na endelevu.
“Tumepata bahati kubwa ya kukutanisha wanataaluma na watafiti. Basi tuangalie namna ya kuboresha upatikanaji, uhifadhi na utumiaji wa nishati mbadala kwa watu wenye kipato cha chini kabisa na kwa bei nafuu,” amesema
Mratibu wa Mradi wa ENRICH Tanzania unaojihusisha na matumizi ya nishati mbadala, Dkt. Joseph Sungau, alieleza kuwa ushahidi unaonyesha kuwa maeneo mengi ya Tanzania yana fursa za kuwaruhusu wananchi kutumia nishati mbadala na endelevu.
“Nashauri zifanyike tafiti ili Watanzania watumie nishati endelevu katika viwanda vikubwa, vidogo na majumbani kwa kutumia vyanzo ambavyo havijazoeleka sana katika kupata nishati,”Dkt.Sungau alisema.
Amesema mkutano umeandaliwa ili kuwakutanisha watafiti , watunga sheria na wadau wengine wa mambo ya nishati kujadili maswala ya kiteknolojia ili watu wengi wapate nishati ambayo itawakomboa kiuchumi.
Dkt.Sungau alivitaja vyanzo vya nishati endelevu ambavayo vinapatikana sehemu nyingi za Tanzania kuwa ni upepo wa kutosha unaovuma, maporomoko ya maji na jua kali kwa wingi.
Mkutano huu umeandaliwa na Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Alicante cha nchini Hispania na kuhudhuriwa na washiriki kutoka nchi za Uganda, Kenya, Spaniola na Tanzania.
No comments:
Post a Comment